Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu na kumpongeza Waziri Hasunga na Manaibu wake Mheshimiwa Mgumba na Mheshimiwa Bashungwa kwa jitihada zenu za kubadilisha kilimo nchi Tanzania.

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kwenye Mkoa wangu wa Katavi. Mkoa wangu wa Katavi sisi asili yetu ni wakulima. Mkoa wa Katavi una Squire mita 47,586 ambapo asilimia 58.6 ni misitu pamoja na Mbuga za wanyama na asilimia 44 tunatumia kwa kilimo.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wangu huu wa katavi una mapungufu yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, pungufu la kwanza hatuna Maafisa Ugani. Mkoa unahitaji Maafisa Ugani 248; kwa sasa una Maafisa Ugani 164. Tuna upungufu wa Maafisa Ugani 16 Mleleji DC, 42 Mpanda DC, 34 Mpanda DC, 41 Nsimbo DC na 31 Mpimbwe DC; jumla tuna upungufu ya Maafisa Ugani 164. Ninaomba Wizara ya Kilimo mtuletee maafisa ugani.

Mheshimiwa Spika, mkoa wetu una changamoto za miundombinu; tukipata maafisa ugani wataweza kwenda vijijini; na mkoa wetu pia vijiji vyake havipo karibu; umbali wa kutoka kijiji kimoja kwenye kijiji kingine ni umbali kama wa kilometa 10 mpaka kilometa 20 ndipo unakuta kijiji kingine. Nikuombe Mheshimiwa Waziri utupatie Maafisa Ugani ili waweze kuusaidia mkoa wetu wa katavi.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ninalotaka kuomba pia; kwa sababu mkoa ni mpya naomba Wizara ya Kilimo muutupie jicho la huruma, muwapatie Maafisa Ugani hawa vitendea kazi ili waweze kusafiri; angalau pikipiki au hata baiskeli; ukilinganisha na umbali kati ya kijiji na kijiji.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni kwamba Mkoa wetu wa Katavi hauna Maafisa Kilimo, tunauhitaji wa Maafisa Kilimo kama 4, lakini Mkoa wa Katavi una Afisa Kilimo mmoja. Hii yote inasababisha afisa kilimo mmoja hawezi akazunguka mkoa mzima kwenda kuangalia shughuli za kilimo. Niombe Wizara iuangalie mkoa huu.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia; mwaka jana wakulima wa Mkoa wa Katavi walipata hasara sana ya mazao yao. Walipotaka kuyauza waliambiwa mahindi yao hayanya ubora. NFRA walipofika kule katavi waliangalia yale mahindi wakawaambia hayana ubora. Hii yote ilisababishwa na ukosefu wa Maafisa Ugani ambao hawakuwafundisha mahindi yenye ubora ni mahindi ya namna gani, kwa hiyo wakulima waliishia kula yale mahindi bila kuyauza.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la hawa Maafisa Ugani wa Mkoa wa katavi. Kuna mazao mapya yameenda kule Katavi, zao la pamba na korosho. Maafisa Ugani waliopo Mkoani wa Katavi hawana uzoefu na haya masuala. Ningeomba kupitia bodi za korosho na bodi za pamba haya maafisa ugani wapewe elimu ya pamba na korosho ili waweze kuwafundisha wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa manufaa ya zao hili na manufaa ya wananchi wa mkoa huo.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia mwaka jana Serikali ilitoa tozo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Taska malizia unga mkono hoja.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante naunga mkono hoja nilitaka kusema kwamba Serikali ilitoa tozo la asilimia tano kwenda asilimia tatu kwa mazao ya biashara na asilimia tatu kwenda asilimia mbili kwa mazao ya chakula, lakini wakulima hawajanufaika, nataka kuuliza swali, aliyenufaika hapa ni mfanya biashara au mkulima?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)