Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Eng. Christopher Kajoro Chizza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika hoja hii ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wa Wizara hii ambayo nami niliwahi kuitumikia kwa kuleta hotuba nzuri ambayo inatuelekeza tuchukue mwelekeo gani ili kuweza kuwafikishia wananchi wetu maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua bado ziko changamoto nyingi, najua yako malengo mengi ambayo hatujayafikia, lakini hatuwezi kuyafikia bila kuwa na utaratibu ambao tumejiwekea. Kwa sababu hii, naanza moja kwa moja kuunga mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri, kwa sababu hata kama sijaunga mkono, haitatusaidia sisi kueleza ule upungufu ili akaufanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naunga mkono kabisa kwa asilimia mia moja ili niweze kusema mambo yangu sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa na Mheshimiwa Waziri mwenyewe kwa sababu kwa nyakati tofauti Waheshimiwa hawa wamefika katika Wilaya yangu ya Kakonko, wakakagua miradi ya maji ambayo ni kero kubwa, miradi ambayo haijakamilika tangu miaka karibu kumi iliyopita na kwa nyakati tofauti wakatoa maelekezo ni hatua gani zifanyike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua nimepitia kwenye kitabu hiki, nimekuja leo tu, sikuwepo kwa muda mrefu kwa sababu zisizozuilika, baadhi ya mambo nimeona yametekelezwa, lakini yako mengine ambayo hayakutekelezwa; na hayo ndiyo nataka angalau nizungumze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri mara kadhaa anapojibu maswali anasema vizuri sana kwamba maji ni uhai, maji hayana mbadala na huo ni ukweli. Mahali ambako hakuna maji hakuna uhai, hata watu wanaokwenda mwezini huko au katika sayari zingine wanaridhika kabisa kwamba kule hawajaona maji na kwa kuwa hakuna maji hata viumbe hai havionekani. Kwa hiyo Mheshimiwa Aweso anachosema ni kweli kabisa kwamba maji hayana mbadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sera yetu ya Maji, nakumbuka vizuri nadhani ilikuwa mwaka 2002 na mimi nilishiriki, tulikwenda mpaka Zimbabwe mpaka South Afrika tukajiwekea malengo kwamba ifikapo Mei, 2010 upatikanaji wa maji mijini miaka ile ungekuwa asilimia 90, upatikanaji wa maji vijijini mwaka ule ungekuwa asilimia 65. Najua bado ziko changamoto nyingi, kila unapokwenda sasa hivi kilio ni maji, maji, maji. Upatikanaji wa maji Wabunge wengi wamezungumza, mimi sikuwepo lakini nilikuwa nafuatilia angalau kwa vyombo vya habari, upatikanji wa maji bado hatujafikia malengo, bado hali ni tete. Kwa mfano katika Halmashauri ya Kakonko, idadi ya vituo vya maji ni 576, vituo visivyofanya kazi 283, ukokotoaji wa upatikanaji wa maji inasemekana ni asilimia 52 au 53 kulingana na taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nafuatilia wakati mwingine huu ukokotoaji wa upatikanji wa maji na naomba Mheshimiwa Waziri nimefuatilia nikagundua wakati mwingine ukokotoaji hauendani na hali halisi, kwa sababu kwa mfano nilimuuliza Mhandisi mmoja unakokotoaje upatikanaji wa maji ukapata percentage? Akaniambia naangalia visima vilivyopo huenda vinafanya kazi au havifanyi kazi yeye anahesabu visima vilivyopo. Anaangalia kisima kimoja kinatoa maji kiasi gani, per capita onsumption ya maji vijijini na mijini ni kiasi gani? Sasa yeye anajumlisha anasema upatikanaji wa maji kulingana na visima vya maji vilivyopo kulingana na vyanzo vya maji ni huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili naomba lisahihishwe kwa sababu huo si ukokotoaji halisi, huo ni ukokotyoaji ambao unajumuisha vyanzo vinavyotoa maji, vyanzo vya maji ambavyo miradi bado haijaanza kufanya kazi au imekamilishwa lakini haitoi maji, lakini akikokotoa anasema tumepata asilimia kadhaa. Haitusaidii sana kwenda namna hii, ni bora kabisa kwenda na hali halisi ili tunapokuja sasa kuiomba Serikali twende tukiwa na takwimu halisi, ni afadhali tuwe na miradi michache inayotekelezwa mara moja na kutoa maji, halafu tukimaliza tunahamia kwenye miradi mingine kidogo kidogo hivyo kuliko kujiwekea malengo au takwimu ambazo hazitoi hali halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri upatikanaji wa maji katika Wilaya yangu ya Kakonko bado sidhani kama ni asilimia hii. Mheshimiwa Waziri alipokuja mwenyewe nilimpeleka akaona alitembelea baadhi ya miradi akaona mahali ambako miradi mingine walimwambia imetekelezwa kumbe iko asilimia tano, pale Kakonko Mjini aliona mwenyewe, tulikwenda katika miradi mingine Gwijima, tukaenda Kiduduye, Miradi ya Muhange, Katonga, Kiga, Gwalungu, Nyeguye, yote hiyo ama haifanyi kazi au imetekelezwa kwa kiwango ambacho hakistahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ziko wazi kwa nini baadhi ya miradi haitekelezwi vizuri. Naomba ku-declare interest mimi ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC, nimepata nafasi kupitia miradi mingi hasa ya ujenzi, barabara, shule, maji, changamoto kubwa ambazo niliziona na hizi ndizo nataka nizisemee halafu niketi, lakini Mheshimiwa Waziri azifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ambayo nimeiona katika miradi yetu ya maji, Mheshimiwa Waziri amesema tuna uwezo wa kitaasisi katika mikoa, katika mabonde ya maji na katika halmashauri na nimesoma katika kitabu chake ukurasa nadhani wa 12, lakini hali halisi kwa kweli bado bado hasa katika halmashauri, bado uwezo wa kitaasisi ni mdogo na uwezo huu naupima. Mimi nimekuwa katika Kamati ya LAAC tunachokifanya, tunatazama kwanza taarifa za CAG, halafu tuna- single out miradi fulani Fulani, unaikagua. Tulichokibaini na wenzangu akina Mheshimiwa Mwalongo na Waheshimiwa wengine bila shaka watakubaliana na mimi, tulichokibaini ni uwezo mdogo kwanza katika mchakato mzima wa kutoa zabuni hizi, zabuni hizi zinatolewa kwa wakandarasi, baadhi ya wakandarasi wasio na sifa hawana…