Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Spika, Serikali imetangaza dhamira yake ya kuanzisha Bima ya Mazao ili kukabiliana na majanga. Ni wazo zuri na naliunga mkono japo litazamwe kwa makini isije kuwa ni gharama kwa mkulima na faida kwa makampuni ya bima. Hata hivyo, napenda kurudia wito wangu kuwa kuna haja ya kuwa na Skimu ya Hifadhi ya Jamii kwa Wakulima. Bima ya Mazao yaweza kuwa moja ya mafao yatakayotolewa na mfumo huo.

Mheshimiwa Spika, nasaha yangu kwa Serikali ni kuanzisha Skimu ya Hifadhi ya Jamii ya Wakulima ili kuwavutia kuweka akiba, kupata bima ya afya, Fao la Bei na mikopo nafuu ya pembejeo. Fao la Bei husaidia bei ya mazao ikianza kushuka. Kwa sasa bei za mazao zikishuka wakulima watarudi kwenye umaskini kwani hawana fidia ya bei kushuka (Fao la Bei). Kukiwa na price stabilisation mkulima anakuwa na hakika hata bei ikishuka chini ya kiwango cha gharama zake za uzalishaji Skimu ya Hifadhi ya Jamii itamfidia na hivyo kuendelea na shughuli zake msimu unaofuata.

Mheshimiwa Spika, mwezi Januari, 2018 niliandika Kuhusu Skimu hii kwenye zao la korosho, nanukuu:

“Mwaka huu peke yake iwapo wakulima 600,000 wa korosho wangekuwa kwenye hifadhi ya jamii, wangeweza kuweka akiba ya TZS 144 bilioni (14% ya Mapato yote ya korosho katika msimu mpaka sasa). Ingekuwa tumefanya hivi tangu 2015/2016 na 2016/2017, leo skimu ya Hifadhi ya Jamii ya Wakulima wa Korosho peke yake ingekuwa na thamani ya zaidi ya shilingi 300 bilioni. Hizi zingeweza kuwekezwa kwenye biashara ya pembejeo za kilimo, kuboresha mashamba, viwanda vya kuongeza thamani (processing factories). Pia ingetatua kabisa tatizo la afya kwa kuwapa wakulima wote Bima ya Afya bila kuathiri akiba zao.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, kupitia Skimu wakulima wanaweza kuingia kwenye mpango wa nyumba bora kwa kupewa mikopo ya muda mrefu ya nyumba na hivyo kufuta kabisa umaskini. Mkulima wa Tanzania anaathiriwa sana na mitaji ya pembejeo, uhakika wa bei za mazao yao na gharama za matibabu wanapoumwa wao na familia zao. Yote haya yanajibiwa na hifadhi ya jamii. Zaidi ya yote mkulima anakuwa na akiba ya uzeeni, pale ambapo hataweza tena kulima anakuwa analipwa pensheni ya kila mwezi. Haya ndio mapinduzi tunayoyataka kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nawasihi Wabunge kulitazama hili na kufanya kazi na Serikali ili kuleta mabadiliko makubwa kwa wananchi. Serikali ianze na wakulima wa baadhi ya mazao kama vile tumbaku, kahawa, pamba, karafuu, chai na mkonge. Baada ya kutekeleza na kujifunza kwa wakulima hawa tunaweza kupanua wigo kwenda kwa wakulima wote nchini.

Mheshimiwa Spika, skimu ya namna hii pia yaweza kutekelezwa kwa wafugaji na wavuvi pia. Mfano wakulima wa korosho wapatao 600,000 nchini wakiwa kwenye Hifadhi ya Jamii (kwa kutumia ushuru wa korosho - exports levy), tutaweza kufikia watu 3.6m wenye Bima ya Afya katika mikoa yote inayolima korosho ambao ni sawa na wananchi wote wa Lindi, Mtwara, Tunduru na baadhi ya Wilaya za Mkoa wa Pwani. Kupitia Skimu na mafao yake wakulima hawatakopwa mazao yao, pembejeo zitafika kwa wakati na wakati wa hali mbaya ya bei, watafidiwa gharama zao za uzalishaji.