Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia katika hoja iliyoko mezani. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia kupata nafasi hii. Nitaanza kuchangia katika suala la mazao mkakati ambayo unayaona hayamo ndani ya utekelezaji katika bajeti nzima ya mwaka huu. Zao la kwanza katika Tanzania ambalo linaingiza uchumi mkubwa ni zao la korosho. Hata hivyo, zao hili la korosho halimo kabisa kama ni zao ambalo linaweza kuchangia uchumi wa nchi wameliacha nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima analima, anasafisha shamba, anapulizia dawa, lakini unapofikia wakati wa kuuza anaanza kukwamishwa anaambiwa ana kangomba, sasa nini maana ya kangomba? Ni vitu ambavyo vinajitokeza kuwakwamisha wafanyabiashara wasiweze kufanya biashara ya tasnia ya korosho. Kwenda kununua mchele Mbarali sio kangomba, kwenda kununua mahindi Rukwa sio kangomba, kwenda kununua chochote sio kangomba, kangomba inaingia kwenye zao la korosho. Tujiulize swali, je, huyo mwananchi aliyekuwa kijijini maporini, barabara hakuna anaipelekaje korosho yake Liwale Mjini? Mwananchi aliyekuwa Namtumbo kijijini anapelekaje korosho yake Namtumbo Mjini wakati hakuna barabara? Sasa iweje watu wengine wanapewa nafasi ya kuleta mazao yao wakayauza huria lakini inapofika tasnia ya korosho tunaambiwa ni kangomba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wameshindwa kufanya biashara zao safari hii, wamekwamisha uchumi kwa ajili ya kangomba. Naiomba Serikali iliangalie neno la kangomba ilifute kabisa kwa vile kama wengine wanaweza kufanya biashara Tanzania nzima haina haja ya kuliweka neno la kangomba likawakwaza wananchi. Mwananchi amekaa Mpigamiti anataka kuja Liwale hana gari, hana usafiri, anapelekaje korosho yake. Naomba hili neno la kangomba lifutwe kabisa linaleta chuki na maudhi katika maeneo ya wakulima wa korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la korosho na mazao mengine mchanganyiko hayakutengenezea mfumo wa kibiashara ambao ungeweza kusaidia mazao yao yaweze kununuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa Rwanda wametengeneza one stop center kwa ajili ya manunuzi ya biashara zao, wamejiingiza katika World Trade Center mbalimbali duniani, leo sisi tunategemea mazao yote tupeleke Kenya au Uganda au Rwanda, tujiulize wataalam wetu wanafanya kazi gani hapa Tanzania? Wanafanya nini kuhakikisha wana-promote mazao? Tanzania tuna mazao lakini huwezi kuuza mazao yako mpaka yapelekwe Rwanda, kwanza tujiulize tumezidiwa nini na Rwanda mpaka sisi tukashindwa kufanya vile? Pana upungufu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kakunda alikuwa mjumbe mwenzangu, namfahamu, ana uwezo mkubwa sana, pale unapoona kuna watendaji ambao huwezi kufanya nao kazi, bwana mhamishe au mtoe, sasa hivi tunataka Tanzania yenye uwezo, yenye uchumi na utekelezaji katika masuala ya biashara na viwanda. Hao ndio tunakwenda nao na unamwona Mheshimiwa Rais amesimama, ana uchungu lakini, je, unao watendaji wa kufanya nao kazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja suala la balance of trade; leo Tanzania tunasema tunataka uchumi wa viwanda, watu wameanzisha viwanda, leo Kiwanda cha Dangote, tunaagizia katika miradi mikubwa ya Stiegler’s Gorge na miradi mikubwa ya SGR, wanaagiza cement Tanzania walikaa nao chini wakasema jamani ongeza viwango vyako ili angalau cement ya Dangote iende katika uchumi wa maendeleo tunayofanya sasa hivi. Matokeo yake dola imepanda, kila kitu sasa hivi na wahujumu wanapitia humo humo kuingiza cement kutoka nje, nondo kutoka nje, vifaa vyote vya ujenzi vinatoka nje, tutakwenda katika uchumi ambao hauna balance of trade. Tuna wafanyabiashara wanaoleta vinywaji, maji yanatoka China, juice zinatoka China, kila kitu kinatoka nje Bakhresa atafanya kazi gani, Udzungwa atafanya kazi gani, tumefikia mahali halafu wanapewa misamaha ya ushuru, wanapewa zero VAT, matokeo yake atakwendaje mfanyabiashara wa ndani, hivyo tunavokwenda ina maana tunapingana na mifumo na sheria ambazo zinawakwaza wafanyabiashara. Wafanyabiashara kila mmoja anafunga (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi wa vyandarua huko Arusha, chandarua kinatoka China zero kibovu, sasa huyu atauza chandarua bei gani A to Z ameshakuja zaidi ya mara tano anajiuliza zinaletwa chandarua mbovu na Tanzania bado tuna malaria, analeta chandarua ambacho kina dawa na kila kitu anaambiwa bwana, hawasikilizwi tu! Tumefika mahali tunajiuliza kweli tumetaka nchi hii tuiendeleze, mfumo tuliokuwa nao uko sahihi na uchumi wetu, tumejipanga kweli ama laa. Maana yake kujipanga at least 10 years mbele ili angalau tujue tunafanya moja, mbili, tatu, matokeo yake pale panaachwa hapa panashikwa, matokeo yake watu wamekaa desperate hawajui wanafanya nini kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imani yangu, tujipange maana yake nikiangalia nenda Temeke maduka yamefungwa, Kariakoo maduka yamefungwa, kila mahali maduka yamefungwa, leo Watanzania wanakwenda kununua bidhaa Uganda, bandari iko Dar es Salaam ukichukulia mzigo kutoka Dar es Salaam mpaka Uganda unalipwa lakini kwa nini anapata unafuu wa kwenda Rwanda, pana kitu kimesimama hapa. Sasa nataka niorodheshe katika vitu ambavyo vinaukwamisha uchumi wa biashara na viwanda kwanza TRA. TRA ni mwiba, mwiba, mwiba wa uchumi wa Tanzania, watendaji wabovu ambao wako ndani ya TRA wamejigubika wimbi la TRA wanaifanya nchi hii iyumbe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kusema ni wapi, isipokuwa waifumue TRA na waaangalie upungufu uko wapi, maana yake leo unafungua kampuni, hujaanza kazi wanakwambia tunakudai, watakusumbua na kesho wanakwambia tunakufungia. Mwenye kiwanda ana vurugu mara OSHA, pana regulatory bodies 47 atafanyaje kazi mtu kama huyu? Ina maana tumewakwaza wafanyabiashara wasitoke, matokeo yake tumebakia tumesimama, mbele hatuendi, nyuma hakutikisiki, mtihani kabisa mimi nauona huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inakuja ajira ndani ya viwanda, nilikuwa Kamati ya PIC, tukatembelea kiwanda cha EPZ cha kutengeneza jeans, unasema Tanzania tumeajiri watu 59,000 wameajiriwa kama vibarua, wanachukuliwa kila baada ya miezi mitatu. Baada ya pale anafukuzwa, inakuja benchi ya pili, hii huwezi kuita ajira. Ajira ambayo na analipwa mshahara mdogo kwa mwezi 100,000 na wanakimbia kuwa atalipwa haki zake za msingi. Sasa tunatakiwa tuangalie viwanda vinaendana na matatizo ya ajira, isiwe tunaleta viwanda lakini ajira tunawaletea watu wa nje na maeneo mengine kama unaenda unakuta wamejaa watu wa nje sio Watanzania. Tulisimamie suala la viwanda vya ndani na ajira ya Watanzania ili kuweza kuleta tija na Watanzania hao wajione wako katika nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejionea Kiwanda cha Dangote kikiajiri watu kutoka nje 120 mpaka wafagiaji, sasa tunajiuliza, watu wale wa Mtwara ambao tumesema tutapata opportunity ya kupata kazi na kupata ajira na kila kitu mpaka mfagiaji anatoka nje, tuna haja gani ya kuwa na Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanzisha viwanda, tunasikia leo tumeleta matrekta, vijana hawa wadogo wanaomaliza darasa la saba ilibidi wapelekwe VETA wakasomee hata ufundi mchundo iwasaidie hata trekta likiharibika atakuwa anaweza kufanya kazi na ndio walivyotoka China, walivyotoka Thailand na nchi mbalimbali, lakini vijana wale wamekaa majumbani, wanacheza pull, wanakula madawa ya kulevya, matokeo yake mfumo wa kibiashara uliotengenezwa katika kipindi kifupi umefanya nchi imedhoofika na imedorora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nasema nashukuru sana. (Makofi)