Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru Mungu kupata nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu sana kwa Taifa letu la Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na bajeti, hii nafikiri ni ya nne na sisi Kambi Rasmi ya Upinzani tumetoa mawazo mbadala kuweza kusaidia Taifa letu kusimamia masuala ya uchumi. Tunashukuru kuna wakati mnakubali kuna wakati mnakataa lakini mwisho wa siku Watanzania watajua kwamba sisi tulikuwa tunatoa mawazo kwa ajili ya kusaidia Watanzania wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti zinapotangazwa nchi za Afrika Mashariki kwa siku moja inasomwa na hii imefanywa kimkakati sawasawa na tulivyosaini kama nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nchi ya Kenya imeweka bajeti yake kiasi cha dola bilioni 30.2. Naizungumzia Kenya kwa sababu mimi binafsi naamini vitu vingi sana tunavyofanya sisi wenzetu wanatuangalia tunafanya nini na sisi pia tunawaangalia wanafanya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti yetu imefika shilingi trilioni 33, wakati wenzetu bajeti yao ukichukua Burundi, Rwanda, Uganda na nchi zingine za Afrika Mashariki, Kenya peke yake imetuzidi. Kwa nini nazungumzia hilo? Soko lililopo hapa nchini ukienda kwenye spices zote kwenye maduka ya jumla vifaa vya Kenya vimejaa hapa nchini na sisi kama nchi ya Tanzania tunajinasibu ni nchi ya viwanda kwa miaka hii minne hizi bajeti tumezizungumzia ni kitu gani ambacho tumezalisha na kimeuzika katika soko la Afrika Mashariki kama wenzetu walivyofanya? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango na timu yake nzima ni lazima tufanye kazi kimkakati ili kuweza kuinua uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wenzetu wanatangaza bajeti yao sisi Waziri wetu Mheshimiwa Dkt. Mpango anazungumzia tunaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni mtu gani achaguliwe atoke CCM. Wakati huu siyo wa kuzungumzia mambo ya vyama ni wakati wa kuzungumzia mustakabali wa Taifa hili hasa katika mambo ya kiuchumi. Kwa hiyo, naomba Msomi Mwalimu Mheshimiwa Dkt. Mpango simamia sehemu uliyopewa na wananchi lakini na Mungu amekupa hiyo nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna vipaumbele kama Taifa. Katika kipaumbele cha kwanza ambacho nimekisoma kwenye kitabu cha Mheshimiwa Dkt. Mpango amezungumzia suala la kilimo na viwanda. Kinachonishangaza asilimia 40 ya mapato na mgao umeenda kwenye nishati na ujenzi. Kipaumbele ni kilimo ambacho kina asilimia zaidi ya 70 ya Watanzania hawana pembejeo za kutosha, masoko ya mazao yao hata wakilima na network ya hiyo East Africa tunayoizungumzia ya kupeleka bidhaa. Matokeo yake Wakenya wamewekeza maparachichi kule kwetu Rungwe na Mbeya wanalima na wanapeleka kwao wanafanya packing wanaenda kuuza nchi za nje Sweden na sehemu mbalimbali, wakati wananchi wetu sisi wa Tukuyu wanaendelea kuuza kwa bei rahisi maparachichi hayo. Ukisema kipaumbele chako ni kilimo au viwanda tunategemea bajeti uliyoipanga asilimia hiyo 40 ungeiwekeza huko ili iweze kuwa na tija na manufaa kwenye Taiga letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi bado nashangaa Mafisa Ugani katika kilimo ni wachache. Kwa mwaka wa nne sasa ajira hazijakuwepo kupata Maafisa Ugani wa kutosha katika kilimo. Masoko kama nilivyosema, tunatumia SIDO wakati mwingine wanajitahidi kutangaza masoko madogo lakini haya masoko ni watu gani wanapata taarifa kwa wakati? Tumesaini mikataba mbalimbali, biashara kwenda AGOA, watu wetu wanazo hizo taarifa? Tunahitaji kubadilika na hasa kuhakikisha wakulima wanatendewa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mbegu zinazouzwa sasa hivi ziko chini ya kiwango. Je, watafiti tulionao, tuna Chuo cha Uyole, SUA, Serikali imepeleka kiasi gani cha pesa ili waweze kufanya utafiti na kuweza kuwasaidia hawa wakulima kutoa mazao bora na yenye tija katika soko la kidunia? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Chuo cha Uyole hakijapata pesa za maendeleo kwa muda mrefu sana na huwezi kuendelea bila kuwekeza kwa watafiti au kwa hawa wataalam. Tuna mazao ya ng’ombe wale wanaozalisha mitamba, vifaa vya kutosha hawana then unafikiria unaweza ukashindana na nchi kama ya Kenya ambayo leo hii wametuacha kwa mbali sana katika bajeti yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweka tozo nyingi sana ambazo naziita tozo za kuudhi. Mheshimiwa Mbunge mmoja alizungumza jana juu ya peremende na sausage na vitu kama hivyo, wenzetu Wakenya wametazama matumizi ya simu, Wakenya wengi wanatumia simu za mkononi wameona ni bora kutoka asilimia 10 ya tozo waliyokuwa wanadai wamepeleka asilimia 12 angalau zile asilimia 2 pesa inayopatikana iende kwenye afya. Hizo ndiyo akili za kufanya kwa sababu kutokuwa na simu hutakufa, kwa hiyo, kama unataka kuwa na matumizi ya simu basi simu yako utakapotumia pesa inayopatikana ikasaidie afya na hasa mama na mtoto katika Taifa lao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hicho hicho kilimo, pesa za maendeleo bajeti iliyopita shilingi bilioni 98 zilitengwa na Bunge lilipitisha lakini ni kiasi kidogo sana cha shilingi bilioni 41 zilikwenda. Sasa unawezaje kufanya maendeleo wakati pesa ambayo umeitenga haijafika kwa wakati na kuweza kufanya kazi iliyokusudiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipaumbele cha pili tumesema ni ukuaji wa uchumi wa Mtanzania. Mtanzania huyo atakuwaje kiuchumi wakati wanafunzi hawapati kwa wakati mikopo, tunatengeneza vijana wa aina gani na ni uchumi gani tunauzungumzia? Tumesema vijana wanaosoma masomo ya sayansi na hasa wanawake kwa mfano Udaktari wapate mikopo asilimia 100 lakini kuna wasichana wengi wanarudishwa hawajaweza kupata mikopo na hawana uwezo wa kulipa ada, tunatengeneza uchumi wa aina gani? Unapozungumzia kukua kwa uchumi wa mwananchi mmoja mmoja ni pamoja na kujali na kuwa na dialogue na hao watu kuweza kujiendeleza ni jinsi gani tunaweza kupeleka Taifa mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vitambulisho vya Taifa vilizungumziwa wapi, sisi kama Wabunge haikuletwa humu Bungeni, ni uchumi gani ambao mnauzungumzia? Bado tunahitaji Watanzania waweze kuendelea kiuchumi. Baada ya miaka minne ndiyo mnakumbuka kukaa na wafanyabiashara na hii ni kwa sababu hampendi kusikiliza mawazo mbadala mngechukua hatua mapema haya matatizo yasingetukuta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Deni la Taifa. Mwaka jana nilichangia hapa nikasema Deni la Taifa limekuwa ni tatizo, naogopa kusema kansa nitaambiwa nifute, limekuwa ni tatizo. Leo hii limefikia shilingi trilioni 51 kutoka shilingi trilioni 49, hii ni hatari. Kibaya zaidi katika kulipa deni hili bado tunaweza kushindwa kulilipa kwa wakati na mwisho wa siku watoto wetu watapata shida sana kulipa haya madeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitoa wazo kuhusiana na Deni la Taifa kabla Serikali haijakopa ilete humu ndani sisi kama Wabunge tuone umuhimu wa hilo deni kama linatakiwa kukopwa tupitishe kwa pamoja maana sisi ni wawakilishi wa wananchi. Nadhani ni vyema tukaliangalia hili deni la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakuja kwenye taulo za kike, wewe na mimi kama mama tunaowatetea wasichana na wanawake, leo hii unasema kwamba tumerudisha kodi kwa sababu wafanyabiashara walishindwa, mimi sioni kama Serikali imesimama katika nafasi yake maana ni Serikali ilitakiwa kuwasimamia hawa watu kusambaza au kushusha bei. Leo hii mazao ya Coca-Cola, Pepsi yanauzwa bei moja kwa sababu kuna bei elekezi, Serikali ilishindwa nini kuweka bei elekezi kwenye taulo hizi za kike? Mwisho wa siku kwenda hedhi ni suala la kibaiolojia na mimi sikupanga kwenda hedhi, ni kitu nimezaliwa nimekikuta, kwa hiyo, tusiwahukumu wanawake na mabinti zetu kwa sababu ya hali yao ambayo Mungu amewapa. Naomba Serikali itakaporudi ijaribu kufikiria hili suala na waweze kulibadilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado nina…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono bajeti yetu ya Kambi Rasmi ya Upinzani, ahsante. (Makofi)