Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Alfredina Apolinary Kahigi

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia Wizara ya Maji, hoja ambayo iko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea na mchango wangu, namshukuru Mheshimiwa Waziri Mbarawa; Naibu wake, Mheshimiwa Aweso kijana wangu, kwa kazi ambayo wanaifanya, tunaiona. Nisiwe mwizi wa fadhila, wanafanya kazi usiku na mchana, tunaona wanakimbizana, Mungu awabariki sana na Mungu azidi kuwatia nguvu. Ni lazima nimsifie (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge ninayetoka Mkoa wa Kagera, Kanda ya Ziwa. Mkoa wa Kagera tuna Majimbo mengi ambayo yanapakana na Ziwa Victoria. Ziwa Victoria tuna Wilaya nyingi ambazo zina upungufu wa maji. Kwa mfano, Wilaya ya Bukoba Vijijini, Wilaya ya Muleba Kaskazini na Kusini, Wilaya ya Misenyi; kuna baadhi ya kata ambazo zina matatizo ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha kiangazi ambacho tunaelekea mito inakauka, wanawake wanapata shida kubwa sana ya kupata maji. Pamoja na kwamba Ziwa Victoria, liko sehemu nyingi sana limetambaa Mkoa wa Kagera, lakini kijiografia tuko juu ya Ziwa Victoria. Kata nyingine ziko juu ya Victoria. Naiomba Serikali iwasaidie wananchi wa Kagera ambao wako juu ya milima waweze kuwapatia maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, ninaomba Serikali iweke mkazo, wananchi ambao wanalima kwenye vyanzo vya mito, wanaokata miti ovyo ovyo na kuchoma miti, wakatazwe kabisa wasifanye vitu hivyo, ndivyo vinavyopelekea tukakosa maji kwa wingi. Zamani mito ilikuwa inatiririsha maji vizuri, lakini sasa hivi inakauka, ni kwa sababu ya matatizo hayo. Serikali iwekee mkazo jambo hilo kusudi waache kukata miti na kulima kwenye vyanzo vya mito. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, naiomba Serikali, kwa wale ambao wamejaliwa kujenga nyumba ambazo zina mabati, ni vizuri wakavuna maji ya mvua, wajenge matanki ya saruji madogo madogo, kwa watu wale ambao wanajiweza ili maji yale ambayo yanapotea kwenye ardhi yaweze kuwasaidia wakati wa kiangazi, itakuwa ni jambo zuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile na maji yale ambayo yanapotelea kwenye ardhi, kama watu wangekuwa wanayavuna, mito mingine kipindi cha mvua isingekuwa inafurika na madaraja kuvunjika. Huenda ingekuwa inasaidia na yenyewe kwa ajili ya kuyavuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine naomba, kuna mradi wa Wilaya ya Karagwe, huo mradi ulianza mwaka 2005, ndipo ulipozinduliwa, mradi wa Lwakajunju. Mwaka 2010 upembuzi yakinifu ulikamilisha jambo hilo, mwaka 2018, Mheshimiwa Rais alipokuja kufungua barabara ya Kyaka Bugene, alisema kwamba shilingi bilioni 70 tayari zimeshatoka kwa wafadhili, huo mradi unapaswa kuanzishwa. Mpaka leo hii ninaposema, hakuna kitu ambacho kimeshafanyika. Mheshimiwa Waziri ninaongea na wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, alisema kwamba huo mradi uanze, maana shilingi bilioni 70 tayari zimeshatoka kwa wafadhili India, lakini mpaka leo hii huo mradi haujaanzishwa na wananchi wa Karagwe, wanapata shida sana ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Karagwe wana milima mirefu, wanawake wanafuata maji kwenye mabonde, wanapata shida sana. Naomba Mheshimiwa Waziri akija ku- wind-up atuambie huo mradi unaanza lini? Maana umekuwa mradi, mradi, ngonjera, ngonjera, wananchi wa Karagwe wanawake wameota vipara wanapata shida. Naomba Mheshimiwa Waziri anipe jibu ambalo liko sahihi, maana wamenituma nije nisemee hilo jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nilitaka kusema, ni kuhusu…, aah, yameniishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)