Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia muda huu. Naomba nimshukuru Mungu kwa kutulinda mchana kutwa na ametupa fursa tena kwa mara nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Waziri pamoja na Naibu Mawaziri wote wawili kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Kusema kweli Mheshimiwa Hasunga hongera sana, tunamwona jinsi anavyokimbizana. Nafikiri mafanikio kupitia kilimo kwa Watanzania yatawezekana, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Mkoa wetu wa Katavi tunalima zao la tumbaku. Zao hili sasa hivi limeweza kuyumba kwa sababu, makampuni ambayo yanakuja kuchukua zao hili katika Mkoa wetu wa Katavi wameleta makisio kwa wakulima, kila mwaka wanaweka makisio, sasa kila siku wananchi wa Katavi wanavyopewa yale makisio sio ya kupanda ila makisio yale ya kushuka. Sasa kutokana na hiyo uchumi kidogo wa Mkoa wetu wa Katavi umepungua kwa sababu zao hili kupitia halmashauri zetu zilikuwa tunapata manufaa makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kwa sababu, zao hili ni zao la kibiashara. Najua Waziri ana mikakati mingi mikubwa, mipana, naomba hili zao lifufuliwe upya, tutafute wadau ambao watakuja kununua zao letu la tumbaku kwa sababu, sasa hivi Mkoa wetu wa Katavi kupitia halmashauri zetu mapato yamepungua sana. Sasa sio kwenye halmashauri zetu tu hata Taifa mapato yameshuka, naomba tukazie mkazo kupitia tumbaku zao hili liweze kutafutiwa wadau ili waweze kununua katika msimu ujao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Serikali, katika Mkoa wetu wa Katavi msimu huu na msimu uliopita tulilima pamba. Pamba imeitikiwa sana hususan katika Wilaya yetu ya Tanganyika wamelima takribani kilo milioni 16 wananchi wameweza kufanikiwa kupata. Naomba sasa Bodi ya Pamba iweze kuja kuchukua kwa sababu, wananchi wetu wa Katavi pamba hiyo wameivuna wameweka majumbani. Sasa ili tuweze kupata manufaa makubwa na wale tuweze kuwapa hamasa kubwa wananchi wa Mkoa wa Katavi tunaomba basi hii Bodi iweze kuja kununua ili sasa wananchi hawa waweze kutafuta mbegu nyingine kwa ajili ya msimu ujao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja katika mbolea. Pembejeo ni kitu muhimu sana, naomba, ndani ya nchi yetu tuna mazingira tofauti ya hali ya hewa. Ukiangalia Mkoa wa Katavi, Rukwa, Kigoma mvua zinaanza kunyesha mwezi wa Kumi, Kigoma mwezi wa Tisa katikati mvua zinaanza kunyesha. Sasa pembejeo zinakuja Mkoa wa Katavi Januari, je, Januari huyu mkulima atapata manufaa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima hawezi kupata manufaa hata kidogo. Vilevile sasa hivi kuna matapeli wengi wanawaletea wakulima wetu pembejeo feki ambazo hazina tija kwa sababu, wanajua kabisa huku mjini watu wanaelewa; wanajua kuwa wakipeleka vijijini kule watu hawaelewi wanawapelekea pembejeo, wanawapelekea viatilifu ambavyo ni vya bandia, fake, sasa tija inakosekana. Mkulima analima akiweka ile mbolea, vile viatilifu havina manufaa katika ule mmea, sasa wananchi wetu wanapata hasara. Naomba kwa sababu tuna Shirika la ASA, shirika hili ni zuri sana, sasa hivi shirika hili linafanya kazi nzuri na ukizingatia sasa hivi wanajiendesha wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wao wanalima mbegu na mbegu yao ni bora halafu wanauza bei rahisi. Kwa kilo ya alizeti wanauza Sh.3,500 lakini tukienda madukani mbegu ileile inaizwa Sh.35,000 mpaka Sh.70,000, sasa tuimarishe Shirika hili la ASA ili sasa Watanzania waweze kupata tija kwa sababu, shirika hili litafanya kazi nzuri zaidi. Vilevile shirika hili halipati pesa miaka mitano sasahivi hawajapeleka pesa kwenye Shirika la ASA. Naomba tuliimarishe Shirika hili la ASA litakuja kuwaletea tija Watanzania kwa sababu ni shirika la wazalendo, sasa sidhani kama wanaweza wakafanya vitu tofauti, vilevile hizi mbegu fake, viatilifu fake, vitapotea shirika hili tukiliimarisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kwenye umwagiliaji. Kwetu Mpanda, Wilaya ya Tanganyika, Kata ya Kalema tulipeleka pesa kwa ajili ya umwagiliaji, ile skimu haijamalizika mpaka leo. Wanajua kama hizi skimu zinatumia pesa, wakandarasi, siku hadi siku value for money inabadilika, ina maana hii skimu sasa hivi haiwezi kufaa tena na wananchi wa Kalema hawawezi kupata tija. Sio Kalema tu katika Mkoa wetu wa Katavi kuna Kata ya Ugala, skimu yake mpaka leo ilimalizika, lakini haifanyi kazi, ina maana kuwa inaharibika haitaendelea kufanya kazi vizuri. Tuna Kata ya Urwila skimu yake haijakaa vizuri, tuna Kata ya Mbede skimu yake nayo haijakaa vizuri, naomba katika kata hizi ambazo tumeweka umwagiliaji, umwagiliaji ndio mkombozi wa Watanzania. Tukiweka skimu hizi vizuri, hawa wananchi wakilima mara mbili mara tatu tutapata faida kubwa na mazao mengi yataweza kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya nchi yetu ya Tanzania kuna Kanda ambayo Iringa, Njombe, Ruvuma, Songwe, Rukwa, Katavi, katika zone hii ni wakulima sana wa mahindi. Sasa hivi ukiangalia katika nchi ya Zaire kuna uhaba sana wa chakula wananchi wengi wanapeleka mazao yao Zaire na sisi ndani ya Mkoa wetu wa Katavi kupitia Kata yetu ya Kalema inajengwa bandari pamoja na Rukwa inaweza kujengwa bandari, ili kanda hizi zote wakapeleka mazao yao katika Bandari ya Kalema pamoja na Kasanga, mazao haya yakapelekwa Zaire Watanzania hawa wakapata kipato kupitia bandari hizo mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwa sababu, nchi ya Zaire hakuna chakula, Burundi wanategemea sana Tanzania, tukiweka mazingira mazuri nafikiri tutapata mafanikio makubwa sana. Naomba sana kupitia Waziri Mheshimiwa Hasunga, najua alikuwa anafanya ziara sana wakati ule alivyokuwa maliasili...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)