Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Hamadi Salim Maalim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kojani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uzima wa kuweza kusimama hapa katika Bunge hili na kupata nafasi ya kuchangia katika bajeti hii ya Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze mchango wangu kwa kunukuu maelezo yangu niliyoyatoa katika bajeti ya mwaka jana nilipoichambua bajeti na kusema kwamba bajeti iliyoletwa ni hewa. Bado narudia maelezo yangu yale yale kwamba na bajeti mara hii pia ni bajeti hewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya mwaka jana mpaka kufikia mwezi Aprili, 2019 imechangia shilingi trilioni 21.22 ukiachia miezi mwili iliyobakia kuna shilingi trilioni 11.24 ili ikamilishe bajeti yote. Siamini kwamba miezi miwili tunaweza tukakusanya shilingi trilioni 11 tukaweza kukidhi bajeti nzima ya Serikali. Bajeti ya mara hii imeongezwa kutoka shilingi trilioni 32.48 kufikia shilingi trilioni 33 kwahivyo bado naendelea kusema maelezo yangu kwamba bajeti iliyoletwa ni hesa na haitekelezeki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanini nakasema ni hewa? Bajeti hii imepanga kutumia shilingi trilioni 9.721 kwa Mfuko Mkuu wa Serikali ambapo ukizigawa hizi kwa miezi 12 tunalazimikiwa ni kila mwezi kupata shilingi bilioni 810.08; mishahara imapangwa kutumia shilingi trilioni 7.558 ambapo kwa kila mwezi tunatakiwa tutumie shilingi bilioni 629.83; OC ni shilingi trilioni 3.576 ambapo kwa kila mwezi tunatakiwa tutumie shilingi bilioni 298.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye fedha za maendeleo, ukitoa fedha za nje, tuchukue yale makusanyo ya ndani tu tumepanga kutumia shilingi trilioni 9.737 ambapo kwa kila mwezi ni shilingi bilioni 811.416. Jumla ya makusanyo yote haya na matumizi yaliyopangwa ni shilingi trilioni 2.548 kwa kila mwezi. Hivi kweli tuna uwezo wa kukusanya shilingi trilioni 2.5?

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi siamini kwamba Serikali yetu ina uwezo wa kukusanya shilingi trilioni 2.5 labda iwe ni mara mbili zaidi tuichukue kama tutumie miaka miwili ndiyo tutaweza kukusanya hiyo, lakini kwa mwaka mmoja hatuna uwezo wa kukusanya shilingi trilioni 2.5 ukichukua uzoefu wa miaka yote mmine tuliyoingia katika Bunge hili na makusanyo yaliyokuja na bajeti ilivyotekelezwa inaonesha kwamba bado bajeti hii ni hewa na itapelekea ugumu sana kutekelezwa katika Wizara mbalimbali za Serikali. Hapo nimetoa malipo ya wafadhili yaani wahisani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukichukua na wahisani ina maana tunatakiwa tupate shilingi trilioni 2.757 kila mwezi ili tuweze kutekeleza bajeti yetu na iweze kwenda sawa, lakini kwa maana hiyo nasema kwamba bado bajeti ni hewa na italeta ugumu katika utekelezaji wake. Kambi Rasmi ya Upinzani ilipowasilisha mawazo yao ilijaroibu kuivuta bajeti kutoka shilingi trilioni 33 mpaka kufika shilingi trilioni 29 angalau na Serikali ingeona mapendekezo kama hayo kidogo tukawa na lile gap ambalo halitekelezeki likawa ni dogo, lakini leo tunafikia gap ambalo halitekelezeki karibu shilingi trilioni tisa/ trilioni nane. Bajeti ambayo haitekelezeki kwa kiasi chote hicho jamani? Hebu Waziri wa Fedha akija hapa atueleze kwanini wanatuletea bajeti ambayo inakuwa na gap kubwa sana ambalo halitekelezeki kiasi kwamba tunashindwa hata kutekeleza miradi ya maendeleo, kulipa madeni ambayo Taifa linadaiwa na nchi za nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kifungu hicho naomba sasa niende kwenye kifungu cha pili ambacho ni Zanzibar ndani ya Muungano. Mheshimiwa mwenzagu aliyetangulia hapa Mheshimiwa Ally Saleh alijaribu kuelezea mapato ya Muungano, mimi nitakwenda upande mwingine. Katika kitabu hiki cha bajeti ambacho Mheshimiwa Waziri aliwasilisha hapa ndani ya kitabu hiki ukianza ukurasa wa mwanzo mpaka mwisho, Zanzibar imetajwa mahali pawili tu alipotajwa Rais, Dkt. Salmin na pale ambapo Zanzibar iliondolewa VAT kwenye suala la umeme. Hivi Zanzibar haipo kwenye Muungano hata iguswe katika maeneo hayo tu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiachia mbali kitabu hiki cha bajeti, kitabu cha miradi ya maendeleo Zanzibar haikuguswa hata sehemu moja. Miradi yote ya maendeleo iliyoelezwa mle ipo Tanzania Bara tu, hivi kweli Zanzibar mnaitendea haki gani jamani kiasi kwamba nimenukuu humu kwamba ndani ya kitabu kile cha miradi ya maendeleo kuna Wizara ya Elimu ya Juu inatekeleza miradi chungu nzima kwenye vyuo vikuu, mbona Zanzibar hawakupewa kwenye Chuo Kikuu cha SUZA angalau japo kile kimoja? Kuna shule zenye form five na form six angalau wangetengenezewa maabara japo moja tukajua kwamba na Zanzibar ipo kwenye sehemu ya Muungano, lakini kwa kweli mnachofanya katika suala zima la bajeti hii Zanzibar hamkuifanyia fair na wala hamko sahihi kuitenga Zanzibar wakati Zanzibar ni sehemu ya Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilijaribu kuangalia kitabu hiki ukurasa wa 16 mpaka ukurasa wa 25; yameleezewa mafanikio ya Awamu ya Tano ya Serikali ya CCM. Kuanzia ukurasa huo mpaka hapo niliposema wa 16 mpaka 25 hivi Serikali ya CCM iko Tanzania Bara tu? Maana ikiwa Zanzibar hakuna Serikali ya CCM, mafanikio haya yaliyoelezwa humu kwa upande wa Tanzania Bara tu Zanzibar hakuna miaka yote hiyo jamani? Sijui kama Zanzibar mnaitendea haki kwa kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba jamani, tunaomba kama Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano itendewe haki. Kuna miradi ambayo ipo kwenye kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kwa mfano; kuna Bandari ya Wete, Bandari ya Mkoani, Bandari ya Mpigaduru, Uwanja wa Ndege wa Zanzibar, uwanja wa Ndege wa Pemba basi hata mmoja angalau mkasema kwamba tunaondoa mdudu mchuzini tunawapa angalau hii Bandari ya Mpigaduru angalau japo moja jamani, hivi kweli mnayotundea ni haki jamani? (Makofi)

MBUNGE FULANI: Sio haki.

MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kwenye kifungu cha madeni ya Taifa; kwenye madeni ya Taifa mwaka jana hapa tuliambiwa mpaka Aprili, 2018 deni la Taifa lilikuwa shilingi trilioni 49 na katika bajeti ile ya mwaka jana ikapangiwa kwamba deni la Taifa litalipwa kwa shilingi trilioni 10 na juzi wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya Wizara ya Fedha hapa Waziri alipoulizwa suala la madeni ya Serikali akasema kwamba tumeanza kulipa ila tumeanza kulipa ya miaka ya 1980, hivi hiyo miaka ya 1980 haipo kwenye ile jumla ya deni lililowasilishwa mwaka jana? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana ikiwa haimo mtuambie kwamba deni lile la trilioni 49 ni la mwaka jana tu 2018 na hivyo katika mwaka jana 2018 halikutekelezwa kwa sababu inaonyesha kwamba mara hii deni lile limeongezeka kufikia shilingi trilioni 51, zile shilingi trilioni 10 zilizotengwa mwaka jana kwa ajili ya kulipa deni zilipelekwa wapi hebu tuambieni mlizipeleka wapi shilingi trilioni 10 za mwaka jana? Waziri wa Fedha ukija hapa utueleze shilingi trilioni 10 zilizotengwa mwaka jana kwa kulipa madeni ya Taifa zilipelekwa wapi mpaka deni lile la shilingi trilioni 49 la mwaka jana likaja tena mwaka 2019 vilevile kama lilivyo likiongezwa tena linafikia shilingi trilioni 51. Itabidi ukija hapa mtupe maelezo kwa nini halikulipwa shilingi trilioni 10 za madeni ya nje zilizopangwa kulipwa zilipelekwa wapi mtuambie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo naomba niende kwenye kifungu cha tozo; nina imani kwamba ukienda dukani kununua vitu ukinunua kidogo bei itakuwa ni kubwa, lakini ukinunua vingi kwa vyovyote vile muuza duka atakupunguzia. Hali kadhalika ukienda kwenye kiwanda ni hivyo hivyo nashangaa kuona kwamba madereva wamepigwa changa la macho kwenye leseni, madereva walivyokuwa wanalipwa miaka mitatu leseni ilikuwa shilingi 40,000, juzi Mheshimiwa Waziri katika kuwasilisha bajeti yake akasema sasa tunahamisha kutoka miaka mitatu hadi miaka mitano kutoka shilingi 40,000 mpaka shilingi 70, 000 hivi jamani hamuoni kwamba mnawapiga changa la macho madereva?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukinunua khanga pair tatu dukani utauzia kila khanga pair shilingi 7000 lakini ukinunua pair tano utauziwa bei ya jumla hivi miaka mitatu na miaka mitano mingi ni ipi tuambieni mimi nashangaa kuona kwamba Mheshimiwa Waziri wa Fedha anatupandishia bei kwenye miaka mingi, lakini miaka midogo bei inakuwa ni ndogo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)