Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Risala Said Kabongo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia kuhusiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS). TFS imepewa dhamana ya kusimamia maeneo ya misitu 461 nchini. Maeneo haya yanahifadhiwa kwa malengo makuu matatu:-

(1) Ikolojia; hakuna anayefahamu umuhimu wa maji nchini, kwa binadamu, wanyama na mimea. Mfano, Jiji la Tanga wanategemea maji yake kutoka chanzo cha Msitu wa Amani Nature Reserve, Mkoa wa Kilimanjaro wanategemea maji kutoka chanzo cha Msitu wa Chome na Jiji la Dar es Salaam wanategemea maji kutoka Mto Ruvu – Msitu wa Uluguru ukiwa ndiyo chanzo chake.

(2) Lengo la pili ni kuhifadhi viumbe hai. Misitu hii inahifadhi viumbe adimu duniani. Mfano, vyura wa Kihansi na vinyonga wa pembe tatu.

(3) Lengo lingine ni kwa ajili ya utalii. Mfano Msitu wa Asili wa Amani, Chome, Maporomoko ya Kalambo na Msitu wa Rondo. Kwa siku za karibuni misitu hii imekuwa ikivutia watalii kutoka nchi za Asia kwa ajili ya utalii wa forest bathing kuondoa stress.

Mheshimiwa Naibu Spika, Utalii wa Kupiga Picha. Wasanii wa kizazi kipya wameonekana kuvutiwa sana na misitu yetu na wanakwenda kurekodi filamu katika misitu yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Utalii wa Kuangalia Ndege wa Aina Mbalimbali Katika Msitu wa Rondo mkoani Lindi. Ndege hawa wanatoka mabara mbalimbali ya Ulaya na kuweka makazi yao katika Msitu wa Rondo. Msitu huu unashika nafasi ya 43 duniani kwa kuwa na ndege wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mazuri haya lakini misitu hii imekuwa na changamoto mbalimbali. Changamoto ya miundombinu ya barabara kabla na baada ya mvua. Mfano, Maporomoko ya Kalambo, barabara ya lami Sumbawanga kuelekea Makao Makuu ya Wilaya ya Kalambo kuelekea Bandari ya Kasanga mpaka wa Kongo na Tanzania kipande cha kilometa nane kuingia kwenye Maporomoko ya Kalambo, barabara ni mbaya sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia TARURA kuiangalia barabara hii ili kusaidia watalii wanaotembelea Maporomoko ya Kalambo pamoja na kuvutia wawekezaji wanaowekeza katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze TFS, Kamishna Prof. Silayo kwa kujenga ngazi zenye Urefu wa mita 270 kwa ajili ya kutembea kwenye maporomoko hayo na lengo ni kukamilisha ngazi zenye urefu wa mita 570 kwa mwaka huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati imetembelea Amani N. Reserve – hali ya miundombinu ni mbaya sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu za idadi ya watalii wa misitu 2015/2016 ni 2,200, mwaka 2016/2017 walikuwa 3,000 na mwaka 2017/2018 walikuwa 3,500. Kwa takwimu hizi kama wangewekeza kwenye miundombinu tungepata watalii wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado mapato yanayotokana na misitu ni kidogo sana. Mwa 2015/2016 ni 245,000,000, mwaka 2016/2017 ni 310,000,000 na mwaka 2017/ 2018 ni 370,000,000. Pamoja na idadi kubwa ya maeneo ya misitu 461, ni maeneo 13 tu ndiyo yanayojiendesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Mapato Ghafi kwa Serikali iangaliwe upya ili kusaidia hizi taasisi kujiendesha; asilimia 30 corporate tax, asilimia 18 VAT, asilimia 15 gawio la Serikali na asilimia 3 SDL; jumla ni asilimia 66. Mashirika haya hayawezi kumudu kujiendesha, tuwekeze kwenye miundombinu ili kuongeza wawekezaji na idadi ya watalii na mapato yataongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mchango wangu kwenye Wizara hii nichukue fursa hii kuwapongeza sana Wizara ya Maliasili na taasisi zake zilizochangia gawio kubwa Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto nilizozionesha kwenye mchango wangu Wizara hii imechangia kwa mwaka mmoja in order of priority, Tanzania Telecommunication Regulatory Authority, Tanzania National Park, Ngorongoro Area Conservation Authority, Tanzania Forestry Services. Taasisi tatu kati ya hizi ni Wizara ya Maliasili na Utalii, hii inaonesha umuhimu wa maliasili kwenye uchumi wa nchi, ni lazima tulinde maliasili zetu. Naomba kuwasilisha.