Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nianze na kumpongeza Waziri Mheshimiwa Japhet Hasunga, Naibu Mawaziri Mheshimiwa Bashungwa na Mheshimiwa Mgumba pamoja na Makatibu Wakuu na Watendaji wote wa Wizara kwa kuwasilisha hotuba ya bajeti hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kupongeza Serikali kwa usajili wa wakulima; jambo hili ni jema sana. Ni imani yangu sasa zoezi hili la usajili wa wakulima nchini Serikali itaweza kutambua:-

(i) Ardhi itakayotumika katika kilimo

(ii) Mahitaji halisi ya wakulima kama mbolea, mbegu, madawa na viuatilifu, upangaji wa bajeti utarahisishwa.

Mheshimiwa Spika, lakini naitaka kujua, je, hili la usajili litachukua muda gani kukamilika na linafanyikaje? Je, uelewa wa wakulima katika kujisajili ukoje?

Mheshimiwa Spika, miradi ya umwagiliaji; hadi kufikia mwaka 2017, jumla ya skimu 2,942; skimu zilizoendelezwa zipo 960 tu na skimu ambazo bado hazijaendelezwa zipo 1,987 na katika Mkoa wetu wa Iringa una jumla ya skimu 58 za umwagiliaji. Hapo ni lazima tukiri Tume ya umwagiliaji haikufanya vizuri katika kipindi kilichopita. Hivyo, niipongeze Serikali kwa kuona umuhimu wa kuondoa baadhi ya watendaji katika Tume hiyo na kuunda Tume mpya. Ni vyema sasa Serikali ingefanya upembuzi yakinifu wa miradi ile iliyokaribia kumalizika au miradi yenye tija ili ipatiwe kipaumbele kupatiwa pesa kuliko kutoa pesa kidogo kidogo katika miradi mingi matokeo yake huwa inakuwa miradi haikamiliki mingi na pesa inapotea bila tija yoyote. Pia Benki ya Kilimo na Mfuko wa Pembejeo watoe asilimia 20 kusaidia miradi ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, Maafisa Ugani; asilimia 25 ya wakulima wadogo nchini ndiyo wanapata mbegu bora na asilimia 10 ya ardhi inayolimwa ndiyo inatumia mbolea, lakini uajiri wa Maafisa Ugani na mazingira ya kazi vimekuwa ni changamoto kubwa sana nchini. Mfano, kati ya mwaka 2014 - 2016, Maafisa Ugani waliopata mafunzo na kuhitimu walikuwa 3,189 lakini kati ya hawa, asilimia 20 tu ndiyo walipata ajira. Upungufu wa vituo vya kuwapatia maarifa wazalishaji wadogo na uwezo mdogo wa rasilimali (wataalam wa teknolojia). Je, nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha Maafisa Ugani wanaajiriwa?

Mheshimiwa Spika, Benki ya Kilimo; tunapongeza kwa kuzindua Benki ya Kilimo. Benki hii itakuwa ndiyo mkombozi kwa wakulima nchini na vizuri Serikali itoe ruzuku ya kutosha kwa Benki hii kwa sababu kushuka kwa mikopo sekta ya kilimo kulinganisha na sekta nyingine, hii inatokana na taasisi za fedha kuchukua kilimo kama sekta hatarishi (risk) na uanzishwaji wa Bima ya mazao utasaidia wakulima wetu kukopesheka kama kutakuwa na ukame, mafuriko, uvamizi wa viwavi jeshi na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, changamoto katika vituo vya utafiti; tulifanya ziara katika vituo vya utafiti hali ni mbaya sana. Bila Serikali kuona umuhimu wa kutenga pesa ya kutosha ili tafiti ziweze kufanyika hata sera yetu ya uchumi wa viwanda itakuwa kazi bure sababu viwanda vyetu vitakosa malighafi ya uzalishaji. Mfano, mbegu tu ya mahindi ni asilimia 65 kutoka nje, mboga mboga asilimia 99 kutoka nje. Serikali ingewekeza katika Taasisi ya ASA wakawekewa miundombinu ya umwagiliaji, matrekta na zana za kilimo, hiki kituo kingeweza kuzalisha mbegu za kutosha.

Mheshimiwa Spika, zao la pareto; hili ni zao la biashara katika Mkoa wetu wa Iringa. Pia kipo kiwanda katika Wilaya ya Mufindi. Kiwanda kina uhitaji wa maua ya pareto kiasi cha tani 5,000, lakini wakulima wana uwezo wa kuzalisha tani 2,500 tu. Tunawapongeza sana wamiliki wa Kiwanda cha Pareto kwa kuwapatia wakulima pembejeo na utaalam, lakini mbaya zaidi kuna walanguzi wanaokuja kuwarubuni wakulima maua yao. Je, Serikali inalinda vipi viwanda vyetu nchini dhidi ya hawa walanguzi? Hata tulipofanya ziara katika mashamba ya parachichi Mkoa wa Njombe kulikuwa na changamoto ya walanguzi toka nchi jirani kuwarubuni wakulima wetu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.