Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwanza nitoe pole kwa Wanzazibari kwa kufiwa, kwa kuondokewa na Viongozi wawili muhimu, Mheshimiwa Ally Juma Shemuhuna, na Mheshimiwa Ally Fereji Tamimu, Mwenyezi Mungu awaweke mahali pema.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri kwa hotuba nzuri na nizungumze machache tu katika hii Sekta ya Kilimo kwamba ukiacha malighafi ya mazao ambayo wenye viwanda pia wana mashamba kama viwanda vya sukari ambavyo kuna mashamba ya miwa, viwanda vya chai na mashamba makubwa ya mpunga ambayo yana viwanda vyake kama yale ya Kapunga kule Mbarali na viwanda vya maparachichi, tumekuwa tunapata matatizo makubwa kwenye mnyororo wa thamani kwenye viwanda vya mazao ambayo hayana mashamba kama korosho, viwanda vya nguo, viwanda vya kukamua mafuta, alizeti, pamba na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, nizungumze machache tu katika hii sekta ya kilimo, kwamba ukiacha malighafi ya mazao ambayo wenye viwanda pia wana mashamba kama viwanda vya sukari ambavyo kuna mashamba ya miwa, viwanda vya chai, na mashamba makubwa ya mpunga ambayo yana viwanda vyake kama yale ya Kapunga kule Mbarali na viwanda vya maparachichi.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tunapata matatizo makubwa kwenye mnyororo wa thamani kwenye viwanda vya mazao ambayo hayana mashamba kama korosh, viwanda vya nguo, viwanda vya kukamua mafuta, alizeti, pamba na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni kweli nikiri kwamba tunahitaji uchambuzi wa kina ambao utafanywa na Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau wengine ili hatimaye tuweke mfumo wa uhakika wa kuhakikisha kwamba viwanda vyetu hivi, hasa ambavyo havina mashamba vinakuwa na uhakika wa kupata malighafi; na hiyo ndiyo itatupatia sustainability ya viwanda vyetu ambavyo vimekuwa vinaathiriwa sana.

Mheshimiwa Spika, ushindani wa bei kwenye soko umekuwa mkubwa kiasi ambacho viwanda vyetu vimekuwa vikipata shida kushindana bei na makampuni mengine ambayo yamekuwa yanatoa bei kubwa sana kwenye soko na matokeo yake viwanda vimekuwa vinakosa malighafi na hivyo kufa. Ukiangalia katika kipindi cha miaka mitano hadi 10 iliyopita viwanda vingi vya korosho vimekufa kwa sababu ya ushindani wa bei kwenye soko na hivyo kukosa maghafi.

Mheshimiwa Spika, kama nchi suala la kuendelea kuuza malighafi yetu kwenye nchi nyingine ni sawa na kuendeleza viwanda, ajira na faida kwenye nchi nyingine, kwa sababu bidhaa hizo a mbazo huzalishwa viwandani baadaye zitarudishwa tena kwenye nchi yetu na kuuzwa na kunuliwa na Mtanzania kwa bei ya juu zaidi. Endapo tutaendeleza mtindo huo hatutajikomboa kiuchumi. Watu wetu wataendelea kukosa ajira na hata faida za kiuchumi zitakuwa kidogo. Kwa hiyo Serikali inalichukulia suala hili kwa uzito mkubwa ili kuanzia mwaka ujao tuwe na mfumo mzuri utakaohakikisha viwanda vyetu vinapata malighafi ya kutosha kwa mwaka mzima na hivyo kulinda ajira na faida zaidi kwa Watanzania na wakati huo huo wakulima waendelee kupata bei nzuri.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la mapendekezo hapa. Wenzetu wamekuwa wanazungumzia mashtaka kwa wahujumu uchumi. Mimi niseme tu kwamba suala hilo ni suala la kisheria na sheria zina utaratibu wake ikiwemo kuwa na ushahidi wa kutosha kukamilisha taarifa za uendeshaji wa mashtaka. Sasa wakati tunamuachia Mwanasheria Mkuu wa Serikali mambo kama hayo tunatambua jambo moja la muhimu kwenye sekta ya korosho; kwamba kabla Mheshimiwa Rais hajachukua uamuzi wa Serikali kumkomboa mkulima kwa kumlipa shilingi 3,300 kwa kila kilo hakuna kampuni ya ununuzi hata moja ilikuwa imefikia offer ya bei hiyo ambayo Mheshimiwa Rais aliamua kuitoa kwa ajili ya kumkomboa mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ajabu ni kwamba mara baada ya Serikali kuanza kuwalipa wakulima shilingi 3,300 kila kilo baadhi ya makampuni yalijitokeza kusema kwamba sasa tupo tayari kulipa hiyo bei ya 3,300 au zaidi. Kwa hiyo hapo kama uchunguzi utaelekea kwenye mambo kama hayo mimi nadhani hapo tutaunga mkono wala hakutakuwa na shaka. Kwa hiyo kama tutachunguza kwa mwelekeo huo, si vibaya.

Mheshimiwa Spika, lakini si afya sana kuwekeza kwenye uchunguzi wa aina hiyo badala ya kuwekeza kwenye ufumbuzi wa kudumu wa matatizo yetu, hususan kuhakikisha viwanda vinapata malighafi na pia wakulima wanapata bei nzuri; kwa maana ya kuweka vizuri mfumo wa masoko ya mlighafi na mfumo wa masoko ya bidhaa za viwandani ili twende vizuri kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kuhusu Indo Power…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa, dakika zimeisha.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, dakika moja tu. Indo Power ni kampuni halali ambayo imesajiliwa kwenye orodha ya makampuni ya Kenya, na hii ilithibitishwa na Balozi wa Tanzania nchini Kenya na Balozi wa Kenya nchini Tanzania kwa barua rasmi ambazo zipo. Kwa hiyo kampuni hii inafanya kazi kihalali. Sasa kushindwa kuelewana na benki yake kwa ajili ya kutoa fedha za kununua korosho isitangazwe kwamba hiyo ni kampuni ya kitapeli. Ninataka kuthibitisha Bungeni hapa kwamba kampuni hiyo mpaka jana imeendelea kufanya biashara nchini Kenya, Afrika Mashariki na Dunia nzima. Kwa hiyo tumeachana na mkataba huo tunaendelea na kampuni nyingine, korosho zitauzwa na tutatangaza hapa Bungeni kabla Bunge halijaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Naunga mkono hoja.