Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Eng. Joel Makanyaga Mwaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chilonwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. JOEL M. MWAKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hoja ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya, niipongeze Wizara kwa maana ya Waziri, Naibu Waziri pamoja na timu nzima ya Wizara kwa bajeti yao nzuri waliyotuletea safari hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naomba kwa sababu ya muda, niende tu moja kwa moja kwenye jambo mahsusi ambalo ningependa kuongea leo. Kilimo kwa Kanda ya Kati, sehemu kubwa tutegemee kilimo cha kumwagilia. Suala la mvua hapa Dodoma ni tatizo kubwa sana, Dodoma ina register mvua nyingi sana lakini zinazokuja bila mpangilio unaoweza kuwezesha mazao kukua na kutoa mazao yanayotegemewa. Kwa hiyo njia peke yake ni kulala kwenye kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikizungumza suala la kilimo cha umwagiliaji, maana yake tunahitaji mabwawa. Tunayo mabwawa ya zamani ambayo yapo tayari lakini bado kuna mipango ya kuweka mabwawa mapya; hivi ndiyo vitu vya Serikali kuweza kuvishughulikia kwa ukaribu kabisa katika eneo letu hili la kati.

Mheshimiwa Spika, mabwawa ya zamani, nimebahatika mara mbili hivi kwenda na Mawaziri kwenye maeneo ya mabwawa kwenye Jimbo langu la Chilonwa. Nimekwenda kwenye Bwawa la Bwigiri, Bwawa la Ikoa na Waziri, wakati Maji na Umwagiliaji, Mheshimiwa Kamwele, lakini na juzi nimekwenda na Naibu Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Omary Mgumba. Hoja ya wananchi kwamba mabwawa yanafukulika ilichukuliwa na Serikali na kusema kwamba wanayafanyia kazi hatuoni mrejesho wowote juu ya mabwawa haya.

Mheshimiwa Spika, ninaiomba Serikali, iwasaidie wananchi wa eneo hili ili waondokane na tatizo hili wanalolizungumza Waheshimiwa Wabunge wengine waliopita, la kila wakati kulia njaa ilhali Dodoma ina ardhi nzuri inayokubali mazao yote, Dodoma unalima kila aina ya zao.

Mheshimiwa Spika, nimeshangaa, sasa hivi Jimboni kwangu wanavuna pamba, sikuamini wakati tunaambiwa tupande pamba lakini sasa hivi wanavuna pamba, maeneo ya Segala kule, nimekwenda nimeshangaa na macho yangu. Kwa hiyo kila zao linakubali ila shida ni maji. kwa hiyo, tunaomba sana masuala ya mabwawa haya, hebu yapate mrejesho unaoeleweka ili wananchi wawe na uhakika wa kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, niende pia kwenye suala la mafunzo kwa wakulima hawa. Wakulima wanahitaji kupewa mafunzo ya nini cha kufanya kwenye maeneo yao mbalimbali. Si kila ardhi inakubali kila zao, basi wapewe elimu ya eneo hili hapa wajue afya ya udongo wa eneo walilopo inakubali mazao gani ili waweze kupanda hayo mazao. Vilevile, hata ikibidi watumie mbolea basi watumie mbolea gani katika udongo ule badala ya kutumia kila mbolea kwa kila zao kila sehemu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda basi nichukue nafasi hii kwa heshima na taadhima niunge mkono hoja kwa asilimia 100, ahsante sana. (Makofi)