Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Kilimo. Kwanza nawapongeza Manaibu Waziri na Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa wanayofanya kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, leo suala langu ni gumu kidogo ingawaje kabla sijaanza watu wanaanza kucheka. Mimi nakuja na suala la bangi, nchi nne za Afrika sasa hivi zimeruhusu kilimo cha bangi kwa ajili ya matumizi ya dawa za binadamu. Ni vizuri wakati wowote wakati dunia inapopata nafasiā€¦

SPIKA: Hebu Waheshimiwa Wabunge tusikilizane, yanapoongelewa mambo ya maana na muhimu tunasikiliza, Katibu weka vizuri dakika zako hebu anza vizuri, Mheshimiwa Kishimba endelea.

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Spika, ni vizuri sana wakati dunia inapopata kitu kipya na sisi Watanzania kuwa wa kwanza kuwahi kama wenzetu wanavyowahi. Ninavyoongea gazeti la Mwananchi la tarehe 18 mwezi wa Tano Jumamosi, nchi ya Uganda imekwisharuhusu kulima bangi kwa ajili ya dawa za binadamu. Dawa nyingi za maumivu hasa za kansa Mheshimiwa Waziri wa Afya, Naibu Waziri wa Afya Mheshimiwa Ndugulile anafahamu vizuri kwamba nyingi kwa asilimia 80 zinatokana na bangi.

Mheshimiwa Spika, nashangaa kwa nini wataalam wetu wa TFDA wangekuwa wameshachukua sampuli muda mrefu wakati wanaziangalia kwenye maabara, wangetujulisha kwamba ndani ya hizi dawa kuna bangi na wangemuuliza supplier hii bangi unapata wapi. Maana yake sisi wenyewe tunayo bangi na ukiangalia vizuri bangi tunayoona kila siku inakamatwa kukatwa ukweli bangi hiyo siyo kwa ajili ya kuvuta, bangi hiyo imekuwa ikienda kwenye dawa za binadamu. Ushahidi ninao Lesotho na Zimbabwe wameruhusu na mimi nimefika kwenye kiwanda cha Zimbabwe ambacho kinatengeneza dawa za binadamu kwa kutumia material ya bangi.

Mheshimiwa Spika, gunia moja la bangi leo Tanzania ni shilingi milioni nne mpaka milioni nne laki tano, lakini Lesotho na Zimbabwe ni dola elfu saba, karibu milioni ishirini na bangi yote hii ya Tanzania yote inakwenda kwenye madawa ya binadamu ambayo sisi tunaletewa kuja kutumia kwenye hospitali zetu. Sasa kuna ubaya gani Serikali ikaanza kutoa permit au vibali watu kwenye maeneo mbalimbali na kuhalalisha watu waanze kulima bangi hiyo ili tuweze kupata faida na kuondoa mgogoro mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siwezi kuungana na Mheshimiwa Musukuma kwenye suala la kuvuta, suala la kuvuta sheria iendelee palepale kwamba watu hawaruhusiwi ,lakini kwa kuwa sasa ni halali kwa ajili ya madawa ya matumizi ya dawa za binadamu, tuna sababu gani ya msingi sisi kutowahi hilo soko? Hata kama tutakataa leo, baada ya miaka minne wakati bei itakuwa imeanguka hata tukiruhusu haitatusaidia. Ni vizuri Waziri wa Kilimo awasiliane na Waziri wa Afya waone namna gani watafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa namna ilivyo bangi ni zao ambalo kwanza haliliwi na wadudu, hakuna wadudu wanaokula bangi na eka moja ya bangi unapata gunia sita. Kama ni gunia sita kwa bei ya milioni 20, ni milioni 120 lakini leo wananchi wetu wanauza milioni nne na ndiyo zao peke yake Tanzania kwa leo ambalo mkulima akiwa amepewa advance, Mheshimiwa Heche naona ametoka. Kwa hiyo badala ya kuendelea na mgogoro huu tunaomba Wizara ya Kilimo wafikirie contract farming ya bangi ambayo sasa inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi ya Canada imeruhusu, yenyewe imeruhusu kuvuta, lakini Canada ni miongoni mwa nchi saba tajiri na Mheshimiwa Waziri wa Fedha nafikiri anatarajia kuomba pesa huko akipewa pesa za bangi atakataa na atazijuaje kwamba hizi ni za bangi. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nafikiri ni vizuri sana, tumeona tumepoteza vitu vingi sana kwa ajili ya kuchelewa. Tulikuwa hapa meno yetu ya tembo yanakwenda Burundi kwa miaka 30, mpaka mwishowe biashara ya meno ya tembo imekwisha. Tumeshuhudia dhahabu zetu zikienda tunachelewa sana sana kufikiri, juzi hapa kwenye Uwanja wa Ndege wa Entebbe tarehe 11 Machi zimekamatwa tani saba za dhahabu. Ukiangalia tani saba za dhahabu Uganda haina dhahabu, dhahabu hizo zimetoka Tanzania, lakini namna hii hii tunachelewa baadaye dunia inabadilika si tunaendelea kulima matikiti maji. Tunaomba na uzuri kama Waziri wa Kilimo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali yuko hapa kama watapitisha hili na Wabunge nafikiri watakuwa watu wa kwanza kabisa kujisajili na hali yetu kama unavyoijua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)