Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo

Hon. Godbless Jonathan Lema

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza niulize swali moja, hivi nyie Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lema unamuuliza nani?

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakuuliza wewe…

MWENYEKITI: Mwenyekiti haulizwi swali, Mwenyekiti anasikiliza michango…

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachangia.

MWENYEKITI: Haya changia.

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasema hivi sisi ni Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunapoishauri Serikali hatuishauri kwa sababu tuna chuki, tunaishauri kwa sababu hii ni nchi yetu. Sasa mara nyingi unaona unapoishauri Serikali kwenye mambo critical watu wanasimama kuomba miongozo na utaratibu, hatupo hapa ku-shine, tupo hapa kulisaidia Taifa. Ninyi mna-shine, ninyi ndio mna Serikali, ni Mawaziri tusikilizeni sisi tuwaambie muende mkafanyie kazi haya mambo. Hii nchi ikiharibika, inaharibika yote kama ambavyo mafuriko yakija hayachagui CHADEMA, CCM wala CUF. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, neno utawala bora linachukuliwa kirahisi sana, leo Taifa hili imefika mahali mtu hajatiwa hatiani na mahakama, anpata msamaha kama mtuhumiwa, yaani mimi napelekwa mahakamani leo, ninawekwa jela miaka mitano, ninaitwa nimetakatisha fedha halafu baadaye unatangazwa msamaha kwamba anayetaka kuomba msamaha aje; sijatiwa hatiani na mahakama kuitwa mwizi nasamehewa kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unamkamata mtu mwaka wa kwanza, wa pili, wa tatu, wanne; mimi mwenyewe ukiniweka ndani kama familia yangu haipo stable, mke wangu na wazazi wangu watasema omba msamaha, kubali makosa uza nyumba ukae nje kuna maisha mengine zaidi ya haya. Kuna watu wanaomba msamaha leo si kwa sababu ya hatia, ni kwa sababu familia zao zimechoka kuona watu wakiwa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu utawala bora tunaouongelea sio wa kwetu, kimsingi waliopo jela wengi ni wakwenu tukiongelea kwa mambo ya itikadi. Utawala bora tunaouongelea leo ni kulinda maslahi ya kila mtu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uchaguzi mwaka huu, pengine asilimia ndogo sana ya Wabunge watarudi. Kwa namna kesi ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi zinavyoendeshwa sasa, kila mtu hapa ana-qualify kuwa mtuhumiwa na kwenda jela. Mimi nimekwenda magereza kuna watu wana M-Pesa 900,000 wamepewa utakatishaji fedha wapo magereza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utawala bora sio kujenga barabara na kununua ndege, utawala bora ni kutengeneza misingi ya haki ambayo inadumisha utu katika Taifa hili. Mimi leo ukinipa barabara kilometa milioni moja Jimboni kwangu lakini ukamchukua mtu mnyonge maskini ukamuweka jela, huyu mnyonge kutoka jela ina maana kwangu kuliko barabara; utu ni wa msingi kuliko vitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyosema utawala bora wa haki, tunataka Bunge liwe huru, mahakama ziwe huru na Serikali iwe huru. Tunapopingana na Serikali hatupingani kwa sababu tunamchukia Rais. Na hakuna mtu anasema kila kitu anachofanya Rais ni kibaya lakini nyie sio malaika na ndio maana mnapata usingizi na mnakufa, kwa vile sio malaika mkubali mshauriwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo hali ni mbaya, tunakwenda kwenye uchanguzi Mkuu mwaka 2020. Tumeona matamko huko nje ya UVCCM, matamko yanayotamkwa vijana wa UVCCM nikitamka mimi asubuhi saa 4, saa 6 nipo magereza na bila dhamana. Badala ya Serikali kuchukulia hatua matamko makali kama haya, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi anasema ninawaonya vijana wa UVCCM. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilihudhuria kesi za mauaji ya Rwanda Arusha, watu wote waliotiwa hatiani ni kwa sababu ya matamko. Tulinde Taifa hili kwa upendo, tulinde Taifa hili kwa kuonana sisi ni watu wema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukikaa kantini Wabunge wanakaa kwa caucus, wanaogopa hata kukaa na sisi wakati wa Jakaya mnafumuana humu ndani, mkitoka nje jioni mnakwenda mnakunywa chai na juice; hiyo ndio ilikuwa siasa, leo siasa imeshindikana. Polisi ndio wanasaidia kuumiza watu; yakija maswali hapa mnakata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitagombania Ubunge mwaka 2020 kesho kutwa, sigombanii kwa sababu nitashinda ama nitashindwa, nagombania kuweka alama ya kwamba wakati demokrasia inapita kwenye majaribu, sikuogopa nilisimama imara nikapigana hii vita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi wote mnaweza mkarudi kwa sababu uchaguzi wenu hauamuliwi na kura, unaamuliwa na bunduki lakini nawaambia mnachojenga katika Taifa hili ni kitu kibaya sana kwa vizazi vinavyokuja. Ni bora Mungu awape hekima leo muone mnachokifanya. Utawala bora leo Mawaziri hawana confidence na ndio maana hakuna innovation. [Maneno Hayo Hapo Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi ya Bunge]

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuwepo na uwezo…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lema confidence ya Mawaziri subiri sasa, haya Mheshimiwa Jenista.

KUHUSU UTARATIBU

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo kwenye utaratibu na hilo la confidence ya Mawaziri wala sina shaka, nchi inatuona tuna confidence na tunafanya kazi ya kutosha. Kwa hiyo, hayo ni mawazo ya Mheshimiwa Lema. Mimi nakwenda kwenye suala la kiutaratibu, la confidence wala sitazungumza kwa sababu taifa linatuona confidence yetu na Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba suala la utaratibu, Mheshimiwa Lema amesema hapa na jambo hili hatuwezi kuliacha kwamba ushindi ambao umekuwa ukipatikana kwenye chaguzi ndani ya nchi hizi umeamuliwa na mtutu wa bunduki. Jambo hili kwa mujibu wa taratibu, Kanuni ya 61(1)(a) jambo ambalo Mbunge hana uhakika nalo na si la ukweli hatakiwi kulisema Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua chaguzi zote zinaendeshwa kwa misingi ya sheria na Katiba.

WABUNGE FULANI: Aaaaaa!

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri kwa sababu Kanuni ya 63 inanitaka mimi ni-prove hiki ninachokizungumza, kifungu cha 44 cha Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kimesema kama kuna mtu ameona uchaguzi katika eneo lake haukuwa haki na
halali, ana uwezo wa kwenda ndani ya siku 30…

WABUNGE FULANI: Aaaaaa!

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Nisikilizeni basi…

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa, endelea. Waheshimiwa tutulizane basi amalize. Mheshimiwa Jenista naomba uendelee.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 44 cha Kanuni za Uchaguzi kwa mfano kwenye Serikali za Mitaa tulizomaliza juzi kimeeleza wazi ndani ya siku 30 kama mtu ana ushahidi uchaguzi haukuwa halali aende akashitaki…

WABUNGE FULANI: Na weweee!

WABUNGE FULANI: Huyoooo!

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujapata hiyo kesi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Jenista. Naomba tutulizane basi, Waheshimiwa Wabunge tusikilizane. Utaratibu ni hivi ndio ukweli wenyewe; Tanzania kama nchi haijawahi kupata ushindi wa aina yoyote kwa mtutu wa bunduki.

WABUNGE FULANI: Eeeeee!

MWENYEKITI: Sio hivyo sasa mnakwenda mbali hebu subirini. Tanzania kama nchi haikuwahi kupata sifa hiyo, kama kuna maeneo yametokea hayakufanywa kwa usahihi, sheria zipo hilo ndio lililozungumzwa. Mheshimiwa Lema tumalize hapo, kama umekusudia nchi nzima kwa maana ya Tanzania naomba ufute hiyo kauli.

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushauri. Mheshimiwa Jenista kwa jinsi unavyopenda Uwaziri siku ukitumbuliwa unaweza ukafa baada siku mbili kwa sababu huwezi ku-defend kila jambo eti kwa sababu uonekane, kuna saa ku-chill ni wisdom, una-chill tu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe unajua haya mambo tunaongea unafahamu na ni hivi, hatufanyi ili kuwa Mbunge; nimeshakuwa Mbunge awamu mbili, hatufanyi mimi kuwa Mbunge. Tunaposema utawala bora katika Tume huru ya Uchaguzi, naomba niongezee muda tafadhali sana…

MWENYEKITI: Malizia.

MHE. GODBLESS J. LEMA:Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema utawala bora ulenge katika Tume huru ya Uchaguzi sio tume ya kuisaidia CHADEMA, tume ya ku-harmonize future ya Taifa hili. Kwamba kusiwepo na mashaka, ni hatari sana watu kufikiria eti huwa mnaiba kura. Hilo tu lenyewe ni hatari yaani tu kufikiria kwamba huwa mnaiba kura ni hatari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa cha muhimu ni nini, ili kuwa na future nzuri, wananchi wanatakiwa wawe na imani na uchaguzi, wananchi wakiondoa imani na uchaguzi, watatafuta alternative. Haya mambo yanahusu wajukuu na watoto zenu, wewe utakuwa mzee ama utakuwa umetumbuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba hili suala lizingatiwe, sasa tukisema tuanze kuleta ushahidi hapa Pompeo mwenyewe amesema…

MBUNGE FULANI: Taarifa

MHE. GODBLESS J. LEMA: Pompeo amesema kwani hamuona Wamarekani wamesema nyie…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

WABUNGE FULANI: Aaaaa!

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jenista.

MWONGOZO WA SPIKA

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mwongozo.

Nimwabie tu Mheshimiwa Lema kwamba humu ndani sisi Mawaziri tunapofanya kazi tunaendelea kulinda heshima na hadhi ya Serikali. Haya maneno ya kutumbuliwa ama kutokutumbuliwa hayatukatishi tamaa, sisi tunaendelea kupambana. Kwa hiyo, kwetu hiyo sio hoja na Mheshimiwa Lema wala asifikiri atanitoa kwenye hoja kwa kunitishia kutumbuliwa, huo utashi utani… (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye mwongozo bado ninaendelea kusisitiza kwamba Ibara ya 74(7) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinaitamka Tume ya Uchaguzi kwamba ni idara huru. Ibara ya 11 na ya 12 inaeleza mipaka ya Tume ya Uchaguzi kutokuingiliwa na chama wala taasisi yoyote.

WABUNGE FULANI: Aaaaaa!

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeomba hapa suala la kiutaratibu kwamba hatuwezi kama Ibara tu ya Katiba inaonesha uhuru wa vyombo tulivyonavyo, hawezi Mbunge humu akaendelea kusimama akadai kwamba uchaguzi tunaoshinda kwenye nchi yetu unatumia mtutu wa bunduki, haiwezekani. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Hivyo hivyo!

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalize kwamba ni lazima jambo hilo liondolewe kwenye hansard vinginevyo hatuwezi kumaliza kikao hiki kwamba nchi hii inashinda kwa kutumia…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mwongozo.

MHE. JOHN W. HECHE: Taarifa.

MWENYEKITI: Waheshimiwa ngoja nimalize moja halafu tutaendelea na lingine…

MHE. JOHN W. HECHE: Taarifa kwa Jenista

MWENYEKITI: Aah! Hakuna taarifa kwa Jenista, hakuna taarifa kwa Mheshimiwa Jenista. Mheshimiwa Heche naomba ukae chini…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge hebu tutulizane, Waheshimiwa Wabunge naomba tutulizane. Mnapoteza muda wa kuchangia mambo muhimu, kote nasema naomba mtulizane. Ikiwa kama tunahisi kwamba Katiba inasema ipo sahihi na Katiba lazima wote tunaiamini na ndio tunaapa kwa Katiba hapa. Ikiwa Katiba inasema kwamba tume ni huru na imepewa mamlaka kamili kama kuna Katiba imevunjwa pahala tunajua taratibu zipo wapi, kama hamkwenda mtulie mnyamze mnasema kitu ambacho sicho.

Mheshimiwa Lema nilikwambia pale mwanzo kwamba nchi hii haikuwahi kupata ushindi kwa mtutu wa bunduki kwa maana ya Tanzania. Kwa hiyo, ili umalizie vizuri mchango wako naomba hiyo kauli uifute na kama hujaifuta nitaiondosha kwenye hansard.

MHE. ESTER A. BULAYA:Mheshimiwa Mwenyekiti, mwongozo.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Chief Whip naomba utulivu, kwa hilo naomba utulie amalizie kuchangia Mheshimiwa Lema.

MBUNGE FULANI: Taarifa.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mwongozo wa Mwenyekiti.

MWENYEKITI: Lema amalize kuchangia…

MHE. ESTER A. BULAYA: Ni haki kama aliyokuwa nayo Jenista Mhagama upande wa Serikali, nijibu mwongozo wa Mwenyekiti.

MWENYEKITI: Naomba amalize Mheshimiwa Lema halafu utazungumza.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mwongozo wa Mwenyekiti

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mwongozo wa Mwenyekiti, nina haki kama aliyokuwa nayo Mheshimiwa Jenista Muhagama upande wa Serikali Chief Whip. Mwongozo wa Serikali.

MBUNGE FULANI: Ndiyo

MWENYEKITI: Naomba amalize Mheshimiwa Lema nitakupa ruhusa, muache Mheshimiwa Lema amalize.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Nakupa nusu dakika umalizie Mheshimiwa Lema.

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nusu dakika ni wewe bora uiondoe kwenye hansad ila mimi siwezi kufuta ukweli. Ni sawasawa na kuanza kujisachi kama mimi ni mwanamke ama ni mwanaume. (Makofi/Kicheko)

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Taarifa.

MHE. GODBLESS J. LEMA: uchaguzi sio huru kwa hiyo kama unaiondoa kwenye hansard hakuna shida lakini mimi siwezi kufuta.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Taarifa.

MWENYEKITI: Hapana, Mheshimiwa Lema nakwambia hivi kwamba kauli uliyozungumza si kauli sahihi, hata ukienda kwenye Kamati ya Maadili utatuhumiwa kwa kosa lako. Tanzania haikuwahi kupata ushindi kwa mtutu wa bunduki, kwa hiyo naomba ufute hiyo kauli…

MBUNGE FULANI: Hataki

MBUNGE FULANI: Atoke nje, atoke nje.

MHE. GODBLESS J. LEMA: Tulishinda kesi ya uchaguzi Ndalambo kule Momba na mahakama ilisema polisi walitumia silaha kutangaza…

MWENYEKITI: Hiyo sio Tanzania, ni sehemu ndogo sana. Kwa hiyo, naomba hiyo iondoke nimeshaiondoa kwenye hansard. Malizia mchango wako, haya umeshamaliza basi ukae chini.

MWENYEKITI: Tayari, Mheshimiwa Lema naomba tumalize hapo basi…

MHE. GODBLESS J. LEMA: Nimemaliza?

MWENYEKITI: Naomba ukae chini tumalize basi.