Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Zainab Mndolwa Amir

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Kilimo pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku. Pia pongezi hizi pia ziwafikie watendaji wote wa Wizara.

Mheshimiwa Spika, maoni au ushauri wangu ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, fedha zinazopangwa na kupitishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya kilimo zitolewe kwa wakati ili kuweza kutekeleza miradi hiyo na kuleta tija katika kilimo.

Mheshimiwa Spika, pili, Serikali itafute masoko ya uhakika ya mazao yetu nje ya nchi ili kuweza kupata fedha za kigeni, pia wakulima kuweza kulima zaidi na kupata kipato cha kujikimu.

Mheshimiwa Spika, tatu, pindi wakulima wanapolima na kuvuna mazao yao na kuamua kuyauza Serikali wakati wa kuuza isiingilie kati kwa kuwapangia bei ya kuuza kwa sababu wakati wa kulima walitumia jitihada za wenyewe bila kupata msaada wowote wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, nne, Serikali kwa kutumia wataalam wetu wa kilimo itoe elimu ya kutosha kwa wakulima wetu jinsi ya kutumia mbegu bora, mbolea na madawa ya kuua wadudu ambao wanaathiri katika ukuaji wa mazao ili kuweza kulima kisasa zaidi na kupata mazao bora na yenye tija.

Mheshimiwa Spika, tano, Serikali ihamasishe wakulima kulima zao la mpira katika mikoa mingine kama ilivyofanya katika zao la korosho ili kuweza kupata malighafi ya kutosha katika Kiwanda cha General Tyre kilichopo Arusha maana kinategemea malighafi kutoka mikoa miwili tu Tanzania nzima; Tanga na Morogoro na hii wakati mwingine husababisha kiwanda kusimamisha uzalishaji kutokana na ukosefu wa malighafi.

Mheshimiwa Spika, sita, Serikali ihamasishe wananchi (wakulima) walime mazao ambayo yatatumika kama malighafi katika viwanda vyetu vya hapa nchini, hivyo kuweza kujihakikishia soko la uhakika.

Mheshimiwa Spika, saba, Serikali iwalipe kwa wakati wakulima ambao mazao yao yanauzwa katika vyama vya ushirika, pia mazao ambayo Serikali imeamua kuyanunua hususan zao la korosho kuwalipa fedha zao ili wakulima hao waweze kupata fedha za kuandaa mashamba yao pindi msimu wa kilimo ukifika, pia waweze kupata fedha zao na kuweza kuzitumia katika kuhudumia familia zao.

Mheshimiwa Spika, nane, Serikali iboreshe mnyororo wa thamani wa mazao yetu ili kuweza kuuza katika soko la dunia kwa kuwa ubora wake utakuwa umeongezeka.

Mheshimiwa Spika, tisa, Serikali katika maeneo ambayo wakulima wanatumia zaidi kilimo cha umwagiliaji, iwawezeshe wakulima hao kuwapatia vifaa mbalimbali ambavyo vitasaidia katika umwagiliaji wa mazao yao maana wakulima wengi hutumia njia za kienyeji, mfano, kuchimba mifereji katika kumwagilia mazao yao.

Mheshimiwa Spika, mwisho, nawaombea afya njema na umri mrefu katika kutekeleza majukumu yao Waziri na Naibu Mawaziri wake pamoja na watendaji wote wa Wizara.