Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, ukizingatia hili ni Bunge la mwisho la kipindi changu cha kukaa Bungeni nikiwakilisha wananchi wa Jimbo la Mlimba. Nawashukuru Watanzania wote na wananchi wa Jimbo la Mlimba kwa kunipa ushirikiano katika kipindi changu chote cha miaka hii mitano kasoro.

Mheshimiwa Spika, namshukuru vile vile Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kuniamini mara ya pili; katika kipindi kilichopita nilikuwa Naibu Waziri Kivuli wa Wizara ya Maji, sasa hivi nimekuwa tena Naibu Waziri Kivuli wa Wizara ya Ujenzi. Nakushukuru pia kwa kuwaamini wanawake wengi ndani ya chama chetu na Kambi yetu. Kweli wanawake tunaweza bila kuwezeshwa bali tukipewa fursa.

Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia bajeti yangu hii ya mwisho kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye kipindi hiki cha Bunge. Ningeweza kuchangia mambo mengi sana kama kawaida yangu, lakini inapotokea dharura ama shida katika nchi, ni vyema nikajielekeza katika shida iliyopo ndani ya nchi yetu hususan kwenye huu ugonjwa huu wa Corona ambao ni muhimu sana tukauchangia kama Wabunge kuangalia hali za maisha yetu na wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa pole kwa wananchi wote ambao wamepatwa na maradhi haya ndani ya nchi yetu na wengine ambao hatujapimwa, hatujui afya zetu, lakini vilevile nitoe pole kwa ndugu wa marehemu ambaye alikufa ndani ya nchi yetu na akazikwa na Serikali. Huu ugonjwa ni hatari.

Mheshimiwa Spika, bajeti ya Waziri Mkuu ni bajeti ambayo inaenda kuangalia Wizara zote. Vilevile tumejionea wenyewe ndani ya nchi hii mabadiliko ya hali ya hewa ya nchi yetu hasa ndani ya mkoa wa Morogoro hususan ndani ya Bonde la Kilombero, Ulanga na Malinyi.

Mheshimiwa Spika, hili bonde lilikuwa linatoa mazao mengi sana, lakini mwaka huu kulingana na mvua zilizoanza mapema, hakuna mkulima aliyepanda mpunga. Walikuwa wanasubiri angalau mvua hizi za mwanzo zilizoanza ziishe ndiyo wapande, lakini mpaka sasa ninavyozungumza, bonde lote limejaa maji, hakuna mkulima ameweza kupanda. Kwa hiyo, hali ya hatari ndani ya bonde letu inaweza ikawa hatari zaidi jatuja suala la njaa.

Mheshimiwa Spika, hivyo basi, napenda kushauri, kwa bajeti hii ya Waziri Mkuu, Serikali iliangalie hili na kitengo chake cha maafa, kitengewe fedha za kutosha kuokoa hali ya Watanzania hususan wananchi wa Mlimba na Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Spika, hali ya ugonjwa bado iko tete, hata hivi karibuni nimetoka kuongea na Mkurugenzi wangu kujua amefanya nini katika kujikinga na hiyo hali kuanzia maofisini mpaka kwa wananchi, kwa sababu yeye ndiye anayekusanya mapato ya wilaya zetu. Alichonijibu, anasema ni kweli ameweka maji na sabuni na nikamsisitiza kwamba ni muhimu sana kununua na sanitizer hasa katika maofisi kwa sababu mtu anaweza asinawe maji lakini akiwa na sanitizer itamsaidia zaidi katika kushika vitabu na mambo mbalimbali hapo ofisini na amenikubalia anasema atafanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, hali ni tete. Sasa kama sisi hatujapimwa: Je, hali kwa Watanzania ikoje? Nakumbuka Mheshimiwa Kaimu Kiongozi wa Kambi, Mheshimiwa Halima Mdee, aliomba angalau tuanze na sisi Wabunge tuangalie afya zetu sisi ambao tunawakilisha wananchi, tuone hali halisi halafu twende kwa wananchi vile vile.

Mheshimiwa Spika, hili suala linatakiwa liwe nchi nzima kuwe na mafungu ya kutosha, kuwe na vitendanishi vya kutosha ili tupime afya za wananchi wetu tunapochanganyikana tuonekane kwamba tumeshapima. Hii kupima tu kwa kipima joto, kwa kweli mtu anaweza akanywa Panadol na akija hapo akakutwa joto limeshuka kwa dakika chache, lakini hali inakuwa siyo nzuri. Kwa sababu dalili zake ni nyingi, siyo kukohoa tu; mtu unaweza ukaanza kupandwa joto lakini Corona ndiyo unayo na bado hujaanza kukohoa. Sasa tunavyojiaminisha kwa kujipima tu joto, naona siyo sawa kabisa.

Mheshimiwa Spika, hiyo hali ni muhimu tukaiona na kwamba kuwe na bajeti ya kutosha katika Kitengo cha maafa ili tuone namna gani tunaenda na milipuko inavyotokea ndani ya nchi yetu. Siyo hiyo tu, katika Wizara ya Afya kama ilivyosema, kwamba ni asilimia 15 tu ya bajeti iliyotekelezwa. Je, sasa Serikali inakuja na mpango gani mahususi kuhakikisha kwamba hela ya kutosha inatengwa katika hii Wizara ili inapotokea mambo ya mlipuko tusitegemee tu misaada na sisi wenyewe tuwe na uwezo wa kujikinga? Leo unasikia kwamba hapa ni Mloganzila ndiyo wameweka, labda Waziri Mkuu alitembelea Kibaha.

Mheshimiwa Spika, je, unaonaje sasa huku vijijini kwetu? Kwa mfano, Jimbo la Mlimba kuna treni, kuna wakulima, wafanyabiashara wanatoka Dar es Salaam, wanatoka Tanzania nzima wanaenda kule, lakini wananchi wa kule hawajui hali halisi ya ugonjwa huo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kupimwa na wananchi katika vijiji vyetu na katika maeneo yetu na kuweka hizo tahadhari na hospitali kila wilaya au kule tusiokuwa na Hospitali za Wilaya, kwenye zile Hospitali za Kata ambazo ni Vituo vya Afya, kuna haja kabisa ya kuweka emergency ili tunapopata mgonjwa kwa dharura tuwe tunajua tunampeleka wapi? Siyo kama ilivyo sasa hivi, watu tumekaa tu, hatuelewi kitu gani kinaendelea, utafikiri hatuko duniani, tumejifungia hapa.

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie katika hotuba hii ya Waziri Mkuu kuhusu masuala ya NIDA. Pamoja na kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani amesema NIDA sasa hivi wana mashine, wana hela, lakini hali halisi ikoje ndani ya Wilaya ya Kilombero hususan Jimbo la Mlimba? Wananchi wa Jimbo la Mlimba hawana uwezo wa kupata vitambulisho hivyo vya NIDA kwa sababu hawana cheti cha kuzaliwa wala hawajamaliza la Darasa la Saba.

Mheshimiwa Spika, wako wengi, watu wamezaliwa huko mashambani au machungani, hawajasoma, lakini ni Watanzania wanaotakiwa wapate hizo laini za simu na vyeti. Sasa hivyo hali, naomba kama alivyosema, siyo mipakani tu, watambuliwe na vijiji, hata kwenye vijijini kwetu Wenyeviti wa Vijiji na Mikutano ya Vijiji iwatambue hawa wananchi kama kweli ni Watanzania, wapewe barua ili wapate kujisajili kwenye NIDA. La sivyo, watakaa hivyo, wataonekana siyo Watanzania ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, hiyo ni muhimu sana na bajeti vilevile ilikuwa ndogo hawajafika kabisa watu wa NIDA ndani ya Kata za Mlimba. Kati ya Kata 16, wamefika Kata mbili tu, Kata 14 hawajafika. Naomba hilo lichukuliwe kwa uzito, waende wakasajili watu ili wapate hivyo vyeti.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa uchaguzi tumeshuhudia, mimi mwenyewe nilikuwa kwenye uchaguzi mdogo Sofi, hali ni mbaya, tunahitaji Tume Huru ya Uchaguzi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ni dakika 10!

SPIKA: Eeh, ukiangalia hata saa yako.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mbona mimi saa yangu iko tofauti!

SPIKA: Haya malizia sentensi ya mwisho.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, yaani dakika saba tu ndiyo mimi nimeongea.

Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchaguzi ndiyo amani ya nchi hii. Bila kuwa na Tume ya Uchaguzi, tunaingiza nchi katika hatari kubwa. Leo tunacheka tuko hapa, lakini hakuna mtu atakayevumilia kuona anaporwa, kuona anafanyiwa vitu vya ajabu, wakati ametimiza masharti halafu tume inakuwa ya mtu mmoja, anateua mtu mmoja.

Mheshimiwa Spika, Katiba iko wazi, tunahitaji Tume Huru ya Uchaguzi ili kuzidisha amani ndani ya nchi yetu. Bila haki, amani haitakuwepo. Haki ni tunda la amani ndani ya nchi yetu. Tusifanye mzaha tukatekeleza kizazi, amani haitakuwepo na miundombinu tunayoifanya ni sawasawa na bure. Naomba sasa Tume Huru ya Uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, mlete sheria, turekebishe vipengele na Bunge ndiyo hili ili twende kwenye uchaguzi salama. Chadema hatuhitaji uchaguzi usogezwe mbele hata sekunde moja. Tunataka hata leo ukitangazwa uchaguzi tuingie kwenye uchaguzi na Tume Huru kwa sababu uwezo tunao, tumejipima tunaweza na kwenye chaguzi ndogo mlishuhudia. Tulishinda, mkatupora. Watanzania hali haijabadilika, hali ni mbaya. Tunaomba Tume Huru ya Uchaguzi, Katiba iseme wazi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Ninyi Makatibu wa Mezani, acheni mambo yenu hayo!

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Suzan. Nakushukuru sana kwa mchango wako.

Whoops, looks like something went wrong.