Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Lucy Fidelis Owenya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi. Nipende kuipongeza Kambi ya Upinzani kwa hotuba yake nzuri pamoja na ile ya Kamati. Nategemea Mheshimiwa Waziri atachukua maoni yale na kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajikita zaidi katika Sekta ya Utalii. Kwenye report nyingi tumeona kwamba, sekta hii ni kati ya sekta inayochangia katika pato la Taifa kwa asilimia 17.5 na asilimia 25 kwa fedha za kigeni, lakini naona Serikali bado haijaichukulia seriously hii sekta ya utalii. Kwa mfano kwenye fedha za maendeleo ziliidhinishwa shilingi bilioni 26.8, lakini zilitoka bilioni 10.5 tu. Sasa kwa mtindo huu na fedha hizi zilizotoka ni kutoka kwa wafadhili, hata Kambi ya Upinzani imeelezea hilo. Sasa ningependa kujua Serikali wamejipangaje ili tuweze kuwa na fedha zetu wenyewe, ili tuweze kuendeleza maeneo ambayo yanahitajika kuendelezwa? Mfano, kama tunataka kuendeleza Katavi, tunataka kuendeleza kule Southern Circuit, lakini kwa mtindo huu sioni kama wafadhili wakijitoa ina maana hatutaendeleza zile parks nyingine zilizokuwa zinatakiwa kuendelezwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii sekta ya utalii ni moja ya sekta ambayo inazalisha ajira nyingi sana. Mfano, Mlima Kilimanjaro kwa mwaka 2017 zilipatikana ajira takriban elfu 20 kwa wapagazi. Hii achilia mbali bado wafanyakazi wa mahotelini, wafanyakazi ambao wanapeleka watu mbugani na kadhalika. Kwa hiyo, ningeiomba Serikali kwa kweli, ihakikishe kwamba, inaichukulia hii sekta very serious.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine cha kusikitisha ni hizi kodi. Tumekuwa tukizungumzia kila siku, unakuta mtu analetewa kodi ya OSHA 1.5 million, kodi ya NEMC 1.5 million, kodi ya COSATA 1.5 million, bado kodi nyingine nyingi tu zaidi ya 36; sasa unajiuliza COSATA wanakuja wanakutoza kwa sababu umeweka television ndani ya hoteli, lakini tukumbuke kwamba, huyu mwenye hoteli bado analipa mfano kwa DStv, Azam Tv na kadhalika. Sasa ningependa kujua OSHA wanakuja wanatoza labda 1.5, wanawasaidiaje hawa wafanyabiashara, hawatoi elimu wanakuja kuangalia kama mmeweka waya vizuri za umeme na kadhalika, lakini return on investment, wanawasaidia nini wale wafanyabiashara ambao wanakuja kuwatoza hizo hela? Hizo hela zinaenda kufanya nini maana hazirudi kwa wale wafanyabiashara kuja kufanya ile biashara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linalofanya destination ya Tanzania inakuwa expensive ni hizi hidden cost. Unakuta mfano, mtalii akitoka let say Amsterdam kwa package ya siku nane, kutokea kule Amsterdam atalipa dola 4,698 kwa mtu, lakini akija Tanzania analipa dola 5,797 kwa mtu. Kwa hiyo, destination ya Tanzania inaonekana ni expensive sana nami naamini kabisa ni kwa sababu ya hizi tozo ambazo tunaziongeza kwa hiyo, mfanyabiashara kazi yake ni kufanya biashara kwa hiyo, kila chochote anachokipata anakiongezea kwa yule mteja kwa hiyo, destination inakuwa ni very expensive.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningetaka Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara ya Fedha labda watusaidie, high season inakuja mwezi wa Sita na bureau de change wamezifunga. Kwa huu muda mchache walivyozifunga zimeleta bughudha kubwa sana, watalii au wageni wanaokuja kwenye hizi sehemu za wageni unakuta benki zinafungwa saa 10.00 hazi-operate kwa 24 Hours na wakati wa holidays pia zinafungwa na Jumapili zinafungwa, sasa hii inakuwa ni bughudha kwa wageni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nagependa kujua, sidhani kama ni bureau de change zote ambazo zilikuwa zina matatizo, pengine zile zilizokuwa hazina matatizo zingefunguliwa. Kama haiwezekani basi ningeomba Serikali labda walete mobile bureau de change, wawashauri benki wawe na yale magari waweze kutoa hii service kwa sababu hoteli nyingi hawawezi kuweka fedha nyingi ndani ya hoteli kwa sababu ya ujambazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tukiendelea kwa mtindo huu ina maana tunarudi kwenye miaka ya 70 ya black market na watalii au wageni wataanza kutuuzia fedha fake na Tanzania tutakuwa kwenye bad records. Kwa hiyo, naomba twende na wakati, tuko kwenye karne ya 21 jamani, tusirudi tena kwenye miaka 30 iliyopita. Wakati ule tulikuwa tunaficha fedha kwenye vitanda na nini, sasa hivi na sisi twende kwa wakati, sijui hao wanaomshauri Mheshimiwa Rais au walioishauri BOT kufunga zile bureau de change walikuwa wana maana, pengine walikuwa na maana nzuri, lakini sidhani kama kila mtu alikuwa na kosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kulizungumzia ni kuhusu utalii wa utamaduni. Nchi zilizoendelea wana-keep historia zao, unatumia majengo kama Ulaya unakuta museam watu wakienda kwenye museam wanalipa fedha, lakini hapa kwetu unakuta kama Dar-es-Salaam tulibomoa majengo yale ya kale na kujenga maghorofa, lakini kuna vivutio vingi sana katika kila wilaya. Mfano mzuri ni kule Moshi Vijijini, Old Moshi, wakati wa Vita ya Kwanza na ya Pili ya Dunia Wajerumani pale Kikarara walijenga mapango kule chini, lakini mapango yale yamekaa tu idle, sasa sijui kama Wizara wanalitambua hili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hawalitambui basi ni vizuri kwenda kufungua yale mapango iwe kama moja ya vivutio vya utalii ili wale Wajerumani wanavyokuja au tunavyoenda kuuza utalii kule Ujerumani na nini iwe ni mojawapo ya kivutio cha utalii. Kwa ushauri tu, pengine Wizara ingeangalia ni jinsi gani inaweza kutembelea katika kila wilaya wa-identify vitu gani ambavyo vinaweza vikawa ni vivutio na kudumisha utamaduni wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ningependa kuzungumzia kuhusu kuutangaza utalii. Utalii tumekuwa kweli tukiutangaza, lakini mara nyingi wafanyabiashara wamekuwa wakitangaza zaidi na inakuwa ni ghali sana kwao. Sasa nimekuwa nikishauri mara nyingi TTB iwezeshwe ili wafanyabiashara sasa waweze kupunguziwa bei waweze kuitangaza Tanzania zaidi; Mheshimiwa Waziri hapa amesema kuna watalii kutoka Israel walikuja 1,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjulishe Mheshimiwa Waziri kwamba, hawa watalii waliokuja mwaka huu 1,000 wamekuwa wakija kila mwaka wakati wa low season. Kwa hiyo, asije aka-add up ufikiri labda ni tangazo limefanywa mwaka jana ndio tukapata watalii 1,000. Hawa watalii kutoka Israel 1,000 they have been coming here all these years for the past five years wamekuwa wakija hapa kwa hiyo, sio watu wageni. Inabidi sasa tuangalie ni jinsi gani tunaenda kwenye new destinations huko nchi za Russia, Zchesklovakia na nini, maana sasa hivi ndio utalii mpya umekuja wawawezeshe TTB waweze kwenda kule twende tukaingie kwenye hizi new market sio tung’ang’anie tu hizi market za Ujerumani sijui, Uingereza na Ulaya, lakini twende kwenye hizi nchi ndogondogo nina hakika kabisa tukienda huko tutapata watalii wengi zaidi na tutaongeza pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, nashukuru sana. (Makofi)