Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi hii ya kuchangia Mpango huu wa Taifa ambao ni muhimu sana. Kabla sijaanza napenda kutoa pole kwa wananchi wa Muheza kwa mafuriko ambayo wameyapata pamoja na Mkoa mzima wa Tanga na kuwahakikishia kwamba Serikali inashughulikia matatizo yao na athari zote ili kurudi kwenye hali ya kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Waziri Dkt. Mpango kwa kutuletea Mpango mzuri na ambao hata ukiuona unaona kweli uko kwenye mwelekeo mzuri. Mimi sitakwenda kwenye takwimu ambapo naona tunakwenda vizuri kwenye ukuzaji wa uchumi ambao kwa sasa tuko kwenye asilimia 7.2 na tunategemea 2020/2021 tufikie asilimia 10 na hata mfumuko wa bei uko vizuri tu kwenye asilimia 3. Kwa hiyo, nitajikita kwenye miradi ambayo imeanza na inaendelea kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo limezungumzwa kwa bidii sana na wachangiaji wengi lakini na mimi napenda kuongeza kwamba tunategemea kwenye Mpango huu ambao utakuja basi suala hili lipewe umuhimu wa kipekee. Tunaamini kabisa kwamba kilimo ambacho Watanzania wengi wanafanya na kinatoa ajira karibu asilimia 65 tunategemea kwamba kitatuinua. Ni suala la kuweka mipango vizuri kuhakikisha kwamba suala la umwagiliaji linapewa kipaumbele, suala la uanzishwaji wa mabwawa linapewa kipaumbele na naamini kabisa kwamba tukiweka fedha nyingi kwenye kilimo basi tutaweza kuendelea kwa haraka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na mambo hayo, kuna masuala mengine ambayo yako kwenye kilimo kwa mfano suala la chai. Nimefarijika sana hapa nilipomsikia Naibu Waziri asubuhi akisema kwamba wana mpango wa kuanzisha mnada hapa nchini na kuondokana na suala la mnada wa Mombasa. Suala hilo sisi Muheza limetuathiri sana kwa sababu kampuni kubwa ambayo inalima chai pale inapeleka chai yake kwenye mnada Mombasa na Mombasa wananunua na wanafanya packaging na kurudisha tena kuuza hapa hapa nchini. Suala hili kiuchumi kwakweli linatuathiri sana na ni vizuri liangaliwe kwa uhakika na umakini kabisa ili tuanzishe mnada wetu hapa tuondokane na kupeleka haya mambo Mombasa. Vivyo hivyo ni vizuri pia kuangalia mazao mengine na kuanzisha hasa mazao ya viungo na mazao ya machungwa ili tuweze kuwa na bei elekezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Kitengo cha TMX ambacho Kamati ya Bajeti ilitembelea, kitengo hiki ni kizuri sana ambapo kikitumika vizuri basi Serikali inaweza ikawa na mazao mengi elekezi kwa bidhaa nyingi sana. Naomba kabisa Mheshimiwa Waziri Kitengo hiki kitumike ipasavyo. Tulikwenda pale lakini tumeona kwamba kitengo hiki hakitumiki kama inavyopaswa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile limeongelewa suala la uvuvi, Bandari ya Uvuvi ni muhimu sana. Bandari hii ilianzishwa kwenye bajeti iliyopita na ilitengewa fedha, nakumbuka mwaka 2017 kuna fedha ambazo zilitengwa lakini haijapewa umuhimu wake. Tunaamini kabisa kwamba tukifungua Bandari ya Uvuvi basi tutakuwa tumefika mbali sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la PPP ambalo nimekuwa nikiliongelea kila mara na naamini kabisa juhudi ambazo zinafanywa na Serikali sasa hivi, miradi hii mikubwa yote, SGR, ndege, umeme kwenye Bwawa la Nyerere naamini kabisa haya yangeoana na PPP sasa hivi hapa Tanzania tungekuwa tuna-boom. Kwa hiyo, naamini kabisa kwamba tumepitisha sheria hapa mwaka jana lakini mpaka sasa hivi hatujaona utekelezaji wake. Mheshimiwa Waziri tumekuwa tukisisitiza na naomba kusisitiza kwamba tangaza hiyo miradi ambayo tumeichagua. Tuliiona hapa miradi kumi ambayo bajeti iliyopita mlitusomea, tafadhali itangazwe ili watu wajitokeze na kama hawatajitokeza tuone tuna tatizo gani lakini ni suala ambalo linatakiwa lipewe umuhimu mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ATCL tumepita, nashukuru ndege zimefika lakini cha msingi hapa ni kuhakikisha kwamba tunaboresha na tunaanzisha route nyingi zenye tija ili kuweza kuleta watalii na wawekezaji hpa nchi kwetu. Tunataka Airport ya Dar es Salaam iwe hub, tuhakikishe kwamba hii Terminal III ambayo ipo inatumika kikamilifu. Sasa Terminal III bado ndege ziko chache lakini tunaamini kabisa kwamba wanaohusika watafanya juhudi kuweza kushughulikia na kuhakikisha kwamba Airport yetu inakuwa changamfu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la bandari ni muhimu sana. Uboreshaji wa bandari umekuwa mzuri, Bandari ya Dar es Salaam inaboreshwa vizuri, vilevile ya Tanga na Mtwara. Nimefarijika sana kwamba sasa hivi Bandari ya Tanga inachimbwa ili kuweza kupata kina kikubwa na naamini baada ya kazi hiyo kukamilika basi meli kubwa zitaweza kutua pale badala ya kwenda kutua Mombasa ambapo ilikuwa zinatua kule na baadaye zinaweza kuletwa hapa nchini. Kwa hiyo, suala hili ni la kupongezwa na tunaomba kabisa muendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa bajeti nilizungumzia kiwanda kimoja kikubwa sana ambacho kinatarajiwa kujengwa na Wachina kule Tanga Hengia. Kiwanda hiki cha saruji tunategemea kitakuwa kikubwa na kuleta ajira kati ya 4,000 mpaka 8,000. Kiwanda hiki tunategemea kitoe tani karibu milioni saba kwa mwaka lakini nilipopita mara ya mwisho Tanga sioni chochote ambacho kinafanyika naambiwa tu mazungumzo bado yanaendelea kuweza kuwaruhusu Wachina hawa waweze kuweka hiki kiwanda. Kiwanda hiki ni kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapopata wawekezaji kama hawa inabidi na sisi tuchangamke wasije wakatupokonya. Kwa hiyo, naamini kabisa wakati wa winding up na nashukuru Waziri wa Uwekezaji yupo hapa watupe msimamo kiwanda hiki kimefikia wapi. Hawa Wachina wanazunguka karibu miaka miwili hapa na vibali mara hiki mara kile, mara incentives sasa tunaomba tupate uhakika nini kinaendelea. Huyu ni mwekezaji mkubwa na tunaamini kwamba atakapoweka kiwanda kile basi mambo yatakuwa vizuri sana siyo kwa nchi hii tu bali hata kwa Mkoa wa Tanga mambo yata-boom.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka kulizungumzia, la mwisho ni suala la Soko la Hisa pale Dar es Salaam (Dar es Salaan Stock Exchange) tulifika pale lakini soko hili limeonekana limeduwaa kidogo haliko very active na tunaona haliko very active kwa sababu watu wengi hawajaliorodhesha, nataka Mheshimiwa Waziri ahakikishe kwamba Sheria ilishapitisha mashirika yote haya ya communication kwamba wajiandikishe kwenye soko la hisa, lakini mpaka sasa hivi ni Vodacom tu ambao wamejiandisha, sasa haya mashirika mengine ya simu kwa nini hayajajiandikisha? Nataka Waziri akija hapa aeleze ili tuweze kujua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni kwamba Soko la Hisa la Dar es Salam lilikuwa linachangamshwa sana na haya mashirika ya kijamii. Sasa baada ya kuunganisha haya mashirika ya kijamii, tangu uunganisho huo umefanyika, shirika hili letu la sasa hivi halijajiandika tena pale wala halijapeleka kununua hisa wala kuuza hisa. Tunaomba shirika hili ambalo limejumuisha mashirika yote ya kijamii basi lijiandikishe ili liweze kufanya lile soko la hisa liweze kuwa very active, baada ya kusema hayo nakushukuru sana na naunga mkono mpango huu. Ahsante sana. (Makofi)