Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru sana na mimi kwa kunipa nafasi nichangie mada iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nianze kwa kuipongeza sana Serikali kwa hatua zinazofanyika katika kuboresha sekta ya kilimo. Zimekuwepo kero nyingi kwa miaka ya nyuma lakini hivi sasa unaona kabisa kwamba hatua zinazochukuliwa zinatatua kero hizo. Kama tunakumbuka kwa wale ambao tumekuwa kwenye Bunge hili muda mrefu, shughuli kwa mfano ya bei na usambazaji wa pembejeo za kilimo limekuwa ni tatizo la muda mrefu, lakini utasikia kwa sasa na hata miaka ya baadaye, hatua ambazo zimechukuliwa za ununuzi kwa mfano wa mbolea kwa pamoja unafanya vizuri; na hii ni hatua nzuri sana ambayo kwa kweli naipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipongeze vilevile Serikali kwa zao la pamba; uzalishaji unaongezeka sana, tunategemea mwaka huu kuvunja rekodi ya zaidi ya miaka mitano nyuma. Hizi ni jiihada za Serikali yetu. Mimi nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Waziri na Naibu Mawaziri wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kazi hii kubwa inayofanyika wote tunaamini kwamba inatakiwa ilenge katika kuweka uhakika wa chakula katika nchi kwa ujumla wake, pia inatakiwa kuwa ni chachu katika dhana nzima ya Tanzania ya viwanda. Mimi mchango wangu upo kwenye haya maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, food security kwa Tanzania bado kwenye baadhi ya maeneo tunapata changamoto. Kwa huu mwaka wa kilimo ambao tunaenda nao, kuna baadhi ya maeneo ambayo hayajapata chakula vizuri kwa sababu ya mabadiliko ya tabia nchi na hali ya hewa kusababisha mvua kutokunyesha vizuri; lakini kuna maeneo ambayo yamepata chakula. Nini solution ya suala hili? Kwa ujumla tumekuwa tukishauri kwamba ni vizuri tukajikita kwenye scheme za umwagiliaji ili kutunza maji yanayopatikana kwa muda mrefu. Suala hili kwa Mkoa wetu wa Shinyanga tumekuwa tukilizaungumza kwa muda, tukiamini kwamba si vizuri Mkoa kila wakati tukisema kwamba tuna matatizo ya njaa basi tunaomba chakula cha msaada. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2013, tulipendekeza katika RCC kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu na Halmashauri ya Shinyanga Vijijini kwa maana ya Jimbo la Solwa na Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, maeneo yake zaidi ya asilimia 80 yanafaa kwa kilimo cha mpunga. Kwa hiyo mkoa ubuni mpango wa kufanya kilimo cha umwagiliaji kwenye maeneo hayo. Zimekuwepo jitihada katika mkoa lakini inaonekana kama vile kuna mawasiliano hafifu baina ya Serikali Kuu, kwa maana ya Wizara na Mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri ya Msalala kwa mfano miaka miwili iliyopita tulipendekeza scheme zaidi ya sita. Tulipendekeza kuwepo scheme kwenye Bonde la Kashishi, kuna eneo linaitwa Kashishi kule, ni kubwa tu ambalo likifanyiwa kilimo cha umwagiliaji tunaweza kupata mazao vizuri. Kuna Bonde la Kabondo, Bonde la Buva, Bonde la Chela kuna scheme ilianza mwaka 2008, haikufanya vizuri; na kuna Bonde la Mwalugulu. Kwa bahati mbaya maeneo yote haya ambayo yanafaa kwa kilimo cha umwagiliaji jitihada ambazo zimekuwa zikifanyika kwenye ngazi za halmashauri, hazioneshi kuungwa mkono na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuombe sana rafiki yangu, mhasibu mwenzangu, Mheshimiwa Waziri hebu fika Msalala uyaone haya maeneo, uone jitihada ambazo tunafanya katika halmashauri ili uone namna ya kusukuma jitihada hizi ili tuwe na uhakika wa chakula. Tunaamini kabisa jitihada hizi za Wilaya na Mkoa zikiungwa mkono, tutakuwa na uhakika wa chakula. Tunataka maeneo haya ndiyo yawe ghala la mpunga kwa mkoa mzima na tuweze kuzalisha na kuuza nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, vilevile kama nilivyosema, kwa upande wa kuunganisha na biashara, kwenye zao la pamba viwanda vinavyoendana na zao hilo bado havijasukumwa sana. Nilitaka kuiomba Serikali kwa maana ya Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Viwanda hebu jaribuni kukaa pamoja ili kuangalia namna ya kuboresha zao la pamba kutoka zao…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Malizia Mheshimiwa

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: …hadi linapoweza kutengeneza nguo pamoja na mafuta.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, jitihada zinazofanyika na Serikali ni kubwa na zinaonekana, naiunga mkono bajeti hii. Nimuombe sana tu Mheshimiwa Waziri aje aone jitihada zetu na tuunge mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi, ahsante sana. (Makofi)