Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE.BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya mimi kuchangia katika bajeti hii. Kwanza niishukuru Wizara na Waziri wa Fedha, amefanya na Idara yake yote, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara ya Fedha, wamefanya kazi nzuri sana, tumeona bajeti hii katika maeneo mengi sana wamepunguza vitu vingi sana na kwa maana hiyo bajeti yenyewe imekwenda katika kukidhi mahitaji ya watu kwenye maeneo mbalimba na makundi mbalimbali, mimi kwa maoni yangu naona wamefanya vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuzungumza miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Mara. Nilikuwa naomba sasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, katika bajeti tuliyokuwa nayo, katika ile miradi ya kimaendeleo katika majimbo yetu, katika miradi ambayo imekuwepo kwa muda mrefu, mradi wa hospitali ya Kongwa ya mkoa wa Mara, mradi wa barabara ya kutoka Makutano kwenda Sanzate; Sanzate - Nata - Mugumu; mradi wa barabara ya kutoka Nyamswa - Bunda - Buramba, mradi wa bandari ya Musoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba katika bajeti hii ambayo mmeiweka basi hiyo miradi iweze kutimilizika na kwa wakati muafaka, ni vizuri sana tunapoweka bajeti tuwe tunaweka vitu ambavyo vinakuwa halisia. Tusiwe na bajeti ambayo inakera wananchi na miradi ambayo nakera wananchi. Tumekuwa na miradi ya muda mrefu kwa Mkoa wa Mara ambayo haiishi. Pamoja na kwamba tunafanya jitihada sana ya kushukuru Serikali kwa kutupa miradi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze zao la pamba, sasa sijui kama kuna Waziri yuko hapa Waziri wa Kilimo ananisikiliza vizuri. Zao la pamba kwa sasa hivi kwa maeneo yote yanayolima pamba sasa imekuwa kama sumu, kwanza bei yake sasa haijulikani ni shilingi 2,000 na shilingi 1,200, lakini ukienda vituoni kuna watu wananunua pamba shilingi 850, lakini pia haina uhakika kwamba mtu akipeleka pamba apate fedha yake kwenye kituo cha kununulia pamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia mwaka jana, unakumbuka kwenye bajeti hapa alikuja Waziri wa Kilimo enzi hizo Mheshimiwa Tizeba, akasema wakulima watakatwa shilingi 100, hata kama mkulima huyu hakukopa pembejeo, lakini kwa msimu huu 2019/2020 huyo mkulima hatakatwa pembejeo zitakuwa bure, lakini mpaka tunapozungumza hapa pembejeo zinakatwa! Watu wanajiuliza, mimi nilikatwa fedha yangu bila kukopa, lakini bado leo nakatwa pembejeo tena ya shughuli gani na Bunge hili liliridhia kukata shilingi moja ya wakulima wa pamba, kwa hiyo, tukafikiri kwamba ni jambo la msingi kuwa katika hali hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, yamezungumzwa mengi, nilikuwa nazungumza, mtu anazungumza mambo ya magazeti, mambo ya nini, jamani magazeti ni uhuru wa kila mtu anavyoona. Magazeti yako wazi na ndiyo maana huwa nawauliza waandishi wa habari, wakati fulani waandishi wa habari ukienda, ukiwanyima taarifa, wanasema wanakushitaki, ukiwapa taarifa, wanakwambia nipe vizuri. Kwa hiyo, nafikiri kwamba magazeti ni uhuru wa kila mtu kufanya anavyotaka. Sasa kusema kwamba gazeti fulani ni la wahuni au la nini, mimi sielewi!

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi hapa wakati wa bajeti Waziri anahitimisha hapa, tumeona hapa tunataja viongozi wa kitaifa wa nchi hii. Wamemtaja Mheshimiwa Pinda, wenzetu wa upande huu hata makofi hawapigi, wakitajwa wazungu wanapiga makofi, kwa hiyo, kuna watu wameshakuwa colonized kwenye mambo kama hayo wanaweza kuwa…(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wahuni ni wapi! Wanaoshangilia watu wa nchi yao au wahuni wanaoshangilia watu wa nje. Kwa hiyo, nafikiri kwamba kuna vitu vingine humu ndani tuviangalie vizuri watu wanapokuwa wanafanya kazi hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nazungumza hoja watumishi, kuna sheria za kimataifa za International Labor Organization ( ILO) ambazo zinamruhusu mtumishi wa Serikali kukopa moja ya tatu ya mshahara wake, lakini tunavyoenda mabenki kwa kushirikiana na watumishi mbalimbali, wamevunja, hiyo sheria wanaivinja. Sasa hivi mshahara wa mtumishi unaweza kukuta shilingi milioni moja, anapata shilingi 100,000; shilingi 400,000 anapata shilingi 50,000; watumishi wengine wanapata sifuri.

Sasa nimeona hapo tunazungumza habari ya kubana matumizi na kupitia sheria mbalimbali ili zilete nafuu.Tutazame hali ya watumishi wanavyokopa katika mabenki, hii sheria ya mataifa ambayo tumeridhia sisi tuitazame tuone watumishi wanapata kwa kiasi gani zile fedha ambazo..., imekwenda. Sheria inasema, kama utamkopesha mtumishi zaidi ya hapo, maana yake unamuua huyo mtumishi, sasa watumishi wamekopa zaidi na kama atakopa zaidi aoneshe vyanzo vya mapato ambavyo wanaweza kukopea, lakini watumishi wengi, hata leo tungeongeza mshahara milioni moja, bado wanapata sifuri. Kwa hiyo, naomba tuliangalie hiyo sheria ambayo inaweza kuwaruhusu watumishi wakaishi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ...

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwita Getere kuna taarifa, Mheshimiwa Keissy.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nipe taarifa mzungumzaji kwamba siyo watumishi tu, hata Wabunge wamefanya hivyo hivyo, sasa nashangaa anawapigia jembe watumishi, wakati Wabunge wamekopa zaidi ya asilimia 80 ya mshahara wao! (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Getere unaipokea taarifa hiyo?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea taarifa yake lakini namkumbusha tu Wabunge nao ni watumishi sawa na watumishi wengine tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nazungumza habari ya vitambulisho, sijui katika suala hili kwanini watu wameling’ng’ania sana. Vitambulisho ilikuwa kumuokoa machinga aliyekuwa anafukuzwa kila mahali anapoenda anafukuzwa, tukaweka vitambulisho kumuokoa kwenye mazingira mabovu. Sasa leo kama kuna watu wanatenda vibaya huko, sasa inakujaje kwa Rais, kuna watu wanatenda vibaya huko, inakujaje? Ni wajibu wa Mbunge kwenye Halmashauri yake kumwambia Mkuu wa Wilaya, kumwambia Mkurugenzi, kuwaambia wale waliopewa kazi kwamba Rais hakuagiza kufanya hivyo. Hakuna haja ya kuja kupiga kelele humu ndani, Rais alitoa vitambulisho, anauza, anafanyaje, vitambulisho vilijulikana toka mwanzo, kwamba vitambulisho ni shilingi 20,000.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwita Getere kuna taarifa, Mheshimiwa Cecil Mwambe.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa ndugu yangu anayeongea kwamba labda hasomi na kufuatilia. Karibuni ilikuja taarifa kwamba TAMISEMI wamekaa na kupitia upya list ya watu wanaostahili kupata vitambulisho. Kwa mfano, Mkoa wa Lindi, Mtwara na kwingine kwenye bahari, wakiwemo pamoja na wapaa samaki, akina mama wanaouza matembele barabarani na wengine. Sasa nataka tu nimpe taarifa, kama watu hawa hawako jimboni kwake na kwamba atoe sasa ufafanuzi vizuri na aichukue hiyo taarifa aseme exactly huko kwenye jimbo lake waotozwa ni nani?

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge,...

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, unajua kuna watu wanakariri siasa, ndiyo hawa hawa!

NAIBU SPIKA:Mheshimiwa Mwita Getere tafadhali.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa sikubaliani nayo kwa sababu huyu amekariri siasa.

NAIBU SPIKA: Subiri kwanza Mheshimiwa Mwita Getere.

Waheshimiwa Wabunge, tukumbushane tena, uvyotoa taarifa huulizi maswali, kwa sababu siyo kazi yake Mbunge kukujibu wewe, ndiyo maana kanuni zetu zinasema unampa taarifa halafu anaulizwa kama anaikubali au hapana. Sasa ukimuuliza swali maana yake unataka akujibu wewe, kwa hiyo, tukumbushane tu hilo. Mheshimiwa Mwita Getere unaipokea taarifa hiyo?

MHE.BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei kwa sababu huyu naye anakariri tu mambo ambayo hayapo. Tumesema makundi mbalimbali yameainishwa, yanaweza kuchukua vitambulisho vya taifa, kadri wanavyoviona vinawafaa, sasa mambo mengi yakitekelezwa vibaya, hayo ni jambo lingine tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuona mwanamke, unaweza sisi kwa kabila letu wa huko tunaozwa na baba, lakini suala la ku-deal ndani huko kama mna matatizo ni ninyi tu mnaokaa humo ndani, si suala lingine tena baba aje kusema kwamba kulikuwa na nini, angalia sana ndugu yangu mambo mengine unayazungumza uone yanavyokwenda huko kwenye maisha yako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nazungumza, bajeti hii, nimuombe Waziri sasa, tumekuwa tunaweka bajeti kila mara, lakini bajeti yenyewe haiendi vizuri kwenye miradi yetu. Nirudie katika hilo, katika mwaka huu wa bajeti tunaouweka...

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kwa mchangiaji huyu hiyo itakuwa taarifa ya mwisho, Mheshimiwa Ryoba Chacha.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka kumpa mzungumzaji taarifa kwamba, vitambulisho vya shilingi 20,000 vimewasaidia wafanyabishara wadogo sana. Zamani kwenye Halmashauri zetu, kila siku mfanyabiashara anatozwa shilingi 500, ukichukua shilingi 500 mara siku 365 ni shilingi 182,000. Leo anaoa shilingi 20,000. Kwa hiyo, ni faida, anayepinga huyo hajitambui, hajui hesabu. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwita Getere unapokea taarifa hiyo?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea taarifa yake.

Mimi narudia tu kusema kwamba bajeti ya mwaka 2019/2020 izingatie miradi muhimu ambayo tumeiweka, itenge kama kuna mradi wa stiegler’s gauge, kuna mradi wa reli, kuna miradi ya kujenga bandari, kuna miradi mbalimbali ya Kitaifa iweke bajeti yake lakini katika miradi yetu pia ya maendeleo katika majimbo yetu, ile miradi ambayo tunakuwa nayo ya barabara, ya maji, ya kila kitu nayo iwekwe miradi yake. Tuhakikishe kwamba bajeti inayowekwa inakuwa na uwiano na even distribution, isiwe sasa sisi tunakuwa na barabara, tunakuwa na maji, tunakuwa na maendeleo bajeti yetu inakuja kidogo halafu inatuumiza sana kwenye maeneo ya wananchi kwenye maeneo yetu. Kwa hiyo tuweke bajeti ambayo inaweza kuwa sahihi kwneye mambo ya maeneo ya Wabunge, lakini maeneo ya Kitaifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)