Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa muda huu ili kuchangia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa kutupa uhai leo hii na uzima. Napenda niungane na Watanzania wote kutoa pole kwa kifo cha Mheshimiwa Dkt. Mengi ambaye amesaidia sana makundi mbalimbali ya jamii, natoa pole kwa wananchi wote wa Tanzania, familia yake na wote walioguswa na msiba huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, napenda nitoe pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri Ummy na Makamu wake, Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, kwa kazi nzuri wanazozifanya za kuboresha afya za Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, naomba nitoe pongezi kwa Madaktari wote wa nchi hii ya Tanzania kwa huduma wanazotupatia za kuboresha afya za Watanzania wote, ndiyo maana tunaweza kuja humu Bungeni na tunaweza kufanya kazi zetu kwa sababu ya Madaktari.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, kwa sababu muda ni mdogo, niende moja kwa moja kwenye changamoto. Mkoa wetu wa Katavi baada ya ile changamoto ya kuwatoa Madaktari na Manesi feki, tumekumbwa na tatizo la uhaba wa watumishi. Nimwombe Mheshimiwa Ummy aweze kutupatia Madaktari kule Mkoani kwetu Katavi, atupatie Madaktari Bingwa; hatuna Gynecologist, hatuna Madaktari wa Macho, hatuna Madaktari wa Mifupa, kiasi kwamba mtu akivunjika mguu kule Katavi inabidi asafiri kutoka Katavi mpaka Muhimbili kwenda kufanyiwa matibabu ya mguu. Kwa hiyo niombe sana watakapokuwa wanaajiri Madaktari auangalie Mkoa wetu wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho napenda kukiomba Mkoani kwetu Katavi, naomba kukiombea Kituo cha Afya cha Mamba, naomba akipatie ambulance, kituo hiki kipo umbali wa kilometa 150 kutoka pale Mpanda Mjini na hakina ambulance. Pia nimwombe Mheshimiwa Waziri, kuna kituo cha afya kilikuwa kinajengwa cha Mwamapuli katika Jimbo la Kavuu, naomba akipatie pesa ili kiweze kwisha kwa sababu anafahamu jiografia ya Mkoa wetu wa Katavi, Jimbo la Kavuu liko kiasi cha kilometa 150 kutoka Mpanda kwenda Makao Makuu ya Wilaya, kwa hiyo naomba akiangalie kituo hiki cha afya. Niombe pia vitendeakazi kama x-ray na ultra sound kwa vituo vya afya vyote vya Mkoani kwetu Katavi kwa sababu viko mbali sana na Makao Makuu ya Wilaya, umbali wa kilometa 150. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho napenda kuzungumzia, nimwombe Mheshimiwa Ummy, iko Sera ya Wazee ambayo Serikali ilipitisha toka mwaka 2003, niombe sasa alete Sheria ya Wazee kwa sababu Sera ya Wazee imekaa umri wa miaka 15, lakini hakuna Sheria ya Wazee, sasa sera ikikaa hivihivi kama sera inaweza siku nyingine Serikali ikaamua tu kwamba inafuta ile Sera ya Wazee lakini ikiwa ndani ya sheria wazee watakuwa protected zaidi. (Makofi

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho ninakiomba ni kuhusu kuajiri hii Sekta ya Afya upande wa Community Health Service. Hawa watu ni muhimu sana kwa sababu wao wanakwenda deep kwenye kaya, ina maana wana uwezo wa kwenda nyumba kwa nyumba kwenda kufundisha mambo ya afya. Ukiangalia kwamba mara nyingi nchi yetu huwa tunapata matatizo ya kipindipindu, ni kwa sababu tuna uhaba wa hawa Maafisa Afya Jamii. Hawa ni muhimu sana kwa sababu wao wanakwenda kwenye kijiji, wanaweza kufundisha umuhimu wa kutumia vyoo, umuhimu wa kunawa mikono kabla ya kula, hii yote itasaidia wananchi wa Tanzania wasiweze kupata magojwa ambukizi. Kwa hiyo, niombe waweze kuajiri hawa Maafisa Afya Jamii kwa manufaa ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia, Mheshimiwa Ummy katika Sekta ya Afya amefanya vizuri sana upande wa madawa, upande wa kujenga hospitali, upande wa kujenga vituo vya afya, lakini upande wa wanawake nimwombe kabla hajaondoka aweke legacy kwa wanawake, aangalie sheria ambazo zinamkandamiza mwanamke, zije humu Bungeni zibadilishwe. Nafikiri hiki ndicho kitakachomfanya aweke historia kwa wanawake, Sheria kama ya Ndoa ya Mwaka 1971, kipengele cha 13 ambacho kimekuwa kigugumizi katika nchi hii kubadilisha umri wa mtoto wa kike kuolewa na mtoto wa kiume kuoa, aweke legacy kwa kubadilisha sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo sheria nyingine pia ambazo ni kandamizi kwa wanawake. Kwa mfano, ipo GN ya mwaka 1963 ambayo ina vipengele vingi sana vinamkandamiza mwanamke. GN hii bado inatumika na nashangaa sana hata kuna kesi ambayo ilishatolewa kwamba GN hii ifutwe, lakini bado nimeona kwamba ni kigugumizi sana kufuta GN hii. Haiwezekani utumie GN ya mwaka 1963 kwa wanawake wa Tanzania ambayo inawabagua sana katika mambo ya mirathi, inawabagua sana katika kutumia ardhi mume wako akifa na pia ina kipengele ambacho kinasema kwamba mwanamke akifiwa na mume wake arithiwe na mdogo wake na akikataa atoke katika ukoo huo. Nimuombe sana afuatilie hizi sheria zote azilete hapa na atakuwa ameweka legacy. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, GN hiyohiyo pia inamtambua mtoto wa kiume kwamba ndio mrithi halali, wanamwita principal heir, lakini haimtambui mtoto wa kike kwamba ni mrithi wa mali za baba yake. Nimwombe Mheshimiwa Waziri basi aweke legacy kwa kubadilisha sheria hizi ambazo ni mbovu, zinamnyanyasa mtoto wa kike ili tutakapoondoka katika Bunge hili, basi akinamama waseme tulikuwa na Waziri mwanamke ambaye pia alishughulikia masuala ya wanawake. (Makofi)