Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na pongezi kwa Mheshimiwa Waziri Dkt. Kigwangala, Naibu Waziri Mheshimiwa Kanyasu, Makatibu Wakuu na viongozi wote wa Wizara kwa kazi nzuri sana wanayoifanya. Naomba mchango wangu ujikite katika mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Regrow; naipongeza Serikali kwa kutoa kipaumbele na kuona umuhimu wa kuendeleza utalii Kanda ya Kusini (Regrow). Mradi huo unalenga kuongeza ubora wa vivutio vya utalii Kusini mwa Tanzania ikiwa ni pamoja na kuimarisha fursa za kiuchumi kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ukiwemo Mkoa wa Iringa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze sana Serikali kwa kuanza kutua ndege kubwa aina ya Bombadier katika Kiwanja cha Ndege cha Iringa. Pamoja na hilo ni vyema sasa Serikali ikaboresha kiwango cha lami barabara inayokwenda katika Mbuga ya Wanyama ya Ruaha, mbuga ya pili kwa ukubwa katika Afrika na ina wanyama wengi. Wizara hii ya Utalii inatoa msukumo gani kwa Wizara ya Ujenzi na kuona hiyo barabara inaharakishwa kujengwa kwa sababu imechukua muda mrefu sana kutangazwa ujenzi, lakini haufanyiki. Naomba kujua ni elimu kiasi gani inatolewa ili kuwaandaa wananchi wanaozunguka Mradi huu wa Regrow wanaandaliwa ili kujiajiri kupitia utalii?

Mheshimiwa Naibu Spika, Ongezeko la Watalii nchini; niipongeze Serikali kwa kufanya jitihada na kusababisha watalii kuongezeka kutoka 1,327,143 mwaka 2017 na kufikia 1,505,702 mwaka 2018 na kuongeza pato la Taifa, lakini ningependa kujua mkakati wa kuhakikisha watalii wengi wanafika katika mikoa yetu ambako kuna vivutio vingi ambavyo bado hatujaona kutembelewa na watalii wa kutosha katika Mkoa wetu wa Iringa. Je, Serikali imejipangaje kuajiri Maafisa Utalii kila Halmashauri, Wilaya na Mikoa kwa sababu, kuna Halmashauri nyingine zina vivutio vingi, lakini hakuna Maafisa Utalii kuna Maafisa Misitu tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.