Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Awali ya yote naomba nitoe salamu za pongezi sana kwa Serikali sikivu ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri sana ambayo anaifanya kwa ajili ya kukuza uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili ya salamu za shukrani zimfikie Mheshimiwa Luhaga Mpina, Mbunge, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, pamoja na timu yake yote Wizarani. Salamu hizi zinatoka kwa wananchi wa Hanga Ngadinda katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba. Wananchi hawa kwa muda mrefu wamehangaika sana kupata eneo la kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hekima kubwa na kwa uzalendo Mheshimiwa Waziri amekubali kuwapa hekta 1,800 ili kutatua tatizo la wananchi hawa. Tunamshukuru sana, sana, sana. Mheshimiwa Luhaga Mpina amekuwa mmoja katika Mawaziri ambao wapo tayari kuchukua maamuzi magumu yanayotatua matatizo ya wananchi. Tunaomba Serikali pia itambue mchango mkubwa wa Waziri huyu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, naomba nijielekeze kwenye kuishauri Serikali katika mambo muhimu yanayohusu kukuza uchumi, hatutapata Tanzania ya viwanda kama hakuna uratibu wa pamoja wa sekta na Wizara zinazotegemeana. Hizi Wizara zinazotegemeana tunaziita Line Ministry. Ili upate Tanzania ya viwanda unahitaji uratibu wa pamoja wa Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Viwanda na Biashara pia kwa karibu sana na Wizara ya Ardhi.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, malighafi asilimia 65 inayohitajika viwandani au niseme viwanda kwa asilimia 65 vinategemea malighafi kutoka katika sekta hizi nilizozitaja ambazo ni sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi, madini lakini ardhi ndiyo Mama katika haya yote ambayo nimeyataja. Kama hakuna uratibu wa pamoja wa hizi Wizara hatutaipata Tanzania ya viwanda.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na eneo la kilimo. Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwenye hotuba yake ameondoa vikwazo vingi sana vya biashara, tunamshukuru na tunampongeza sana, hatua aliyoichukua itatatua tatizo la kufanya biashara nchini na ufanyaji biashara utakuwa rahisi zaidi, lakini Mheshimiwa Waziri wa Fedha amesahau sekta Mama ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania, sekta ya kilimo. Kwenye mchango wangu wakati nachangia Wizara ya Kilimo nilisema, hatutaweza kupata mapinduzi ya kilimo kama hatutawekeza kwenye usambazaji wa pembejeo na usambazaji wa pembejeo vijijini unakwazwa na gharama kubwa za kufungua maduka ya pembejeo na gharama hizo zinachangiwa na TFRA, TPRI, TOSC na TFDA.

Mheshimiwa Naibu Spika, tozo hizi Mheshimiwa Wazri Mkuu alizijibia humu ndani. Mheshimiwa Waziri wa Fedha naomba urejee kwenye majibu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu hizi tozo zinazokwaza uendelezaji wa sekta ya kilimo. Huwezi kupata mapinduzi ya kilimo kama hautaki kuwekeza kwenye usambazaji wa pembejeo. Sasa mtu wa kijijini anayetaka kufungua duka la kusambaza pembejeo na ninaposema pembejeo maana yake mbegu bora, mbolea na viuatilifu, kama hivyo havipo huwezi kupata mapunduzi ya kilimo. Kwa hiyo Mhehsimiwa Waziri wa Fedha naomba rejea kwenye majibu ya Waziri Mkuu kaondoe hizi tozo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Fedha ondoa tozo kwenye TFRA shilingi 100,000, ondoa tozo kwenye TPRI shilingi 320,000, ondoa tozo kwenye TOSC na TFDA ili mjasiriamali wa kijijini aweze kufikisha pembejeo kwa wakulima wadogo bila hivyo huwezi kupata mapinduzi ya kilimo na usipopata mapinduzi ya kilimo hakutakuwa na Tanzania ya viwanda. Hili ni muhimu sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na kama kutakuwa na fursa ya kushika shilingi Mheshimiwa Waziri wa Fedha, wote tunaoamini kwamba wakulima ndiyo mtaji mkubwa wa Watanzania na mtaji mkubwa wa CCM tutasimama na tutashika shilingi yako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema sekta hizi Mama zisipofanyakazi pamoja hatutapata mapinduzi ya viwanda. Ninaomba pia Waziri wa Fedha akubali kuziratibu hizi Wizara zote nilizozitaja. Ukisoma kwenye hotuba ya Waziri wa Kilimo ana vipaumbele vya mazao, atakuambia katika msimu huu kipaumbele changu ni mazao moja, mbili, tatu, nne huyo ni Waziri wa kilimo. Ukienda kwa Waziri wa Viwanda na Biashara ukisoma kwenye hotuba yake Waheshimiwa Wabunge mkasome mtaona baadhi ya mazao ambayo yamepewa kipaumbele na Wizara ya Viwanda na Biashara hayapo kwenye vipaumbele vya Wizara ya Kilimo sasa huyu anayeenda kuzalisha viwanda malighafi anazitoa wapi? Kwa hiyo, uone kwamba hapa ni kama hakuna coordination. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili upate mapinduzi ya viwanda unahitaji coordination. Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Nishati na Madini, Viwanda na Biashara na Wizara ya Ardhi mkubali sasa kukaa pamoja, kutengeneza mpango kazi wa pamoja, utaratibu wa joint planning, mfanye joint evaluation na monitoring ili tuweze kuipata Tanzania tunayoitaka.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maslahi ya muda, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)