Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

Hon. Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia, kuwa mchangiaji wa kwanza jioni hii. Nashukuru sana na nitangulie kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi yake ya uhai na kwa mema mengi ambayo ametujalia katika Bunge letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kuwapa pole Watanzania wenzetu ambao wamekumbwa na maafa ya mafuriko na nimuombe pia Mwenyezi Mungu aiepushe nchi yetu na majanga ya aina hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuipongeza Ofisi ya Spika pamoja na Bunge letu kwa kazi nzuri ambayo tumeifanya jana ya kuwaenzi Maspika wastaafu. Kwa kweli ni kazi moja nzuri sana na ya kihistoria; naomba tujipongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa napenda pia kuishukuru Ofisi ya Spika kwa kuboresha vishikwambi, vimeboreshwa sana na vishikwambi hivi Kamati zetu zimeweza pia kutumia kwa kufanyia kazi za Kamati na vimefanya kazi nzuri sana. Na ukichukulia kwa mfano Kamati ya LAAC tulikuwa tunabeba vitabu vikubwa sana, vinaweza vikafika karibu kilo tatu au zaidi ambavyo vilikuwa vinatutesa sana, lakini kwa vishikwambi hivi sasa tumeepukana na hiyo adha, kwa hiyo tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuunga mkono taarifa za Kamati ya LAAC ambayo ni Kamati yangu, ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC, lakini pia Kamati ya PAC, naunga mkono taarifa zao, au taarifa zetu kwa asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme ninachozungumza ninaongezea tu pale ambapo Kamati ya LAAC imezungumza kupitia Makamu Mwenyekiti wetu, kwa hiyo mimi ntaongezea kiasi fulani. Na nianze kusema kwamba katika maendeleo ya halmashauri au katika maendeleo ya Taifa kwa ujumla, cha kwanza kabisa ni lazima tuwe na rasilimali watu, lakini watu hawa tunaowasema ni lazima wawe ni watu wenye uwajibikaji wa kuridhisha. Lakini pia tunahitaji kitu kingine ambacho ni rasilimali fedha pamoja na vile vingine ambavyo alikuwa akivisema Hayati Baba wa Taifa; ardhi, siasa safi, uongozi bora, lakini mimi ntazungumzia hivi vitu viwili; rasilimali watu na rasilimali fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tukienda katika halmashauri zetu tumekuwa na changamoto kubwa sana katika ukusanyaji wa mapato, na hili linatokana na baadhi ya watumishi kutokuwa waaminifu na vitu ambavyo vimekuwa vikitumika, zile nyenzo ambazo ni mashine za POS, watumishi hawa wamekuwa wakitumia POS bandia, mashine za POS bandia, lakini vilevile wakati mwingine wamekuwa wakizima data, na kuna wakati pia wanazitumia kwa matumizi tofauti na yale ambayo yamekusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu naipongeza sana Wizara ya TAMISEMI inayosimamiwa na Mheshimiwa Waziri Jafo na Naibu Mawaziri wake kwa uamuzi ambao wamechukua hivi karibuni. Uamuzi huu ni wa kuleta mashine mpya za POS ambazo zimeboreshwa vizuri sana. Mambo kama haya ambayo wamekuwa wakiyafanya hayawezekaniki katika mashine hizi mpya. Kwa hiyo, wameleta na wamesambaza mashine ambazo ni zaidi ya 7,000 katika halmashauri zote, mashine ambazo zimeboreshwa, ni za kisasa na zina identification yake kabisa, hawawezi wakatumia mashine bandia.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kikubwa zaidi niseme tu kwamba tunapaswa kumpongeza sana Mheshimiwa Jafo na ofisi yake kwa jinsi ambavyo wamepunguza gharama za kuleta hizi mashine. Wameleta mashine kwa gharama ya asilimia 30 ya ile gharama ambayo ilikuwa ikitumika mwanzoni kununua mashine hizohizo. Kwa hiyo, tunapaswa wote kujifunza na kuiga uzalendo huu ambao wenzetu wametumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo niseme tu hivi karibuni halmashauri nyingi zimepunguza uwezekano wa kuwa na hati chafu, halmashauri zenye hati chafu ni chache sana. Lakini nitahadharishe tu kwamba kuwa na hati safi haimaanishi kwamba halmashauri zenye hati safi ndizo zinazofanya kazi nzuri kimaendeleo; hii si kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hii inatokana na nini; ni kutokana na mfumo wetu wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo kwa sasa. Tunachokagua, unakuta tunakagua input na output, lakini performance audit tumeiacha, impact hatuiangalii sana. Kwa hiyo, tunakwenda kwenye input ambayo kwa Kiswahili nimetafuta sana Kiswahili chake, tulihangaika sana kwenye Kamati lakini nimepekuapekua nikakuta input ni pembejeo, ila sio pembejeo za kilimo. Ukisema input ina maana ni pembejeo, na output ni pato ila sio mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunakwenda kwenye input-output, ikiwa na maana kwamba kama unajenga kituo cha afya umeweka input pale ambazo ni fedha, na output ni kituo cha afya. Sasa tunashindwa bado Ofisi ya Mkaguzi inahitaji kuimarishwa zaidi ili iweze kufanya performance audit. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwa uchache kutolea mfano mradi mmoja wa maji; unaweza usiamini kwamba tuna engineer wa maji ana-design mradi lakini ana-skip ile hatua ya kufanya water treatment, na mradi huu unaripotiwa kwamba umekamilika. Lakini ukishafika kwenye mradi sasa kuangalia performance au impact ya ule mradi, wananchi hawachoti maji pale badala yake wanaendelea kuchota maji katika visima binafsi, tena kwa kununua. Kwa hiyo, hapa ndipo mahali ambapo naona kuna gap, na kwa sababu hiyo niombe sana Ofisi ya Mkaguzi Mkuu iwezeshwe ili iweze kufanya performance audit. Ni kengele ya kwanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utakuta pia – pengine itakuwa ni makusudi ana-skip hii hatua. Na miradi mingi tumeikuta hivyo, ni Kamati tumekwenda na tumekuta mambo kama hayo. Sasa wana-skip baadhi ya hatua, lakini baadaye kuna kichochoro fulani, kichaka tuseme, cha kuibia fedha, wanaweka variation kuongeza fedha na zile fedha unakuta ni nyingi sana, na kwa sababu hiyo sasa ndipo ubadhirifu ambapo unatokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nisingependa niongee mengi sana lakini pia niombe hata kwenye vituo vya afya tuangalie suala la kuboresha hivi vituo vya afya viendane na kupunguza vifo vya akina mama na watoto. Kwa sababu kituo cha afya ni jambo moja lakini impact au ile athari ndiyo tunayoitaka hasa. Sasa tatizo ni ule usimamizi wa wale wahusika katika yale maeneo; waganga wakuu wa wilaya, waganga wakuu wa mikoa, sidhani kama wanafanya usimamizi wa kutosha kwa sababu ukiangalia takwimu utakuta kwamba kazi imefanyika kubwa, fedha zimetumika nyingi lakini vifo vya akina mama na watoto viko palepale katika baadhi ya maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)