Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuweza kuhitimisha hoja yangu.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kutoa maelezo ya hoja mbalimbali zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge niwatambue Waheshimiwa wote waliochangia kwa maandishi na kwa kuongea. Hoja hii imechangiwa na jumla ya Waheshimiwa Wabunge 89 wakiwemo Waheshimiwa Wabunge 47 waliochangia kwa kuzungumza humu ndani Bungeni na Waheshimiwa Wabunge 42 waliochangia kwa maandishi. Nitambue kipekee mchango uliotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, nawashukuru sana kwa maoni yao mazuri na mapendekezo yote na ushauri ambao wameshautoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwani wametoa hoja nzuri zenye malengo ya kuimarisha utekelezaji wa majukumu katika Wizara yangu na kuharakisha Mapinduzi ya Kilimo chetu hapa nchini. Hii inaonesha umuhimu wa kilimo katika usalama wa chakula, lishe, ukuaji wa uchumi, na kupunguza umaskini.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Omary Tebweta Mgumba (Mb) na Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa (Mb) kwa kuchangia hoja hii na kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizotolewa na Wabunge, nawashukuru pia Katibu Mkuu Mhandisi Methew John Mtigumwe, Naibu Katibu Mkuu Profesa Siza Tumbo, na watendaji wote wa Wizara na Taasisi zake kwa ushirikiano na ushauri wanaoendelea kunipa katika utekelezaji wa majukumu yangu. Michango iliyotolewa ni mingi sana na yote ni muhimu sana. Hata hivyo kutokana na ufinyu wa muda nitafafanua baadhi ya hoja zilizotolewa ambazo ni muhimu Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla wakapata ufafanuzi wa moja kwa moja. Ninawahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba majibu ya hoja zote zilizotolewa yataandaliwa na kukabidhiliwa kwa Waheshimiwa Wabunge kabla ya kumalizika kwa mkutano huu wa Bunge la Bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kujibu hoja ya Waheshimiwa Wabunge kwa kueleza mwelekeo wa Serikali katika kuleta mapinduzi ya kilimo hapa nchini. Sote tunatambua umuhimu wa kilimo katika usalama wa chakula, lishe, ukuaji wa uchumi, malighafi za viwandani na kupunguza umaskini. Sote tuko hapa kwa sababu tumepata chakula tumekula, ama kama hatujala muda huu tutakula jioni au usiku; kwa hiyo sisi wote ni wadau katika suala hili.

Mheshimiwa Spika, vilevile Tanzania kama sehemu ya dunia imesaini makubaliano ya kimataifa kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu, (Sustainable Development Goals – SDG). Chini ya makubaliano hayo ya kimataifa lengo namba moja linahusu kutokemeza umaskini na lengo namba mbili ni kukomesha njaa ifikapo mwaka 2030. Malengo hayo yanamaana kubwa kwenye kilimo kwani kama tunataka kutokomeza umaskini na kukomesha njaa ni lazima tuwekeze kwenye kilimo kwa kufanya mapinduzi yenye kuongeza tija na uzalishaji, kuwa na uhakika wa kuzalisha mazao bora kwa ajili ya malighafi za viwandani na masoko ya ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa Mapinduzi ya Kilimo na kama nilivyowasilisha kupitia hotuba yangu Serikali inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya pili ASDP II. Programu hii inalenga kuleta mageuzi makubwa ya sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo. Sisi sote ni mashahidi tunaona tija ilivyo ndogo sana katika maeneo mengi kwenye kilimo chetu. Tunakusudia kufanya kilimo kiwe cha kibiashara zaidi na kuongeza Pato la Taifa kwa wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha yao. Pia tunahitaji kuwa na uhakika na usalama wa chakula na lishe na kuchangia katika Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, historia inatuonesha kuwa nchi nyingi duniani zimepiga hatua kubwa kwa maendeleo kutokana na mchango wa sekta ya kilimo. Nchi kama Uingereza, China, Malaysia, Canada, Korea, Indonesia na nchi nyingine nyingi zimeendelea kwa sababu ya mchango mkubwa wa kilimo katika uchumi wao. Nchi nyingine hizo uchumi wao ulianza kwenye Mapinduzi ya Kilimo na kuelekea kwenye Mapinduzi ya Viwanda. Tunaona kabisa kwa mfano Uingereza ilianza na Agrarian revolution, ambayo ilikuwa ni agricultural revolution ikaja industry revolution na baadaye wakaenda kwenye commercial revolution na political revolution na hatimaye sasa hivi wako kwenye teknolojia ya maendeleo kabisa. Kwa hiyo kwa kweli kila nchi mchango wa kilimo ni mkubwa sana katika hatua ambayo wamefikia.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tumeona nchi nyingi sasa hivi zimefikia kwenye ugunduzi mkubwa wa kuboresha, yaani kuwa na huduma nzuri yaani service industry na sasa nyingi zimeingia katika uzalishaji wa teknolojia. Nina uhakika hatuna namna ya kukwepa kama taifa, na ndiyo maana katika hotuba yangu nilibainisha baadhi ya maeneo muhimu yanayohitaji msukumo wa kipekee na maboresho kuanzia mwaka 2019/2020. Maeneo hayo ni pamoja na maboresho ya sera, na Sheria, kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo, masoko ya uhakika ya mazao na bidhaa za kilimo, na kuwakinga wakulima na majanga kupitia Mfumo wa Bima ya Mazao. Ndiyo maana tumeanza mapitio ya sera ya kilimo ya mwaka 2013, mapitio ya sera ya ushirika pia ya mwaka 2002, pia tumeanza mchakato mkubwa wa kuanza mchakato wa kutunga Sheria ya Kilimo na kuandaa utaratibu wa Bima za Mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ili mabadiliko ya kweli ya kilimo yaweze kutokea lazima tuchukue hatua za kusimamia matumizi endelevu ya ardhi kwa kuwa na sera nzuri, na sheria ya kusimamia matumizi ya ardhi ya kilimo, ikiwa ni pamoja na kupima afya ya udongo ili kuwezesha wakulima kuongeza virutubishi vya udongo ardhini kulingana na mahitaji ya udongo. Vilevile matumizi endelevu ya maji ni muhimu sana katika kuongeza uzalishaji na tija ikizingatia mabadiliko makubwa ya tabianchi yanayotokea duniani na nchini kwetu.

Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya kweli pia yanahitaji uzalishaji wenye tija na faida katika minyororo ya thamani ya mazao yote; katika eneo hili Serikali imejipanga kuongeza matumizi ya pembejeo bora za kilimo ikiwa ni pamoja na uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora za mazao kama vile mahindi, mtama, ngano, ulezi, uwele, maharagwe, na jamii nyingine ya mikundi, alizeti, michikiti, ufuta, karanga, muhogo, parachichi na miwa. Mazao mengine ni kahawa, pamba, pareto, tumbaku, korosho, viazi mviringo, ndizi na zabibu.

Mheshimiwa Spika, tumeanza kuona mabadiliko katika ukuaji wa sekta ya kilimo. Takwimu rasmi za ukuaji wa kilimo zinaonesha kuwa sekta ya kilimo ilikuwa kwa asilimia 6.9 kwa mwaka 2014 na hizi takwimu ni baada ya kubadilisha ile re-base na Kambi Rasmi ya Upinzani ilitoa takwimu namna uchumi ulivyokua, sasa takwimu halisi ambazo ndizo sahihi zinaonesha kuwa kilimo kilikua kwa asilimia 6.9 kwa mwaka 2014, asilimia 5.4 kwa mwaka 2015, asilimia 4.8 kwa mwaka 2016, asilimia 5.9 kwa mwaka 2017 na asilimia 5.3 kwa mwaka 2018. Hizi ndizo official takwimu zinazoonesha ukuaji wa sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, ukuaji huu mzuri wa sekta ya kilimo umetuhakikishia usalama wa chakula nchini kwa muda wa miaka minne iliyopita. Kama nilivyosema kwenye hotuba yangu utoshelevu wa chakula kwa mwaka 2018/2019 ni asilimia 124. Hata hivyo kuna dalili za kutokea upungufu wa chakula katika baadhi ya maeneo kutokana na upungufu wa mvua na mvua kuchelewa katika badhi ya maeneo.

Mheshimiwa Spika, hivyo tuendelee kuhifadhi chakula katika ngazi ya kaya na Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula itanunua chakula cha kutosha na kuhifadhi kwa ajili ya kukabiliana na upungufu unaoweza kujitokeza. Hata hivyo niwahakikishie wananchi kwamba Serikali haitarajii kuzuia wakulima na wafanyabiashara kuuza mazao yao nje ya nchi, narudia hata hivyo niwahakikishie wananchi kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haitarajii kuzuia wakulima na wafanyabiashara kuuza mazao yao nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuongeza matumizi sahihi ya mbolea viuatilifu mbalimbali kama copper, sulfur, na matumizi ya teknolojia za kilimo. Pia tutaboresha matumizi ya dhana za kilimo na kuimarisha huduma za ugani, utafiti na mafunzo. Sanjari na kuongeza uzalishaji suala la masoko ya uhakika wa mazao yanayozalishwa limepewa na litaendelea kupewa kipaumbele kutoka na kuwepo kwa ongezeko la uzalishaji hapa nchini na mahitaji katika masomo ya ndani nje ya nchi. Masoko yataimarika zaidi kwa kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao yakiwemo mazao kama kahawa, mahindi, mbaazi, korosho, parachichi, pareto, tumbaku, mkonge matunda na mbogamboga. Aidha, tutaimarisha ukusanyaji wa takwimu za kilimo, huduma za fedha zinazotolewa kama mikopo na vitu vinginevyo, Bima ya Mazao, usafishaji, utunzaji wa mazao na kujenga uwezo wa wataalam wetu katika maeneo mbalimbali ili waweze kutoa huduma zile zinazohitajika kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo ya jumla naomba nitoe ufafanuzi wa maeneo machache kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja nyingi ambazo zimetolewa kama nilivyosema kwamba sitaweza kuzijibu zote zingine tutazijibu kwa maandishi. Hata hivyo naomba nianze na hoja namba moja ambayo ilikuwa imetolewa; kwamba hoja hii inahusu ushuru wa usafirishaji wa korosho ghafi nje ya nchi yaani Export Levy kurudishwa kwa wakulima kwa ajili ya kuendeendeleza zao la korosho. Hoja hii ilichangiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge, pia Mheshimiwa Cecil Mwambe naye alichangia hoja hiyo.

Mheshimiwa Spika, naomba nikumbushe kwamba Bunge lako Tukufu limeifanyia marekebisho Sheria ya fedha ya mwaka 2018, kifungu cha 17 (a). Kwa mujibu wa marekebisho hayo fedha za ushuru wa usafirishaji wa korosho ghafi nje nchi zitaingia katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Kwa sasa tasnia ya korosho inahudumiwa moja kwa moja na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, na Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, tulikaa wote hapa tulipitisha ile kwa pamoja. Kwa hiyo hilo sasa suala hilo tena halipo.

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili iliyotolewa ilikuwa inahusu Serikal iondoe ushuru kwenye Pembejeo za Kilimo kama mbolea, mbegu na viuatilifu. Hoja hiipia ilichangiwa na Mheshimiwa Neema Mgaya, naomba niseme mchango ulikuwa mzuri sana tunaipokea.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya ushuru wa forodha wa Afrika Mashariki (The EAC Costumers Management Act of 2004) na Sheria ya kodi ya ongezeko la thamani VAT Act of 2014, pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea, mbegu na viutalifu havitozwi kodi wala ushuru wowote. Naomba nirudie, pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea, mbegu na viuatilifu hazitozwi kodi wala ushuru wowote. Aidha, Serikali inaendelea kufanya maboresho ya tozo, ada, ushuru na kodi mbalimbali katika sekta ya kilimo kwa lengo la kuvutia wawekezaji na kuwaongezea wakulima kipato.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi miaka mitatu kuanzia mwaka 2015 Waheshimiwa Wabunge mlifanya kazi nzuri sana katika mjadala, mkasema kuna kodi nyingi sana ambazo ni kero ambazo ni tozo kwenye kilimo mkaiagiza na kuishauri Serikali iziondoe. Nyote mnakumbuka kwamba kuanzia mwaka 2015 jumla ya ushuru tozo na ada 105 zilifutwa kati ya kodi 146 zilizokuwa zinatozwa na kubainika kuwa kikwazo katika maendeleo ya sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa pembejeo Serikali katika mwaka 206/2017 ilifuta jumla ya tozo na ada saba katika tasnia ya mbegu, nne katika tasnia mbolea na moja katika mfuko wa pembejeo. Aidha, Serikali imefanya marekebisho ya kanuni zilizoanzisha tozo na ada hizo kwenye pembejeo ili kuwezesha utekelezaji wake kuwa mwepesi.

Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali imefanya marekebisho ya Kanuni ya Sheria ya Mbolea ya Mwaka 2011 (The Fertilizer Regulation of 2017) ambapo gharama za uhakiki wa ubora wa mbolea imepunguzwa kutoka dola 30,000 hadi kuwa dola 10,000, na muda wa majaribio umepunguzwa kutoka miaka mitatu hadi msimu mmoja katika maeneo mawili ya ikolojia tofauti. Wizara pia ilitunga Kanuni za Kusimamia Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja [Fertilizer Bulk Procurement System (BPS] ambapo imekadiliwa kupunguza bei ya mbolea kwa mtuamiaji wa mwisho kati ya asilimia 10 mpaka asilimia 40 ya bei.

Mheshimiwa Spika, hapa naomba nitoe maelezo kwa undani. Sasa hivi katika utafiti ambao tumeufanya na kuangalia bei ya mbolea nchini na maeneo yote duniani inaonekana kwamba mbolea gharama kubwa ya mbolea inaanzia pale mbolea inapowasili bandarini, kuanzia pale bandarini, gharama za kuitoa pale kuweka kwenye mifuko na kusafirisha mpaka kwa mkulima. Kwa utafiti uliofanyika unaonesha kwamba gharama zile ziko kati ya asilimia 40 mpaka asilimia 60. Kwa hiyo ina maana kwamba tukifanyia kazi vizuri katika hili eneo kuna uwezekano mkubwa mbolea zikashuka bei na zikawa na bei ambayo mkulima anaweza kufaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunakusudia kufanya marekebisho hayo na ndiyo maana tunaupitia upya huu mfumo na hivi kesho tumeita kikao cha wadau wote wanaonunua na kuagiza mbolea nchini wanakuja hapa Dodoma tuna mkutano nao kwa ajili ya kukaa na kujadiliana vizuri kuangalia gharama zote za uendeshaji ili kusudi ikiwezekana mbolea hii ambayo inaagizwa basi ipunguzwe bei na wakulima wetu wapate mbolea ambayo ni sahihi na ile yenye bei nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya tatu ambayo ilikuwa inahusu kuteua Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Korosho kwa mujibu wa Sheria. Hoja hii ilichangiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, pia Mheshimiwa Abdallah Chikota amechangia vizuri sana na wengine waliochangia.

Mheshimiwa Spika, mamlaka ya uteuzi zimeanza uundaji Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania kwa mujibu wa sheria ya tasnia ya korosho namba 18 ya mwaka 2009 na kanuni za korosho za mwaka 2010. Kazi hii itakamilishwa na Serikali baada ya muda mfupi ujao. Naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu tayari tulishamteua Kaimu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Korosho ana takriban wiki mbili alisharipoti kazini na wiki hii tunakamilisha uundaji wa Bodi Wajumbe watatangazwa. Kwa hiyo ninauhakika sasa jukumu lile ambalo wanalo lile la kisheria la kuhakikisha wanasimamia zao la korosho wataendelea kusimamia jukumu hilo moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, lakini naomba nitoe angalizo na utofauti uliopo. Kulikuwa na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, bodi ile ilikuwa haisimamii zao, ilienda kama mnunuzi, na kama wanazo fedha wataendelea kununua wakishindana na wafanyabiashara wengine watanunua na kuendelea kuuza. Lakini Bodi ya Korosho itasimamia taratibu zote kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika, hoja ya nne ilikuwa ni wadau mbalimbali wa korosho hususani halmashauri bado hawajalipwa fedha na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yao. Hoja hii pia ilichangiwa na Wajumbe wengi na Waheshimiwa Wabunge wengi akiwemo Mhandisi Edwin Ngonyani, pia Mheshimiwa Chikota alichangia na wengine wengi.

Mheshimiwa Spika, Serikali imelipa jumla ya bilioni 26.3 kwa watoa huduma mbalimbali walioko kwenye mnyororo wa thamani wa korosho. Watoa huduma hao ni pamoja na wasafirishaji, AMCOS Vyama Vikuu vya Ushirika, waendesha maghala na gharama za magunia. Kwa kuwa uwamuzi wa Serikali wa kununua korosho kulilenga kumnufaisha mkulima hivyo baadhi ya gharama zimebebwa na Serikali zikiwemo Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninachotaka kusema ni kwamba katika wale wadau ambao bado hawajalipwa sasa hivi tukishapata fedha tutahakikisha kwamba nao basi wanalipwa; lakini lazima tukumbuke kanuni inayoelekeza; Serikali moja haiwezi kuitoza kodi Serikali nyingine. Kwa hiyo ukisema Serikali Kuu ilipe Serikali za Mitaa kidogo kwa mujibu wa kanuni na sheria za kodi ni tofauti. Kwa hiyo hapa tunapozungumzia tunazungumzia wale wadau wengine wote waliotoa huduma ambao si Serikali, hao wote tuna uhakika watalipwa bila tatizo lolote.

Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa na hoja kwamba wakulima wengi bado wanadai, naomba nikiri kabisa kweli kuna wakulima mpaka sasa hivi hatujamaliza kuwalipa, zaidi ya bilioni 100 za malipo ya korosho bado zinadaiwa, na mimi nakubaliana kabisa na Waheshimiwa Wabunge, wameliongelea suala hili kwa uchungu mkubwa na mimi kama Waziri wa Kilimo linaniumiza sana, nakosa hata usingizi kwa sababu mimi tungependa wakulima wetu wapate fedha kwa wakati ili waendelee kulima; hatutaki kuona wakulima wanahangaika. Kwa hiyo hili kwa kweli sote linatusumbua, lakini tatizo limekuwa ni upatikanaji tu wa fedha za kutosha za kuhakikisha kwamba tunalilipa.

Mheshimiwa Spika, naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inaendelea kufanya malipo kwa wakulima kulingana na uhakiki uliofanyika; hadi kufikia Mei mwaka 2019 Serikali ilikusanya jumla ya tani 222,830.5 za korosho ghafi zenye thamani ya shilingi bilioni 722, 775,186,000, kati ya hizi fedha jumla ya shilingi bilioni 623,680,510,416 zimelipwa kwa wakulima moja kwa moja ambayo hii ni sawa na asilimia 86 ya madai yote.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kweli Serikali tumejitahidi hatukutegemea kwanza halikuwa lengo kwamba zile fedha labda tutachelewa, tulidhani kwamba baada ya kukusanya tukiuza, tungezungusha zile fedha wakulima wote wangekuwa wamelipwa. Mpaka sasa hivi hatujauza lakini Serikali imelipa zaidi ya bilioni 623, tumejitahidi. Hii haina maana kwamba tunabeza wale ambao hawajalipwa kwa sababu moja ya watu ambao hawajalipwa ni wale wakulima wakubwa ambao mimi nataka walipwe ili waendelee kulima zaidi na kuhudumia kilimo. Kwa hiyo hili tutaendelea kulifanyia kazi na kwa muda mfupi nina uhakika Serikali tutaliangalia na kuhakikisha kwamba tunapata fedha kwingine hata kwa kukopa ili wakulima hawa walime waendelee kupalilia korosho zao na waendelee kuzalisha, kwa hiyo hili tutaendelea kulishughulikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja nyingine kwamba tujikite kwenye ubanguaji, wawekezaji kwenye viwanda vya Serikali walioshindwa kuviendeleza wanyang’anywe. Nakubaliana kabisa na maoni ya Waheshimiwa Wabunge, nchi yetu ni kubwa wala hatuwezi kulinganisha na nchi nyingi, ni nchi iliyobahatika kuwa na ardhi nzuri yenye uwezo mkubwa, yenye watu wengi wenye utaalam mkubwa. Sasa hivi Msumbiji wanabangua korosho zao kwa asilimia 75, sisi nchi kubwa yenye wataalam wengi, korosho zetu zote tunauza zikiwa ghafi. Hii haikubaliki na ndio maana hata viwanda tulivyokuwa navyo vyote, Mheshimiwa Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alianzisha viwanda 12, tukavibinafsisha, tukawauzia watu, baadhi ya watu waliochukua wameshindwa kuviendeleza wala havifanyi ile kazi, ndio maana kwa sababu hiyo Serikali tumeamua kuvirudisha baadhi ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe takwimu, viwanda vinne sasa hivi tumeshavirudisha mikononi mwa Serikali ili kusudi tuwekeze, viendelee na kazi ya kubangua, kusudi korosho zetu zote zibanguliwe hapa nchini. Kwa hiyo tumechukua Kiwanda cha Kubangua Korosho cha Lindi kile cha Buko, wote mnajua. Pia tumechukua kiwanda cha Newala yaani Agrow Focus nacho tumekitaifisha, tumeshakirudisha, tumemnyang’anya yule mwekezaji. Vile vile Kiwanda cha Mtama yaani kile cha Lindi Farmers tumekichukua, Kiwanda cha Nachingwea nacho tumekichukua. Kwa hiyo, viwanda vyote hivi tumeshavirudisha, sasa hivi tunatafuta wawekezaji wapya ili wawekeze na wahakikishe kwamba kwa kweli hivi viwanda vinabangua.

Mheshimiwa Spika, najua kulikuwa na tatizo kubwa ambalo walikuwa wanalisema, walikuwa wanasema wanashindwa kushindana kwenye soko kwa sababu wanakosa malighafi, lakini nataka nilihakikishie Bunge tumejipanga vizuri kuangalia upya sera yetu ya uuzaji ili kusudi viwanda vyote vitakavyoanzishwa vihakikishiwe kupatiwa malighafi ili vitoe ajira na kuongeza thamani. Kwa hiyo, hiyo sera itakuwa nzuri sana.

Aidha, Serikali itaendelea kuhamasisha wawekezaji wanye viwanda vya kubangua korosho ili kuongeza uwezo wa ndani wa ubanguaji na kukuza ajira. Serikali itaendelea kutafuta wanunuzi wa korosho zilizohifadhiwa kwenye maghala ili kutoa nafasi ya kuhifadhi korosho kwa msimu ujao. Nitumie fursa hii kuwaomba hata Waheshimiwa Wabunge, wanaweza wakaunda SACCOS ya kwao wakaanzisha viwanda, hebu tuongoze kwa vitendo, tunaweza tukaanzisha viwanda viwili, vitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna viwanda pale vya kubangua korosho unaweza ukaanzisha kwa Sh.1,000,000,000. Nina uhakika kabisa Waheshimiwa Wabunge tulioko hapa haviwezi kutushinda, kinachohitajika ni dhamira ya kweli ya sisi wenyewe kwamba tunataka kweli tujenge viwanda, tunaweza, hili linawezekana, ukilinganisha na mikopo ambayo huwa tunakopa. Tukiwekeza nina uhakika nchi hii itasogea mbele na tutasogea sana.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kuhusu mawakala ambao hawajalipwa wale ambao walisambaza pembejeo mwaka 2015/2016. Nakubaliana kabisa kwamba kulikuwa na mawakala wengi lakini tulipofanya utafiti, tulipofanya uchunguzi imebainika karibu kila wakala alidanganya, mawakala wote walidanganya. Sasa kama wamedanganya, takwimu ni feki unamlipaje?

Kwa hiyo, sisi tulichokifanya sasa hivi katika hili suala tulipoona kwamba wote kila mtu ana udanganyifu, tumechukua takwimu zao zote tumepeleka TAKUKURU, wanaendelea na uchunguzi, ukikamilika wale watakaobainika kwa kweli hawakudanganya hao wote tutawalipa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja Serikali kupelekea pembejeo kwa wakulima kwa wakati, bei nafuu na kuweka mfumo mzuri wa upatikanaji wake. Hoja hiii imechangiwa na Wabunge mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji. Pia Mheshimiwa Ngalawa, Mheshimiwa Semesi, Mheshimiwa Kakoso na wengine wengi wamechangia hii hoja. Wizara inakamilisha mapitio wa mifumo ya uzalishaji, uagizaji na usambazaji wa pembejeo ili kuandaa mfumo madhubuti utakaohakikisha kwamba pembejeo zilizozalishwa au kuagizwa nje zina ubora na zinapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu kwa mkulima. Aidha, Serikali itahamasisha na kusimamia usambazaji wa pembejeo kwa kuzingatia kalenda ya kilimo katika maeneo mbalimbali nchini kulingana na kanda za kiikolojia za kilimo ili pembejeo zifike kwa wakati unaostahili.

Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali imeliagiza Shirika la Reli Tanzania (TRC) kutoa kipaumbele cha kusafirisha mbolea kwenda mikoa yenye miundombinu ya reli kwa kuwa gharama za usafirishaji kwa njia ya reli ni nafuu ikilinganishwa na usafiri wa barabara. Hili mpaka kuanzia bandarini pale, bandarini pia tumeongea na wenzetu wa bandari kwamba watoe kipaumbele mbolea zinapowasili ziweze mara moja kupakuliwa na kupelekwa katika maghala na ziweze kusafirishwa ziende kule zinakohitajika. Tunajua misimu inatofautiana, kwa hiyo, tumetoa hicho kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa na suala linahusu bajeti ya kilimo kwa kuzingatia Maazimio ya Malabo na Maputo. Hoja hii imechangiwa sana na Kamati ya Kudumu ya Bunge na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imelisema na Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema kwamba bajeti ya kilimo ni ndogo. Naomba nitoe ufafanuzi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kusema bajeti tu haitoshi, ni kweli haitoshi na hakuna siku ambayo tutasema bajeti inatosha, lakini upangaji wa bajeti na vipaumbele unategemeana na nchi moja na nchi nyingine, lakini tunazingatia majukumu ya Serikali ni nini katika hiyo. Kwa mfano katika nchi yetu, Serikali haiendi kulima mashamba, Serikali kazi yake ni kutengeneza miundombinu ili sekta binafsi zikalime, wakawekeza, wakafanye biashara.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunachosema sisi ni kwamba, Serikali ndio unaweza ukaiangalia bajeti ya kilimo lakini kitaalam zaidi bajeti ya kilimo haipimwi kwa hela zilizowekwa kwenye Wizara ya Kilimo peke yake, fedha zote ambazo ziko TAMISEMI kwa asilimia kubwa zile ambazo ziko TARURA zote zinatengeneza barabara zinazohudumia kilimo. Fedha zilizoko Wizara ya Uvuvi, fedha zilizoko kwenye Wizara mbalimbali, kwa mfano sasa hivi Wizara ya Nishati wanasambaza umeme vijijini, ule umeme ni kwa ajili ya kuhudumia wakulima. Kwa hiyo yote hiyo tunaita ni bajeti ya kilimo. Barabara mbalimbali zinajengwa barabara kubwa, reli zinajengwa, viwanja vya ndege vinajengwa, vyote hivyo ni kwa ajili ya kuhudumia wakulima. Kwa hiyo ukitaka upate bajeti ya kilimo peke yake ni vigumu, zote hizo zichukue, angalia, sasa ndio unaweza ukakokotoa ukapata bajeti ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema ni kwamba hatuwezi kusema tunaweza kutekeleza hiyo kama ilivyo lakini lazima tuiangalie kwa vipaumbele ambavyo tunatekeleza na nina imani bajeti zilizotengwa kwenye Miundombinu, Nishati, Mawasiliano, Uvuvi, TAMISEMI zote ni kwa ajili ya kuhudumia kilimo chetu na hivyo nina uhakika kabisa kwamba bajeti ni kubwa na itatosheleza katika kutekeleza majukumu ya mwaka huu.

Mheshimiwa Spika, aidha, Wizara na Taasisi mbalimbali kama vile Viwanda, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Maji, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Nishati zinachangia katika utekelezaji na ukuaji wa Sekta ya Kilimo. Kwa mfano Wizara ya Ardhi, ardhi yote hii ikipimwa na tunasema kwamba ikipimwa ikaeleweka ardhi ya kilimo ni hii tayari watakuwa wamechangia na itakuwa ni bajeti ya kilimo. Pia kuna ASDP II inatekelezwa na Wizara za Kisekta ikiwepo Wizara ya Kilimo, lakini kuna Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Maji, TAMISEMI, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Uwekezaji na kadhalika. Zote hizo ukiangalia shughuli zao kwa asilimia karibu 80% zote zinashughulikia masuala ya kilimo. Kwa hiyo kilimo, nasema ni suala mtambuka na hivyo bajeti yake bado ni kubwa na inatosheleza.

Mheshimiwa Spika, wapo Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia kuhusu masoko na wamezungumza kwa undani sana. Hoja hii ilichangiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mifugo na Maji, Kambi Rasmi ya Upinzani walisema, lakini pia baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walichangia sana kuhusiana na masoko. Serikali inaendelea kutafuta masoko ya uhakika ya mazao mbalimbali ndani na nje ya nchi. Kwa kuanzia tumeanzisha Kitengo cha Masoko katika Wizara ya Kilimo ambacho hakikuwepo ili kihakikishe kwamba kwa kweli kinafanya market intelligence, kitafute masoko nje, kitafute masoko ndani na hata ndani hapa masoko bado ni makubwa bado hatujayatumia vizuri. Kwa hiyo, kwa kupitia kitengo hiki ni imani yangu kwamba tutajitahidi sana kuhakikisha hili tunalifanya.

Mheshimiwa Spika, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kutangaza fursa za masoko ya wakulima, kuingia mikataba ya kibiashara baina ya Tanzania na nchi mbalimbali na kuunganisha wakulima moja kwa moja na wanunuzi kama nitakavyowaeleza hapo baadaye. Aidha, Wizara ya Kilimo inaendelea kutoa vibali vya kuuza na kusafirisha mazao nje ya nchi. Kwa mfano, kati ya mwezi Januari, 2019 na Aprili, 2019; jumla ya tani 22,201 za mbaazi zimesafirishwa kwenda nchi za Qatar, Dubai, Oman, Pakistan, Bangladesh, Malaysia, Kuwait, Indonesia, United Emirates Republic na Ureno. Aidha, katika kipindi hicho jumla ya tani 80,648 za mahindi ziliuzwa nchi za Rwanda, Uganda, Congo, Kenya, Burundi, Malawi, Oman, Sudan ya Kusini na kadhalika na vilevile makampuni yaliyosajiliwa yamenunua mhogo mkavu kati ya tani 254.52 kwa ajili ya kusafirisha kwenda nchini China na kuna kampuni kama tano ambazo zimeshapata vibali vya kusafirisha mhogo.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninachotaka kuwaambia Waheshimiwa Wabunge ni kwamba, hizi jitihada tuendelee nazo. Tutaendelee kuzungumza na nchi mbalimbali, tutaendelea kutafuta wanunuzi mbalimbali wa mazao yetu yote, yale ambayo tunayo na yale mengine tunayoweza kuanzisha ili kuhakikisha kwamba kilimo kinachangia kwa kiwango kikubwa katika uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, Serikali ifanye tafiti kwa zao la parachichi kuendana na hali halisi ya mabadiliko ya teknolojia. Nakubaliana kabisa na hoja hizi zilizotolewa na Mheshimiwa Peter Msigwa, Mheshimiwa Neema Mgaya wamechangia kweli, lakini Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) inafanya utafiti wa kuzalisha mbegu pamoja na miche bora ya parachichi na kuisambaza kwa wakulima. Vilevile Serikali imepeleka taarifa muhimu za kisayansi zinazohitajika kwa ajili ya masoko ya parachichi katika nchi ya China na nchi za Ulaya. Taarifa hizo zimefungua majadiliano kwa lengo la kuweka makubaliano ya kibiashara baina ya Tanzania na nchi hizo. Ni imani yetu kwamba tukishaweka makubaliano yatasaidia sana katika kuhakikisha kwamba kilimo chetu kinakwenda mbele na tunapata masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulitolewa hoja nyingine kwamba kipaumbele kitolewe kupeleka fedha katika Vyuo vya Mafunzo na Taasisi za Utafiti. Hoja hii imechangiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge. Serikali imekuwa ikiongeza fedha kwa ajili ya utafiti mwaka hadi mwaka na hilo ndio lengo letu kwa sababu utafiti ndio uhai wa kilimo, bila utafiti hakuna kilimo. Katika mwaka 2018/2019, jumla ya Sh.697,905,309 zilitengwa kwa ajili ya ukarabati wa maabara za kibaiolojia na bioteknolojia za TARI Tengeru ambapo ilitengewa Sh.399,999,630 na maabara ya kusindika mvinyo ya TARI Makutupora ambayo ilitengewa Sh.297,906,300 kupitia COSTECH. Katika mwaka wa fedha 2019/2020, Wizara imetenga Sh.9,224,033,150 katika bajeti ya fedha ya maendeleo na matumizi ya kawaida. Aidha, TARI Naliendele imetengewa Sh.5,610,547,100 kwa ajili ya kuimarisha na kuendeleza utafiti wa zao la korosho.

Mheshimiwa Spika, zipo hoja nyingi ambazo zimetolewa, lakini kulikuwa na hoja kuhusu utafiti wa udongo na kwamba Serikali ikamilishe kwa haraka. Naomba nilitarifu Bunge lako Tukufu na hoja hii imechangiwa na watu wengi sana. Tathmini ya udongo hadi sasa imefanyika katika mikoa 16 kati ya 26 ya Tanzania Bara na baadhi ya ramani zimeshatolewa kwa vipimo vya aina mbalimbali. Tumeshamaliza katika kanda zote kama nilivyoahidi kwenye Bunge la mwezi wa Pili kwamba tunafanya tathmini katika kanda zetu zote kuweza kubaini udongo uliopo na kuangalia virutubishi ambavyo vinakosekana katika ule udongo.

Mheshimiwa Spika, naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba kazi hii imekamilika na tayari tunayo ramani inayoonesha nchi nzima, ninazo hapa ramani zinaonesha ni aina gani, udongo wetu una nini, vitu gani vinakosekana, vipo hapa na ramani kubwa tunazo tumeziacha pale chini. Ramani zimekamilika, kwa hiyo tuna uhakika, hii kazi imekamilika lakini tunaendelea sasa kwenda mkoa kwa mkoa ili tukipata mkoa kwa mkoa tutajua mkoa huu unahitaji nini na kinakosekana nini.

Mheshimiwa Spika, lengo la hii yote ni nini? Lengo hasa ni kutaka kujua kwamba wanapotumia mbolea tuweze kuwaambia mbolea ambazo ni sahihi kulingana na mahitaji ya udongo na wakati mwingine watu wananunua mbolea unakuta kwamba labda hiyo mbolea vile virutubisho vilivyopo mle ndani havihitajiki. Kwa hiyo ndio maana tumeamua kwamba kuanzia mwaka huu tunafanya jitihada na wawekezaji ili wajenge kiwanda cha kuchanganyia mbolea. Baada ya utafiti huu tuwe na kiwanda sasa ambacho tumekubaliana kinajengwa pale Dar es Salaam, tunatumia magodauni ya pale Dar es Salaam kichanganywe mbolea yaani ile blending plant, tunaweka mwaka huu, ili kusudi wakulima wakisema mahitaji ya udongo wangu yako hivi, basi tunajua mbolea anayohitaji inatakiwa hii na hii. Nina imani kama hilo litafanyika tutaendelea vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kuhus uzalishaji wa mbegu za mafuta, lakini pia uzalishaji wa mbegu hapa nchini bado hautoshelezi. Nakiri kabisa kwamba tuna changamoto kubwa kwenye uzalishaji wa mbegu tunazozihitaji na mpaka sasa hivi uwezo wa nchi kuzalisha mbegu ni karibu asilimia 64 tu ya mahitaji yote, lakini tumeamua kuweka jitihada na kuweka mikakati ya kutosha kuhakikisha kwamba tunapata mbegu zile ambazo tunazihitaji. Kwa hiyo Serikali imeamua kuwekeza vya kutosha katika uzalishaji wa mbegu za mafuta ili kujitosheleza kwa mafuta ya kura na ziada kuuza nje.

Mheshimiwa Spika, kwa kuanzia Wizara imeanza mkakati wa kundeleza zao la mchikichi unaolenga kuzalisha mbegu bora za michikichi kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2018/2019 mpaka 2021/2022. Katika mwaka 2019/2020, Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine wakiwemo JKT na Magereza itazalishwa miche ya michikichi 5,000,000 kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo. Mkakati huu unatekelezwa sambamba na kuwapatia wakulima teknolojia bora za kuongeza thamani kupitia SIDO, TADB, CAMARTEC, NDC na UNIDO.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kabisa kwamba kwa kweli tunahitaji mbegu zilizo bora na kama nchi lazima tuwekeze kwenye mbegu zilizo bora. Hili tuna imani kabisa tutalifanyia kazi vizuri na nitumie fursa hii kuziomba taasisi zingine hapa tumesema JKT na Magereza lakini nina uhakika taasisi zingine zinaweza zikawekeza kwenye uzalishaji wa mbegu, taasisi binafsi, taasisi za umma hasa wanawekeza lakini bado haitoshi.

Mheshimiwa Spika, kwa nini tunahitaji mbegu za kutosha kwa upande wa michikichi? Nchi ya Malaysia ambayo miaka ya nyuma ilichukua mbegu za michikichi kutoka Tanzania inazalisha mafuta, inazalisha mafuta yanayotokana na michikichi kwa wingi sana duniani, lakini mbegu zilitoka kwetu. Sisi wenye ardhi nzuri na ambao tulitoa mbegu, uzalishaji wetu uko chini. Sasa hivi tunatumia zaidi ya bilioni 674 kwa mwaka kuagiza mafuta ya kula, wakati uwezo wa kuzalisha hapa nchini upo, tuna uwezo wa kulima alizeti kwa wingi, tuna uwezo wa kulima michikichi kwa wingi, tuna uwezo wa kulima karanga, tuna uwezo wa kulima mbegu za pamba na nyinginezo, tukazalisha mafuta ya kutosheleza nchi yetu. Kwa nini kila wakati tuagize au tutumie fedha zetu kuagiza nchi za nje wakati sisi tuna uwezo wakuzalisha? Hili ni lazima tulivalie njuga na nitaomba ushirikiano wa Waheshimiwa Wabunge wote tuhakikishe kwa kweli hili tunalisimamia kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia pamoja na uzalishaji wa miche ya michickichi Serikali kupitia TARI inakamilisha utafiti wa mbegu mpya za alizeti zenye uwezo wa kutoa mavuno na mafuta mengi, ili kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora kwa gharama nafuu badala ya kuagiza kutoka nchi za nje. Bahati nzuri nimepata maombi mengi kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge, wananiuliza na wananiomba mbegu bora, wengine wameomba za michikichi, na wengine wameomba za alizeti.

Mheshimiwa Spika, na mimi niseme tu nitahakikisha wote mnapata hizo mbegu, ili kusudi mwende kulima kwa sababu najua ninyi Waheshimiwa Wabunge ndio wadau wangu wakubwa wa kilimo; na ninyi mkilima ndiyo itakuwa mfano hata kwa wakulima kuja kuiga na kuona namna mnavyolima. Maana nchi hii tumefikia mahali unakuta mtu ana ardhi pale hata kupanda miche miwili ya nyanya pale nyumbani hapandi, halafu tunaagiza ilhali ardhi nzuri na kila kitu tunacho. Hii neeme tuliyopewa na Mungu lazima tuitumie vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zipo hoja ambazo wajumbe wamechangia. Suala la umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, wamezungumzia sana suala la umwagiliaji; na mimi niungane na ufafanuzi mzuri sana alioutoa Naibu Waziri. Nataka niwaambie, katika skimu tulizonazo zote zilizokuwa chini ya umwagiliaji ziko zaidi ya 2,600. Huwezi kupata skimu 10 za mfano zinazofanya kazi, kwa hiyo skimu zote zina matatizo; na sisi tumeangalia ule Muundo wa Tume ya Umwagiliaji tukaona hapa lazima tuifumue. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeshaifumua ndiyo maana tumeanza, sasa tunasema wiki hii tunakamilisha muundo mzima na uongozi mpya, na tunawagawia maeneo ya kusimamia. Tunataka kwenye kanda abaki mmoja kwa sababu kwenye kanda hakuna kilimo. Kwenye mkoa wanakuwa wawili, lakini tunataka wale wote, Maafisa Umwagiliaji, ma-engineer wa umwagiliaji waende kwenye halmashauri zetu zinazoshughulika na kilimo wakasimamie skimu kule chini na kila mtu atawekewa malengo ya kuhakikisha kwamba anasimamia. Mimi nina uhakika tukilisimamia vizuri hili litaweza kutatua tatizo letu la miradi mbalimbali ya umwagiliaji ambayo ilikuwa haifanyi vizuri katika nchi yetu, kwa hiyo hili tumeliwekea mkakati wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ipo hoja ambayo Waheshimiwa wajumbe pia, wamezungumzia. Wamezungumzia suala la kahawa; na mimi ni mdau wa kahawa, naijua kahawa kwa sababu nimekulia kahawa. Nimefurahi sana mlivyoichangia kahawa, nimeona Mheshimiwa Selasini na Waheshimiwa Wabunge wengi wameichangia sana kahawa.

Mheshimiwa Spika, kahawa lilikuwa ni zao la mfano, lilikuwa linatoa mchango mkubwa sana kwa fedha za kigeni miaka ya nyuma, lakini sasahivi limeshuka uzalishaji, tunazalisha takribani tani elfu 50, sasa hivi tumesema tumezalisha tani elfu 64, lengo tunataka tuzalishe tani elfu 80, hazitoshi. Tumeweka mkakati kwenye uzalishaji, wenzetu wa TACRI wakishirikiana na Bodi ya Kahawa tumeamua kuanzisha uzalishaji wa miche ya kisasa, ili kuisambaza kwa wakulima mbalimbali na hili tutalisiamamia ili tupate miche iliyo bora ambayo itaongeza uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kuna tatizo la bei, wengi wamezungumzia bei, na mimi nimeona kuna tatizo la bei. Mwaka huu nilipoongea na wazalishaji wanasema tunaweza tukapata kahawa safi tani 50,000, pure coffee; nimewauliza wanunuzi wanne wakubwa duniani watuambie wanahitaji tani ngapi? Wanahitaji tani 65,000. Kwa hiyo, ina maana mahitaji ni makubwa kuliko tulichozalisha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukasema kama hiyo ndio hali basi tuunde kamati maalum ndani ya Wizara, lakini Wizara inatoa mmoja iwe ni kamati huru, tumechukua Benki Kuu, Wizara ya Fedha na taasisi mbalimbali; tumeunda kamati ili ikutane na wanunuzi wakubwa hawa wajadiliane juu ya bei; wakikubaliana iwe ni kazi ya kuuza tu si tena mara kwenye mnada mara nini na nini. Sisi kwenye mnada tunataka twende tupeleke zile zitakazokuwa zimebaki ambazo zitakua hazijanunuliwa ndio maana Naibu Waziri amesema tunasisitiza direct selling, uuzaji wa moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, Dunia nzima nchi nyingi zimeenda katika mikataba ya moja kwa moja, Rwanda wamefunga mkataba na Ujerumani wa miaka kadhaa, na sisi lazima tufike mahali tusaini mikataba ya mauziano ya muda mrefu, hapo ndipo tutapata ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili bei. Si kila mwaka eti tutegemee soko watu wa-bid pale, wakiingia kwenye collussion bei inakuwa ndogo wakulima hawafaidiki na sisi utaalamu wetu wengine ni mdogo. Kwa hiyo tunafikiri hii timu itafanya kazi vizuri na nina uhakika baada ya wiki mbili watakuwa wamemaliza. Kwa hiyo, katika msimu huu tutatumia njia ya mauzo ya moja kwa moja na zile zitakazobaki ndizo tutazipaleka kwenye minada. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ya pili kwenye minada hii, minada ya kahawa, tulichokubaliana tunafanya kwenye kanda. Kanda ya Ziwa utafanyika mnada kule Kagera, Kanda ya Kaskazini watafanyia Moshi, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mbeya, Rukwa, Songwe watafanyia Songwe, na Ruvuma pia kutakuwa na Kanda, tutakuwa na kana nne ambazo minada itafanyika. Lengo ni kupunguza gharama kwa ananchi za kuhangaika kwenda kupeleka kahawa yao kule Moshi kwa ajili ya kwenda kuuza kwa hiyo; sasa wanunuzi watakwenda kule kwa hiyo, tuna imani itasaidia kupunguza changamoto zinazotokana na zao la kahawa.

Mheshimiwa Spika, lakini kuna pareto, mmezungumza sasahivi zao la pareto ndio nchi pekee inayozalisha. Pamoja na kwamba, tunazalisha kidogo, lakini ndio nchi pekee. Takwimu zimetolewa za bei za pareto, lakini hazikuwa sahihi sana.

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema mimi ni kwamba pareto hii ndiyo tunayotaka tuitumie katika uwekezaji wa kuanzisha viwanda vya viuatilifu. Viuatilifu ili vianzishwe vitatumia pareto yetu. Kwa hiyo mimi nina imani hizi jitihada zitasaidia na zitazaa matunda; lakini pia tunahitaji anunuzi wengine. Sasa hivi kuna mnunuzi mmoja, mnunuzi mmoja atashindana na nani? Lazima kuwe na ushindani ndio tunaweza kupata bei nzuri. Kwa hiyo hili tutalifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la mkonge. Miaka ya nyuma Tanzania ilikuwa inaongoza kuuza mkonge nchi za nje, tuliongoza kwa uzalishaji. Sasa hivi tumeshuka tunazalisha kidogo sana. Tumeamua kurudisha heshima ya nchi yetu kuhakikisha tunazalisha mkonge iwezekanavyo. Mashamba ya mkonge yote lazima yafufuliwe na mengine mapya yaanzishwe na changamoto zote tuondokanenazo. Imekuwa ni aibu tunatumia fedha nyingi kuagiza magunia nchi za nje, tunayaleta hapa ilhali tuna uwezo hata wa kutengeneza magunia ya kwetu, lakini pia mahitaji ya mkonge duniani bado ni makubwa. Kwa hiyo tunafikiri nchi yetu lazima irudi kwenye mstari.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kidogo kuhusu zao la tumbaku. Najua muda hautatosha. Tumbaku ina changamoto nyingi na kuna baadhi ya wanunuzi wako wanne tu wakubwa. Mmoja ametoa tishio kwamba, anakusudia kujiondoa mwakani, hajaingia kwenye mkataba. Najua wananchi wanaolima zao la tumbaku wamepata mfadhaiko kidogo. Hata hivyo nataka niwahakikishie kwamba Serikali yenu inafanya majadiliano na huyu mnunuzi, lakini pia tunatafuta wanunuzi wengine. Sasa hivi tumekwenda China tunafanya majadiliano. Tumewaalika waje kuangalia, lakini pia wao wanasema wana mbegu wanazozitaka. Tunataka watuletee hizo zifanyie majaribio waanze kulima. Pia tunaangalia nchi nyingine zinazohitaji hiyo tumbaku. Kwa hiyo pamoja na mambo mengine mimi nina imani mikakati tuliyoiweka itasaidia sana kutatua hili tatizo.

Mheshimiwa Spika, kuna hoja imetolewa kuhusiana na Maafisa Ugani. Maafisa Ugani kweli ni changamoto na mahitaji ni makubwa. Maafisa Ugani kwa mujibu wa muundo wetu wa Serikali wako chini ya TAMISEMI, wale ndio wanasimamia kilimo kule. Sisi kama Wizara ya Kilimo tunatengeneza Sera, tunatengeneza taratibu na miongozo ya kilimo, lakini wanaoenda kusimamia ni wale. Hata hivyo kuna vijiji havina, lakini hata vijiji vingine vina Maafisa Ugani ambako Maafisa Ugani wengine wanakaa bila kufanya kazi. Kwa hiyo sasa hivi kama Serikali tunakaa pamoja na TAMISEMI tunakuja na utaratibu mpya wa kuwasainisha mikataba ya namna ya kusimamia kilimo katika maeneo ambayo wanayasimamia. Kuhusu hoja kuongeza Maafisa Ugani hii tunakubaliananayo tutaendelea kuifanyia kazi kadiri bajeti itakavyoruhusu tutaweza kuendelea kuajiri hao wakulima.

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala moja la msingi. Tumeanzisha usajili wa wakulima. Lengo la usajili wa wakulima ni nini?

Mheshimiwa Spika, kwanza kama nilivyosema wakati nawasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara, tumeanza zoezi la usajili wa wakulima wote nchini. Lengo la zoezi hili ni kutaka kutambua walipo, wanalima nini? Wana maeneo yenye ukubwa kiasi gani? Wanahitaji pembejeo za namna gani? Wanahitaji zana gani? Wanahitaji msaada gani? Tukiwatambua hawa wakulima ndio tutaweza kuwahudumia; unamhudumiaje mtu ambaye hujui? Tunataka kila zao tujue kuna wakulima wangapi? Wanalima eneo kiasi gani? Kwa hiyo, hayo ndio tumeyaanzisha.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe taarifa; na kuna mmoja hapa amesema takwimu hazieleweki, nini na nini; naomba niseme, mpaka sasa hivi mazao ya kipaumble ambayo tayari tueshasajili, tumesajili wakulima 1,669,699, hao ndio tunaotegemea kuwasajili. Tuliowasajili ni 1,464,827 ambao ni asilimia 87.3 katika mazao nane ya msingi, yaani kahawa, chai, kosroho, miwa, tumbaku, na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali kwamba mambo yote mengine tutawajibu Waheshimiwa Wabunge, hoja najua ni nyingi, lakini nitumie fursa hii, nawashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kutoa ufafanuzi wa baadhi ya maeneo machache kuhusu hoja hii ya Wizara ya Kilimo. Baada ya kusema hayo niwaombe Wabunge kwa heshima kubwa kabisa mkiwa wadau wa chakula, mkiwa wadau wa kilimo, wote kwa pamoja muipitishe bajeti yangu bila matatizo.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naafiki.