Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nipende kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kuamua kuleta mabadiliko katika nchi yetu. Nchi yetu ilikuwa na changamoto na maamuzi makubwa na maamuzi sasa yanafanyika, pongezi kubwa sana ziende kwake, hasa ununuzi wa ndege, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais; ujenzi wa viwanja vya ndege, kazi kubwa zinafanyika, sisi wote ni mashahidi katika maeneo yetu; ujenzi wa madaraja na barabara kubwa zinazojengwa ndani ya nchi yetu. Haya yote ni maamuzi ambayo Mheshimiwa Rais ameamua binafsi na wananchi wa Jimbo la Manonga tunampongeza na kumuunga mkono Mheshimiwa Rais na tunasema aendelee kuchapa kazi, sisi tuko tayari kumuunga mkono mchana na usiku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwapongeze watendaji wakuu, Mkurugenzi Mkuu wa TANROADS, Mheshimiwa Engineer Mfugale; lakini pia nimpongeze mwalimu wangu aliyenifundisha chuoni, Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA, Mheshimiwa Mr. Ngewe, pongezi ziende kwake. Amefanya kazi nzuri sana na nimeona juzi kapata hati ya utumishi bora, kwa hiyo nitumie nafasi hii kumpongeza mwalimu wangu kwa kazi nzuri anazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nimpongeze Mkurugenzi Mkuu wa Viwanja vya Ndege, Mheshimiwa Dkt. Hamza Johari, Mwalimu wangu, naye anafanya kazi nzuri, hawa wote Walimu wangu wanafanya kazi nzuri sana, nafurahia, naona jinsi gani wanavyo-perform katika maeneo yao, bila kumsahau Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, naye nampongeza kwa siku ya leo. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kumteua tena kwa mara nyingine aendelee kuhudumu kwa nafasi hiyo ya ukuu wa chuo. Natambua alikokitoa chuo, hali ilivyokuwa na ilivyo sasa hivi ni chuo tofauti sana, pongezi nyingi sana ziende kwako Dkt. Mganilwa, kwa kazi kubwa unazozifanya, tunakupongeza, sisi wanafunzi wako tuko Bungeni tunaona matunda unayoyafanya huko ulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, niwapongeze Mawaziri; Mheshimiwa Engineer Nditiye pamoja na Mheshimiwa Kwandikwa bila kumsahahu Waziri wake, Mheshimiwa Engineer Kamwelwe; Mheshimiwa Waziri anafanya kazi nzuri sana, pongezi nyingi sana ziende kwake maana yake leo nilisema niwapongeze kwa kazi wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nisisahau kumkumbusha Mheshimiwa Engineer Kamwelwe, Waziri kwamba wananchi wake wa Mpanda kule wanapokuwa wanatoka huwa wanapewa rufaa kwenda kutibiwa Tabora, wakienda Tabora na kwenyewe wanapewa tena rufaa ya kwenda kutibiwa pale Hospitali ya Nkinga lakini wakifika pale Ziba kwenda Nkinga barabara ni mbaya sana. Naomba Mheshimiwa Waziri aweke lami pale ili wagonjwa wanaotoka Mpanda, Katavi, Majimoto wapate huduma safi pale Nkinga ili kuwarahisishia wananchi wake wapite kwa urahisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Engineer Kamwelwe kwamba aanze basi na usanifu; barabara ya Ziba- Nkinga – Puge; barabara ya Ziba – Choma na kwa kutambua kwa sababu Choma Chankola kuna kiwanda kikubwa cha pamba. Kwa hiyo kwa sababu tuna kiwanda lazima miundombinu tuiboreshe na Serikali hii tunanadi ni awamu ya viwanda. Kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Waziri katika bajeti yake sijaona akitenga angalau usanifu na barabara hii ya Ziba – Choma, Ziba – Nkinga – Puge ni barabara inayomilikiwa na TANROADS, nimwombe Mheshimiwa Waziri aikumbuke barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, Mheshimiwa Waziri, Engineer Nditiye ile minara…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya Wizara hii, lakini minara Mheshimiwa Engineer Nditiye pale…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.