Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii na mimi nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa mtoa hoja, Mheshimiwa Waziri wa Fedha ndugu yangu Dkt. Mpango kwa kutuletea bajeti hii ambayo kwa kiasi kikubwa sana inaakisi matarajio na matazamio ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda wa takribani miezi minne, tupo hapa Dodoma tukianzia kwenye Kamati kuangalia ni namna gani tunaweza tukaishauri Serikali katika kuhakikisha kwamba tunaboresha bajeti mbalimbali za Wizara. Lakini kumekuwa na maneno kwamba wengi hapa muda mwingi sana tunautumia masuala ya matumizi; maji, umeme, barabara, hospitali, shule na vitu kama hivyo na muda mchache/mfupi sana tunautumia katika namna ya kuishauri Serikali itakavyoweza kuongeza wigo na uwezo wa kupata mapato zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi mchango wangu utajikita zaidi namna gani ya kuishauri Serikali itakavyoweza kuongeza mapato ili sasa yale matumizi yaweze kwenda sambamba na mapato yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninakushukuru sana Mheshimiwa Mpango, nimesoma kitabu chako cha hotuba hususan katika eneo la mifugo na uvuvi, tozo na ada nyingi sana zimefutwa, tunaishukuru Serikali.Lakini tozo na ada nyingi zilizofutwa ni zile tozo zinazohusu masuala ya mifugo zaidi kuliko masuala ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningependa kuishauri Serikali tuangalie sasa namna gani tunaweza tukaenda tukapitia zile tozo na ada mbalimbali zinazohusiana na masuala ya uvuvi. Mvuvi bado ana mzigo mkubwa na mrundikano mkubwa sana wa ada na tozo mbalimbali. Kuna leseni kwanza ya chombo, leseni ya mvuvi mwenyewe, usajili wa chombo, ada/leseni ya kuvua kwa sisi tunaotoka Pwani kule kuvua pweza, samaki, kamba na vitu kama hivyo, kuna utitiri mwingi sana wa ada na tozo kule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunaomba sana Mheshimiwa Mpango utakapokuja basi utuangalie na sisi katika eneo la uvuvi. Hivi ninavyozungumza, pale mpakani Tunduma kuna mizigo na tani kadhaa za dagaa wanaotoka hususan kule Mafia wapo pale wamezuiwa kutokana na ile ada ya dola 1.5, hii imekuwa ni mwiba mkubwa sana kwa wavuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na hawa wafanyabiashara wanaouza dagaa wengi wanatokea maeneo ya Congo, wanakuja kule kwa mfano kule ninapotokea mimi Mafia wanakuja kununua dagaa, lakini wanakutana na tozo na ada nyingi sana. Mimi nilikuwa naomba sana Mheshimiwa Mpango, tunashukuru kwa upande wa mifugo kule mambo yamekwenda vizuri na sisi wavuvi tunaomba pia mtukumbuke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwenye eneo hilo hilo la uvuvi lakini sasa katika eneo la uvuvi wa bahari kuu. Tulizungumza hapa na mimi nimeshachangia mara nyingi sana kwamba namna gani Taifa hili linaweza likanufaika kutokana na uvuvi na mapato yanayotokana na uvuvi wa bahari kuu. Mimi nashukuru sana Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, juhudi tunaziona; kwanza juhudi zile za kufufua lile Shirika letu la Uvuvi la TAFICO, ni juhudi za kupongezwa na kuungwa mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia juhudi tumeona kwamba kwenye bajeti imetengwa fedha kwa ajili ya kununua meli, lakini mimi bado ninaamini zile meli ambazo tutazinunua, uwezo wake hautokuwa mkubwa sana kulinganisha na meli zile ambazo za kigeni zinazovua katika ule ukanda wa kiuchumi wa bahari wa EEZ ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, kwa sasa mimi ningeomba sana na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi simuoni hapa lakini nadhani Naibu atakuwepo. Tatizo lililokuwepo ambalo naomba sana tulianyie kazi, ni ilea da ya dola 0.4 ambayo inatozwa kwa kila kilo moja ya samaki aina ya jodari au maarufu tuna anayevuliwa katika EEZ yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya sana, wale wenye meli kubwa ada hii hawajakubaliana nayo na toka imewekwa wamesusa, hawaji. Sasa bahati mbaya tuliyokuwa nayo, ile mamlaka yetu ya uvuvi wa bahari kuu DSFA, ile inategemea mapato yake yote kutokana na leseni zitakazokatwa na wale wenye meli kubwa wanaokuja kuvua katika EEZ yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa kuwa kutokana na hii ada ya dola 0.4 wameona kwao ni mzigo mkubwa, wamehama wanakwenda katika nchi jirani wanakata leseni, nini hasara yake? Hasara yake samaki siyo kama madini labda ya dhahabu ukasema yapo pale Buzwagi au Bulyanhulu, hayatoki mwaka wowote tunaweza tukachimba, samaki wanatembea…

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. MBARAKA K. DAU: ...samaki, Mheshimiwa…

MHE. MATTAR ALI SALUM: Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dau kuna taarifa. Mheshimiwa Mattar.

T A A R I F A

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nimpe taarifa kaka yangu kwamba hii dola 0.4 ikiondoshwa leo, wapo wawekezaji wenye meli zaidi ya 50 wapo tayari kuja kuvua kwenye nchi yetu. Kwa hiyo, hii dola 0.4 ni tatizo kubwa katika nchi yetu katika uwekezaji wa bahari kuu, asante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbaraka Dau unaipokea taarifa hiyo?

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, siyo tu kwamba naipokea taarifa hiyo pia naomba iwe sehemu ya mchango wangu kwenye Hansard. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kusema samaki hususan, maana yake samaki wanaozungumzwa hapa ni jodari tu (tuna) wale, wale wenye meli kubwa wakija kuvua wao habari ya samaki wengine wanaitwa by catch wale wanaovuliwa kwa bahati mbaya wale hawawahitaji, wao wanahitaji tuna tu. Sasa hawa samaki tuna ni samaki wa makundi, wanatembea, leo wapo katika pwani ya Tanzania, kesho wapo katika pwani ya Somalia na baadaye wapo kwenye pwani nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wewe unapozuia kwa maana ya kuweka masharti magumu kama hii royalty ya 0.4 hawa samaki haina maana kwamba watabaki hapa hapa Tanzania tu, samaki hawa wanahama na wanahama kutokana na texture ile ya bahari inapobadilika kwa sababu kuna hizi pepo za kaskazi, pepo za kusi, kuna nyakati bahari inakuwa na motomoto na kuna wakati bahari inakuwa baridi, kwa hiyo hawa samaki wanahama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tusipotoa ruhusa hii na mimi sisemi ifutwe kabisa, hata kama tukianza na labda 0.1 ili kwanza tuwavute hawa watu na ile Mamlaka yetu DSFA basi ianze kufufuka, tuweze kwenda vizuri na faida zinazotokana na uvuvi wa bahari kuu ni pamoja na vijana wetu kupata ajira kwenye zile meli kwa sababu kwa mujibu wa kanuni za DSFA ni kwamba meli zinapokuja kuvua, watanzania wanapata fursa ya kuwa mabaharia ndani ya zile meli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini faida nyingine, kanuni zinasema na Mheshimiwa Ulega utakuwa unazifahamu, kanuni zinasema wale samaki (by catch) ambao siyo walengwa labda umevua papa, nguru, changu na samaki wa aina hiyo, hawa inabidi uje uwalete katika Bandari aidha ya Zanzibar au Bandari ya Dar es Salaam na inakuwa ni mali ya United Republic of Tanzania.Kwa hiyo, hizi faida zote sisi tunazikosa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningeomba sana, najua kuna mchakato wa kisheria katika kupunguza, kufuta au kufanya hivi, basi tuuanzishe huu mchakato ili tuhakikishe kwamba tunanufaika na uvuvi wa bahari kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuna kitu kinaitwa uendelezaji wa utalii katika kanda ya kusini (southern circuit). Unapoizungumzia southern circuit, mimi nasikitika sana na nimemuona ndugu yangu Mheshimiwa Kanyasu hapa. huu utalii wa kanda ya kusini mbona utalii wa fukwe haupo? Sisi tunaotoka Mafia, Mafia na yenyewe ni sehemu ya kanda ya kusini; sasa hatuoni mikakati yoyote ya kuendeleza utalii katika fukwe ambapo Mafia ni sehemu kubwa sana ambayo watalii wanatakiwa waje pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna faida nyingi sana za kukifungua Kisiwa cha Mafia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)