Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. William Mganga Ngeleja

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ili nichangie hoja iliyoko mbele yetu. Awali ya yote kabisa naungana na wenzangu kuiunga mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri, Engineer Kamwelwe. Pamoja na hayo, nitumie nafasi hii kumpongeza yeye, kuwapongeza Waheshimiwa Naibu Mawaziri; Mheshimiwa Engineer Kwandikwa na Mheshimiwa Engineer Nditiye, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Watendaji wote katika taasisi ambazo ziko chini ya Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo imejitokeza hapa na mjadala unavyoonyesha, ni kwamba Wizara hii imepata fedha nyingi na imekuwa ikiendelea kupata fedha nyingi kwa sababu ni mhimili wa uchumi wetu kwa kadri ambavyo tunaelekea kuifikia nchi ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajadili hoja iliyoko mbele yetu tukiwa tuko katikati kama Taifa kwenye majonzi ya msiba wa Marehemu Mzee Mengi na tunafahamu kwamba jana amelazwa katika makazi ya milele, nasi ndio tunasubiri ratiba yetu kwa kadri Mwenyezi Mungu atakavyotujalia. Kwa hiyo, natumia nafasi kuungana na Watanzania wenzangu kutoa pole kwa familia ya Mzee Mengi, ndugu na jamaa, lakini kuungana na Watanzania kumwombea Mzee Mengi aendelee kulazwa mahali pema Peponi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie kuhusu Jimbo la Sengerema. Kitabu hiki ambacho kwa ujumla wake kinaomba karibu shilingi trilioni tano, Sengerema ni mojawapo ya wanufaika katika miradi ambayo imekuwa ikitekelezwa na ile ambayo iko katika hatua za mwisho kabisa kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaarifu wananchi wa Jimbo la Sengerema kwamba ile barabara yetu ya kutoka Sima kwenda Ikoni inayosimamiwa na TANROADS Mwanza, Barabara yetu ya kutoka Sengerema kwenda Ngoma A zinaendelea vizuri. Pia ile ya Sima – Ikoni, Mkandarasi wetu KASCO anamalizia kipande cha kutoka Sengerema kwenda Nyamazugo. Atakapokimaliza kile, anahamia Sima kwenda Ikoni kuunganisha na Jimbo la Geita Vijijini. Kwa hiyo, ni kazi inayoendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiingia kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Serikali imetukumbusha kupitia hotuba hii kwamba maandalizi ya bajeti hii yamezingatia pia Ilani ya Chama cha Mapinduzi, maelekezo ya Viongozi Wakuu pamoja na Mpango wetu wa Miaka MItano. Sasa kwenye ukurasa wa 60 pale wa Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi kuna barabara inayotajwa pale ya Kamanga – Sengerema kilometa 35.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwani hatua za awali zilishafanyika; upembuzi na usanifu wa kina tayari na sasa nawaarifu Wana-Sengerema kwamba wajiandae kwa sababu mipango yote sasa imeshahamia Serikalini na hasa kwa Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Engineer Mfugale. Nimekuwa na mawasiliano naye, iko kwenye mpango, tunasubiri muda muafaka utakapofika, itatangazwa tenda kwa ajili ya kupata mkandarasi kuanza ujenzi wa lami kwa barabara ya Kamanga – Sengerema na ule mchepuko wake wa Katunguru kwenda Nyamazugo, kilometa 21. Kwa hiyo, naishukuru sana Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu pia kwamba upembuzi yakinifu unaendelea na usanifu wa kina kwenye barabara ya Nyehunge kuja Sengerema ama Sengerema – Nyehunge, kilometa 78. Napo tunaishukuru Serikali kwa sababu ni kazi inayoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilimsikia Mheshimiwa Maige asubuhi na Waheshimiwa Wabunge wengine wamezungumzia barabara inayotuunganisha mikoa mitatu. Nazungumzia barabara ya Busisi kwenda Buyagu – Ngoma A mpaka Nyang’hwale ambalo ni Jimbo lililopo ndani ya Mkoa wa Geita na kuelekea Jimbo la Msalala ambako ni Mkoa wa Shinyanga. Hii ni barabara muhimu na tunaomba Serikali iendelee kujipanga vizuri na sisi tunaikumbusha ili kwamba tunapofika mwaka kesho, basi ama maandalizi yake yawe yameshamilika ama ujenzi uwe umeanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Engineer Nditiye, kwa kazi nzuri aliyofanya alivyotembelea Jimbo la Sengerema kuhusu mawasiliano, ambako bado kuna upungufu, nafahamu kwamba Mheshimiwa Kwandikwa amefika na Mheshimiwa Eng. Kamwelwe kama Waziri amekuwa akipita maeneo mbalimbali pamoja na wasaidizi wake. Pia kwa hili natambua kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Engineer Nditiye alifanya alipofika Jimbo la Sengerema kuhusu maeneo ambayo yana upungufu wa mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Daraja la Kigongo – Busisi, daraja kubwa miongoni mwa madaraja makubwa kabisa katika Bara la Afrika linajengwa pale. Sasa hivi mkandarasi wachambuzi wanaendelea na tathmini ya kumpata kwa sababu tenda imeshafunguliwa. Tunaipongeza Serikali tunasema ahsanteni sana kwa kazi kubwa inayofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengine ambayo nilitaka niyakumbushe, wenzangu wamezungumza. Ukiangalia jiografia ya nchi hii, naomba ATC na ninaamini kwamba wanasikiliza hapa, ile mipango yenu ya kuanzisha route nyingine kutokea hapa Dodoma kwenda Mbeya na kuanzia hapa Dodoma kwenda Mwanza kwa maana ya kuhudumia Mikoa ya Kanda ya Ziwa ifanyike haraka, kwa sababu tunaamini kwamba itarahisisha sana kuokoa rasilimali fedha nyingi inayotumiwa na watumishi wanaokuja hapa kama Makao Makuu ya nchi kwa ajili ya kufanya shughuli za kikazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kuna ujenzi wa meli unaendelea, Ziwa Victoria na maziwa mengine, lakini viwanja vya ndege ikiwemo Kiwanja cha Mwanza, tunasema ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja nataka nizungumze. Tuna miradi mikubwa na ukisoma Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 67 tulipokuwa tunajadili, katika ajira ambazo zimezalishwa mpaka mwezi wa pili mwaka huu tumeambiwa kwamba asilimia 66 imetokana na ajira zilizotokana na uwekezaji wa Serikali kwenye miradi mikubwa, hasa ujenzi wa miundombinu na asilimia 34 imetokea Private Sector.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka niiombe Serikali katika hili, wanaofuatilia mitandaoni, mwezi wa Pili mwishoni pale kulitokea taarifa iliandikwa na mwandishi mmoja akisema asichokijua Mheshimiwa Rais kuhusu ujenzi wa SGR. Alichokuwa anasema ni unyanyaswaji wa Watanzania wanaopata kazi kumsaidia mjenzi mkuu wa miradi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumze hili kwa kina kwamba katika fedha ambazo tunaziingiza katika miradi mikubwa hii, lazima tuwe na utaratibu wa kuwasaidia Wakandarasi wetu wadogo ambao ni subcontractors katika main contractors hawa. Yule mwandishi aliandika akasambaza mitandaoni akataja na jina lake na namba yake ya simu. Mtu mwingine anaweza kusema tusifuate mambo ya mitandao, lakini mtu anapokuwa ameandika na akataja kinachowakera Watanzania, kinachowasibu katika maeneo hayo akaweka na jina lake, ule utayari wake lazima utushtue sisi na liwe ni fundisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Eng. Nditiye, namtaja kama Naibu Waziri kwa sababu nilisikia alifuatilia kwa kile ambacho wananyanyaswa wale subcontractors kwenye ujenzi wa miradi yetu na hasa mradi wa SGR. Wanaingia katika kazi hizo, wanapewa kazi malipo hawalipwi ndani ya muda, matokeo yake wanafilisika kwa sababu wameingia katika ujenzi na wengine wanategemea mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yule bwana mpaka alitaja baadhi ya makampuni. Sasa sitaki kuwa specific nitaje baadhi ya makampuni kwa sababu sina interest yoyote. Ninachotaka niseme, kama Taifa, kwa fedha ambazo tunaziwekeza kwa sababu ni za walipa kodi, lazima tuziandalie utaratibu mzuri wa kuwasaidia Watanzania wenzetu ambao wameingia kule kusaidia. Kwa kadri wanavyonufaika hawa, ndivyo Taifa litakavyokuwa linanufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, chagizo langu ni kuiomba Serikali tuandae utaratibu mzuri wa kusimamia na hasa kuratibu wale subcontractors kwa maana ya local content, wale Watanzania wenyewe hasa ili manufaa haya ya miradi mikubwa tuyaone kwa uhakika na yawe na madhara chanya katika uhai wa uchumi wetu.

Mheshimiwa Niabu Spika, yapo mambo mengi yamekuwa yakizungumzwa hapa. Limezungumzwa deni kuhusu TRC na Serikali kwa ujumla wake na baadhi ya wachangiaji. Mimi sitaki kujibu, lakini ninachotaka kusema, tuwe makini sana. Unapozungumzia deni linaloihusu TRC inawezekana kukawa na deni ambalo linahusu Serikali kwa ujumla kutokana na mkopo ambao tulikopeshwa na Serikali ya Uchina kwa maana ya ujenzi wa Reli ya TAZARA, lakini siyo malimbikizo kwa ujumla wake kwa fedha ambazo zimetajwa hapa kama vile ndiyo zinazostahili kwenda kwa wastaafu au wafanyakazi. Kwa hiyo, naomba nitahadharishe, tuyachambue kwa kina haya tusije tukapeleka taarifa potovu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja na Wanasengerema wajiandae kunufaika na mipango mizuri ya Serikali ambayo imeoneshwa hasa katika ujenzi wa miundombinu ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)