Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema, lakini nashukuru pia kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye hizi taarifa zote za hizi Wizara. Nianze kuwapongeza sana Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati za Wizara zote, Wizara ya TAMISEMI, Katiba na Sheria lakini pia na Sheria Ndogo kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya na wakaleta taarifa nzuri ambayo wametusomea hapa wametuletea hapa, nawapongeza sana. Pongezi kwa namna ya pekee Mawaziri wa Wizara hizi zote mbili, hasa nikianza na Waziri wa TAMISEMI na Manaibu Waziri wote wawili na watendaji wake wote, lakini pia na Watendaji wa Wizara nyingine na Mawaziri wa Wizara hizi zote nyingine ambazo taarifa zao zimewasilishwa hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia kwenye upande wa TARURA, Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini. Kama ilivyoelezwa kwenye taarifa imeoneshwa vizuri sana kwamba TARURA wanashughulikia barabara zenye urefu wa kilometa 108,946. Hizi ni barabara nyingi sana, na hizi barabara ni zile ambazo zimesajiliwa lakini bado kuna barabara nyingi ambazo hazijasajiliwa, nazo pia kwa namna moja au nyingine pengine wanashughulikia nazo, lakini ukiangalia kwenye bajeti yetu bado TARURA wanapewa fedha kidogo sana kama walivyoeleza wenzangu. Sasahivi wanapewa kwenye bajeti asilimia 30 na asilimia 70 inaenda kwa TANROAD, mimi, kama walivyosema wenzangu, nilikuwa napenda nipendekeze kwamba angalau wangeweza kuongezewa ikafika asilimia 45 hivi ili barabara nyingi hizi zinazoenda huku Vijijini ambako ndiko asilimia 80 ya wananchi wanashughulika na kilimo, ili waweze kusafirisha mazao yao vizuri ni lazima barabara za huko ziwe nzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kupitia barabara hizo barabara tutaweza kukuza uchumi wetu; na ukiangalia mapato mengi halmashauri nyingi hasa za Vijijini zinategemea sana hizi barabara. Waheshimiwa Wabunge wamesema hapa kwamba kuna baadhi ya halmashauri hazilipi Madiwani, ni kwa sababu tu hawapati mapato ya kutosha na inawezekana kinachochangiwa wasipate mapato ya kutosha ni kutokana na kwamba barabara ikifika misimu ya mvua kama hii sasahivi mizigo haiwezi kusafiri. Kwa hiyo maana yake mapato yale ambayo wanatakiwa kukusanya kupitia hizi barabara hawawezi kuyapata; kwa hiyo na hatimaye shughuli nyingi za maendeleo, lakini shughuli nyingi pia za halmashauri zinakwama kwa sababu barabara hizi hazipitiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua mfano kwangu mimi kwenye Jimbo langu mimi kwenye Jimbo langu Jimbo la Lupembe asilimia 80 ya mapato linategemea hizi barabara za vijijini, na miezi kama hii ambapo mvua zinanyesha nyingi barabara hizi zote hazipitiki. Kwa hiyo niombe sana Mheshimiwa Waziri mkikaa kwenye Baraza lenu mpitishe hili kwamba angalau TARUARA wapewe hela za kutosha. Wakipata asilimia zaidi ya 40 hivi itakuwa nzuri na barabara nyingi zitaweza kuboreshwa na hatimaye uchumi wa halmashauri utakuwa na mapato yataongezeka na hatima yake miradi mingi ya maendeleo itatekelezwa kwa sababu vyanzo vya mapato vinaweza kupatikana kirahisi, pia mizigo inaweza kusafiri kirahisi kutoka vijijini kwenda mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichangie kuhusu mpango wa kurasimisha, biashara na rasilimali mbalimbali ikiwemo ardhi, nyumba na biashara. Mimi niongelee kidogo juu ya upande wa ardhi na makazi. Tunaushukuru sana, Serikali kwa kuanzisha mpango huu, na unaendelea vizuri na tunaona ardhi zinarasimishwa zinakuwa na thamani. Ilivyokuwa kabla ya mpango huu ardhi nyingi maeneo mengi ilikuwa haina thamani kwa sababu zilikuwa hazijarasimishwa; lakini pia na makazi tunajua watu wengi wamejenga kwenye viwanja ambavyo hazijapimwa, lakini Serikali imeendelea kurasimisha kupitia MKURABITA ili ardhi hizi au nyumba hizo ziweze kutambulika na hatimaye ziweze kupata hati. Lakini tuna changamoto kubwa sana changamoto ya Maafisa Ardhi, pia na Maafisa Mipango Miji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya halmashauri hususan halmashauri za vijijini nyingi hazina wataalam wa ardhi, hazina Maafisa Ardhi Wateule na Maafisa Mipango Miji. Halmashauri ya kwangu, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe nayo ni miongoni mwa halmashauri ambayo muda mrefu haina Afisa Ardhi Mteule na pia haina mtaalam wa mipango miji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunashindwa hata kupanga mipango ya ardhi, tunashindwa hata kupima na kutoa hati imekuwa ni vigumu kwa sababu hatuna wataalam. Kwa hiyo tuombe sana, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo tusaidie tuweze kupata Afisa Mteule pamoja na mtaalam wa mipango miji ili nasi tuweze kupata wataalam ambao watatusaidia kutoa hati pamoja na kurasimisha ardhi na makazi. Vilevile tuweze kupanga miji ili tuweze kupata vyanzo vingine vya mapato na wakati huo huo miji yetu iweze kukaa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu kukamilisha maboma. Tunashukuru sana Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma kama vile majengo ya afya na majengo ya elimu. Kwenye halmashauri yetu sisi bahati mbaya hatukupata pesa ya upande wa afya, kwa maana ya vituo vya afya, lakini niishukuru sana Wizara ya TAMISEMI mmetupatia milioni 200 kwa ajili kujenga kituo cha afya kimoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kupitia Wizara yako Mheshimiwa Waziri mtusaidie tuweze kuongezewa fedha, tukipata angalau milioni 400 tuweze kukamilisha hicho kituo cha afya, na ikiwezekana mtupatie tupate vituo viwili kama zilivyo halmashauri lingine ambazo zimepata sisi tulikosa tumepata mwishoni hizo milioni 200; basi mtuongezee tuweze kukamilisha ujenzi wa vituo vyetu vya afya na maboma mengine ambayo yapo kwenye Halmashauri yetu ya Wilaya ya Njombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwahiyo naamini kwamba tukifanya hivyo tutakuwa tumeboresha sana na watu wengi watapata hii huduma ya afya kirahisi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna changamoto kubwa pia katika uboreshaji wa hivi vituo vya afya na kwenye upande wa elimu. Sasahivi tuna changamoto kubwa ya wataalam, wahudumu wa afya na walimu, hasa walimu wa shule za msingi kwenye elimu. Niombe sana Wizara iajiri walimu wa kutosha ili tuweze kuhakikisha kwamba shule zetu zinapelekewa walimu wa shule za msingi. Kuna baadhi ya shule zina walimu watatu na nyingine zina walimu wanne; kwa hiyo hili ni tatizo kubwa. Hatuwezi kutegemea kuwe na ubora wa elimu kama walimu wanaofundisha ni wanne. Kuna shule ambayo nilisoma mimi Mheshimiwa Waziri inaitwa Shule ya Msingi Kanikelele ina walimu sita tu na wanafunzi wako mia saba na kitu leo hii.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana, tukiongeza ajira za walimu tutasaidia halmashauri nyingi ziweze kupata walimu na hatimaye watoto wetu waweze kupata elimu bora. Kwa hiyo ilivyo sasahivi watoto wengi wanashindwa kupata elimu bora kwa sababu walimu mashuleni hawapo. Kwa hiyo niombe sana katika mpango wetu katika bajeti hii tujikite kabisa kuajiri walimu, lakini pia tujikite kuajiri wataalam wa afya ili vituo vyetu vya afya ambavyo tumevianzisha viweze kupata watalam, pia na shule zetu hizi ziweze kupata walimu ili watoto wetu waweze kusoma vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nililotaka nichangie kidogo juu ya mikopo ya walemavu; wenzangu wameeleza pia; lakini niseme kwamba kwenye upande wa hasa ile asilimia mbili; niombe, kuna wale walemavu ambao wao wenyewe hawana, mmoja amesema hapa kuhusu wale wenye utindio wa ubongo au wengine wana ulemavu ambao hauwawezeshi hata kufanya shughuli yoyote; tuwapatie basi wazazi wao ili waweze kuingizwa kwenye kikundi ili nao wahesabike na ili waweze kupata hii mikopo. Hii ni kwa sababu ilivyo sasahivi inataka mlemavu mwenyewe aweze kuwepo kwenye kundi. hii itawatenga baadhi ya walemavu watashindwa kupata mikopo kwa sababu hawatakuwa na uwezo wa kuingia kwenye kundi. Sasa tukitumia wazazi ama walezi wao wataweza kunufaika na hiyo mikopo ambayo inatolewa na halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru sana kwa nafasi na naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.