Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kutumia nafasi hii na mimi niungane na wenzangu kwanza kuzipongeza kamati zote mbili ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Mahmoud Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini kwa kazi nzuri ambayo wameifanya na ushauri wa kina ambao wametupatia katika Wizara yetu, kwa kweli tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba kilimo ndio uti wa mgongo na tunafurahi kupata michango ya Wabunge wengi ambayo imechangiwa kwa kiwango kikubwa sana; na sisi tunasema kwamba tunapokea michango yote, tutaendelea kuifanyia kazi na baadae tutaona namna tutakavyoweza kutoa majibu hayo.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa sekta ya kilimo inachangia kwa kiwango kikubwa sana katika Pato la Taifa. Inachangia takribani asilimia 28.7 katika Pato la Taifa lna pia inachangia asilimia 65 mpaka asilimia 75 ya ajira mbalimbali ambazo watu wameajiriwa. Vilevile inachangia kwa asilimia 66 katika malighafi za viwandani, na pia tunachangia kwa asilimia 100 ya chakula chote na lishe tunachopata katika nchi hii; lakini zaidi ya hapo kilimo kinachangia kwa asilimia 30 ya fedha zote za kigeni.

Mheshimiwa Spika, kufuatana na mazingira yaliyopo tuna uwezo wa kuongeza uwekezaji katika kilimo na kikaweza kutoa mchango mkubwa zaidi kuliko hizi takwimu zilivyo hivi sasa. Kwa hiyo, pamoja na changamoto mbalimbali ambazo zipo lakini ni wajibu wetu sisi sote kuungana kwa pamoja katika kuhakikisha kwamba tunaondoka katika kilimo cha kujikimu kwenda katika kilimo cha kibiashara. Pia tutoke hapo tulipo ili tuweze kuhakikisha kwamba tunaondokana na tija ndogo na tunapata tija kubwa ili mazao mbalimbali yaweze kuzalishwa vya kutosha.

Mheshimiwa Spika, sasa ili tuweze kufikia hapo kuna mahitaji mengi ambayo tunayahitaji na ambayo Serikali imekuwa ikiyafanyia kazi na wajumbe wengi wamechangia katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, nianze na suala la mbegu. Ni kweli kumekuwa na takwimu ambazo zimetolewa na Wabunge mbalimbali juu ya mahitaji ya mbegu. Kama nchi mahitaji ya mbegu kwa sasa hivi ni tani 187,500; na ninaomba takwimu hizi zikae vizuri. Katika hizi tani 187,500, zinazohitajika kwenye nchi, mbegu ambazo zimepatikana kwa msimu huu mwaka huu ni tani 71,207 na kati ya hizo tani 66,033 sawa na asilimia 93 zimezalishwa ndani, hizo zimezalishwa hapahapa ndani, hazikutoka nje.

Mheshimiwa Spika, mbegu zilizotoka nje ya nchi ni tani 5,175, sawa na asilimia saba tu ya mbegu zote zilizopatikana hapa nchini; na hapa mbegu tunazozisema tunaachia mbali zile mbegu kama pingili za mihogo, miwa, chai, korosho, miche ya kahawa, yote hapa hatujayahesabu; ukihesabu na hiyo ambayo ipo zaidi ya milioni 22 maana yake uwezo wa taifa wa kuzalisha mbegu ni zaidi ya asilimia 96. Kwa hiyo, tunachotegemea nje ni kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunachosema sisi katika yale mahitaji ambayo tunayasema, kwa sababu upatikanaji ni tani 71,000 maana yake wananchi wengi bado wanaendelea kutumia mbegu za asili, ndizo zinazotumika, lakini si kwamba zinatoka nje. Lakini tunakubaliana na maoni ya wajumbe kwamba tunahitaji kuwekeza zaidi ili kuhakikisha kwamba mbegu zizalishwe wakati wa kiangazi, tuimarishe skimu zetu kusudi tuweze kupata mbegu za kutosha.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni mahitaji ya mbolea. Ni kweli kabisa mwaka huu mvua imenyesha vizuri sana katika maeneo mengi na mahitaji ya mbolea yameongezeka kwa kiwango kikubwa kwa sababu wananchi wengi wamehamasika katika kulima. Mahitaji ya mbolea ni tani 586,000 kwa mwaka lakini upatikanaji mpaka sasa hivi tunapoongea leo ni tani 454,339 ndizo zimepatikana. Katika hizo zipo mbelea aina ya DAP ambazo ni tani 71,000 na urea tani 121,000.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo kumekuwa kidogo kuna upungufu wa UREA, mbolea zingine zote zipo, UREA ilipungua. Tulichokifanya ni kuhakikisha kwamba tunaagiza. Hivi ninavyoongea kuna tani 43,000 zipo bandarini na tani 222,000 zipo njiani zinakuja. Lengo ni kutaka kuhakikisha kwamba tunakuwa na mbolea ya kutosha ili ziuzwe kama nguo zinavyouzwa hapa nchini. Kwa hiyo, mbolea zitakuwepo za kutosha bila tatizo lolote.

Mheshimiwa Spika, huu upungufu uliojitokeza ni kwa sababu yule ambaye tulimpa zabuni ya ku-supply kwa mtindo ule wa ununuzi wa pamoja alichelewa kuagiza na hivyo akachelewesha kidogo ndiyo maana tukawa na upungufu wa aina moja ya mbolea, lakini zingine zote zinapatikana kwa wingi hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, mahitaji ya viuatilifu ni mengi na kweli Wabunge wamechangia kwa kiwango kikubwa na sisi tunasema ni kweli kabisa tunahitaji viuatilifu vya kila namna, utafiti tutafanya na maeneo mengine yoyote tutayarekebisha.

Mheshimiwa Spika, najua kwa sababu ya muda haukuweza kutosha, tungeweza kujibu maswali yote lakini tutaweza kuwajibu Wabunge na tutaleta mbele ya Bunge lako Tukufu, ahsante sana. (Makofi)