Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Ahmed Juma Ngwali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ziwani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, lakini niombe Waziri wa Fedha hayupo lakini na Naibu wake anaendelea kufanya mazungumzo kwa hiyo hana concentration ya hiki ambacho nataka kuzungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwekezaji yeyote ili awekeze katika nchi lazima awe amepata mambo mawili; malighafi au soko. Mheshimiwa Rais ametembea Tanzania nzima kuhamaisha watu wajenge viwanda, Mheshimiwa Rais ana nia nzuri sana na mapinduzi ya viwanda, lakini tuna mifumo Tanzania ambayo Mheshimiwa Rais anahamasisha viwanda lakini hiyo mifumo inaua viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, tuna mfumo wa stakabadhi ghalani, mfumo huu unaendeshwa kwa utaratibu wa auction kwa maana ya mnada, lakini ule mnada unaruhusu hata wanunuzi kutoka nje wanunue ile malighafi, kwa mfano korosho. Sasa unapokuwa na international mnada ule ukawachukua watu waliojenga viwanda, ukawahusisha na wanunuzi wa nje, watu waliojenga viwanda hawawezi kununua malighafi kwa sababu hawawezi kushindana bei na mnunuzi wa nje. Kwa hiyo viwanda vinajengwa lakini malighafi ile kwa mfano korosho inachukuliwa inakwenda nje. Sasa maana yake nini; maana yake viwanda vinakufa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni lazima tutafute utaratibu, na nashauri tutafute utaratibu ambao tutakuwa tuna minada miwili ambapo mnada mmoja utawahusisha kupata malighafi viwanda vya ndani lakini mnada wa pili utahusisha viwanda vya nje na mambo mengine. Hilo jambo la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kahawa, mwaka jana tu walijaribu kutaka ku-adapt mfumo wa stakabadhi ghalani, uliwagharimu sana. Viwanda vilijengwa, viwanda vipo vipya kabisa wakati wa ununuzi wa kahawa, kahawa ikanunuliwa na Vyama vya Ushirika, walipokwenda kutaka kununua kahawa wakaambiwa waende kwenye auction, walipokwenda kwenye mnada wanataka kuuziwa kahawa iliyokobolewa. Sasa nini maana ya kujenga hivi viwanda? Kwa hiyo tunaposema mapinduzi ya viwanda tuwe na utaratibu sasa wa kulinda hivi viwanda ili hizo malighafi zinazozalishwa Tanzania tuzipate.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, tunataka kukusanya kodi, kumetokea wajanja wachache wametengeneza programu inaitwa PVoC, PVoC ni programu ya kufanya ukaguzi wa bidhaa nje ya nchi, programu hii ilianza mwaka 2012 kama sikosei. Programu hii inamfanya TBS ambaye ndio Wakala wa Serikali katika ukaguzi huo imechukua mawakala, imeingia mkataba na mawakala, Bureau Veritas, CoC, wameingia na Intertek, wameingia na SGS. Hawa wanakagua bidhaa nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba bidhaa zile hazikaguliwi nje ya nchi. Mimi nimekwenda Japan, nimekwenda China, ukaguzi hakuna, lakini ili ukaguliwe lazima upate certificate ya TBS ya nchi husika. Sasa kinachofanyika, wao wakishapata ile certificate ndiyo wanakuandikia zile documents kwamba umekaguliwa lakini ukweli hawakaguliwi na unalipa dola 800. Sasa kwa nini tulipe dola 800 nje tusifanye direct inspection hapa Tanzania tukalipa dola 800 hapa? Wale mawakala wa kazi gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nadhani kama huu unaweza kuwa ni mradi wa mtu. Kuna watu wana miradi yao na hakuna kontena ya biashara inayokuja Tanzania ambayo haina certificate ya CoC. Kwa hiyo hebu chukua containers elfu tatu kwa mwezi na kwa mwaka ni containers ngapi halafu hizo fedha zinalipwa nje ya nchi. kwa hiyo tunakosa mapato, Serikali inakosa mapato bila sababu na dhamira ya PVoC ilikuwa ni kuzuia bidhaa bandia zisiingie nchini, lakini bidhaa bandia zimeongezeka baada ya huo mfumo. Kwa hiyo hata hiyo dhamira haipo na fedha zinapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la nne, Mheshimiwa Waziri, amekuja ni vizuri; East African Comon Tariff wamefanya jambo jema sana; wamekwenda wameweka kodi kwa ajili ya kulinda viwanda vya ndani lakini kukuza biashara katika Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki. Hata hivyo, wanapofanya hivyo wanasahau kitu kimoja; Zanzibar inategemea exportation asilimia 95, maana yake ni kwamba waki-copy kodi ambazo zimewekwa Afrika Mashariki maana yake Zanzibar hawawezi kuingiza bidhaa. Kwa hiyo ushauri ni nini; wanapofanya haya mambo Mheshimiwa Waziri wachukue walau Waziri wa Fedha wa Zanzibar wakae pamoja, otherwise Zanzibar ni lazima wafanye magendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tano, nimetazama katika vitabu vya Mheshimiwa Waziri vya miradi ya maendeleo, vya mipango sikuona kitu kimoja; tumejenga flyover ile pale TAZARA tumeondoa foleni pale tumepeleka foleni kule Vingunguti.

Mheshimiwa Spika, tutafungua Terminal Three kesho kutwa; tuna Terminal One, Terminal Two na Terminal Three; bora utoke South Afrika inaweza kuwa ukafika mapema kuliko kutoka pale mpaka Hyatt Regency Kilimanjaro. Sasa kwa nini Serikali isitoe Branch ya Standard Gauge ikapeleka moja kwa moja Airport ili tufanye usafiri wa kwenda Airport ukawa rahisi? Kwa sababu kwa sasa ikifunguliwa na hiyo Airport mpya maana yake traffic itakuwa ni kubwa sana. Kwa hivyo niiombe Serikali itafute utaratibu wowote unaona ambao unafaa lakini tuhakikishe safari za kutoka katikati ya mji kwenda Airport ni rahisi kiasi kwamba kila mmoja anaweza kwenda kwa wakati ambao anautaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho; sitaki niseme mengi; kwanza natambua uwepo wa Comrade Shamsi Vuai Nahonda Waziri Kiongozi wa zamani wa Zanzibar; lakini niseme kwamba tuna miradi ya maendeleo yanayohusu watu wa Zanzibar. Mheshimiwa Waziri Wizara ya Fedha imekuwa kikwazo sana kwa sababu hata wewe mwenyewe; Mheshimiwa Waziri wa Fedha sijui kwa nini hatupendi Wazanzibar. Kuna barua hii aliandikiwa kabisa na Saudia Fund for Development; hii ni original kabisa. Napenda Mheshimiwa; mpe aone ubaya wa Mheshimiwa Waziri Mpango.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiisoma utaona namna gani alivyokuwa hatupendi, ana roho mbaya kabisa. Mradi wa bilioni 26 BADEA walishasaini kwa miaka mitano nyuma, barua umeletewa hata kujibu hujajibu, basi si ujibu kwamba haiwezekani? Au kama haiwezekani basi tukopesheni ninyi Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Mnajua kwamba Zanzibar hawawezi kukopa kwa sababu hawana sovereign guarantee, wanaokopa ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa niaba ya Zanzibar, wewe unajua hilo. Kwa hiyo Mheshimiwa Mpango hebu tukuombe, hii barabara ni barabara muhimu sana kwa sababu Pemba kule tuna barabara moja tena imebomoka. Phase one mmefanya vizuri mmetutengenezea barabara tuwanashukuru, lakini tukubali hii barabara ya Wete Chake imalizike usitufanyie hivyo bwana. Mheshimiwa Mpango nitizame maana unaandika hunitizami kama vile kwamba hili jambo hulitaki kulichukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.