Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nami naomba nianze kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi kubwa ambazo zinafanyika katika kukabiliana na tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamezungumza kwamba tatizo la maji kwa sasa lilivyo ni tatizo kubwa sana ambalo naiomba sana Serikali yangu ilitazame kwa mtazamo tofauti. Ni janga ambalo kwa kweli karibia kila mahali kuna kilio kikubwa na jitihada zisipofanyika tukaendelea na mwendo huu tulionao, naamini kila wakati tutaendelea kupokea malalamiko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinadharia Jimbo la Msalala kama miradi yote ambayo imepangwa na Serikali kutekelezwa na kama ikitekelezwa katika muda tuliopanga wa kufikia 2020, Jimbo letu litakuwa limebakiza Kata mbili tu ambazo hazina maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali hasa kuanzia Awamu hii ya Tano lakini pia hata Awamu ya Nne kuna baadhi ya miradi mikubwa ilianza kutekelezwa. Kwa kutaja tu baadhi ya miradi, ukurasa ule wa 31 Mheshimiwa Waziri amezungumzia mradi wa maji wa Ziwa Victoria ambao kwa sasa uko kwenye awamu ya pili ya utekelezaji unaogusa vijiji 100 na Jimbo la Msalala lina vijiji vyake kadhaa ambao unaendelea kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi mwingine mkubwa sana wa zaidi ya shilingi bilioni 15 unaotekelezwa kwa ubia kati ya mgodi wa Bulyanhulu (Acacia) pamoja na Serikali yetu. Unatoa maji Mhangu hadi Kijiji cha Ilogi kwenye Kata ya Bugarama. Kuna mradi mwingine mkubwa tu na wenyewe wenye zaidi ya shilingi bilioni 24 ambao unapeleka maji kwenye Mji wa Kagongwa na Isaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii yote ikitekelezwa; na yote ina sura ya awamu. Kwa mfano, mradi wa Isaka na Kagongwa una awamu mbili, mradi wa Mangu, Ilogi na wenyewe una awamu mbili; na miradi hii ikitekelezwa kwa ukamilifu, itaweza kutatua tatizo la maji tulilonalo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali ifanye juhudi za kutafuta ufumbuzi. Bahati nzuri wazo la kutafuta ufumbuzi au jibu la tatizo tulilonalo limeshatolewa na Waheshimiwa Wabunge hapa. Ukiangalia miradi yote inashindwa kukamilika mapema kwa sababu ya upatikanaji wa fedha ama fedha zinapopatikana kidogo zinakuwa ni zile ambazo ni za mfuko wa maji peke yake, zile za Bajeti Kuu na za wafadhili hazipatikani kwa wakati. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wameshapendekeza hapa, nami niungane nao na niseme tu kwa sababu ni jambo ambalo tulishaliamua hapa, ni vizuri sana Serikali ikakubaliana na ombi letu la kwamba angalau tuongeze tozo kwenye mafuta ili tuweze kutatua tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii niliyoitaja kinadharia ukiisikiliza ni mizuri sana, lakini miradi karibu yote utekelezaji wake uko kwenye viwango tofauti tofauti hakuna ambao uko zaidi ya asilimia 80 na hapo ndiyo tatizo kubwa linapoanzia. Nikianza kwa mfano na ule Mradi wa Vijiji 100; mradi huu tuliuibua hapa Bungeni mwaka 2014, Waziri wa Maji akiwa Profesa Maghembe, tukasema vijiji 100 vilivyoko pembezoni mwa bomba kuu la kutoka Ziwa Victoria hadi Shinyanga vipatiwe maji, Jimbo la Msalala lilikuwa na vijiji 16 katika orodha ya vijiji 100. Mpaka tunavyozungumza hivi sasa vijiji ambavyo vimepatiwa maji ni vijiji vitano tu, kwa hiyo bado vijiji tisa toka mwaka 2014 havijapata maji, hili ni tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mradi wa pili niliousema wa kutoa maji Mangu hadi Ilogi kupitia Wilaya ya Nyang’hwale pamoja na Wilaya ya Msalala, naishukuru sana Serikali na hasa Mheshimiwa Waziri, Naibu wake pamoja na Katibu Mkuu wote wawili Katibu Mkuu mwenyewe Profesa Mkumbo na Engineer Kalobelo wameusukuma sana mradi huu hadi kufika hatua hii ya kuanza kutekelezwa. Tuliubuni namgodi wa Acacia mwaka 2012 na toka 2012 hadi mwaka 2014/2015, hakuna utekelezaji uliofanyika, lakini 2016, baada ya Serikali hii kuingia madarakani ikatoa fedha na mradi umeanza kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa uko asilimia chini ya 50 na lengo lilikuwa kufika Desemba, 2018 bomba Kuu la kutoka Mangu hadi Ilogi liwe limewekwa, hivi sasa halijakamilika. Awamu ya pili ambayo ni kusambaza maji kwenye vijiji vilivyo jirani na yenyewe haijaanza. Naiomba sana Serikali ikubali hili ombi la kuongeza fedha kwenye Mfuko wa Maji ili fedha hizo ziweze kutekeleza awamu ya pili ya kupeleka maji kwenye vijiji ambavyo vipo pembezoni mwa hilo bomba kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Kagongwana Isaka na wenyewe tulisema uwe na awamu mbili, awamu ya kwanza ni ile ya kupeleka bomba kuu na kusambaza maji pale Kagongwa na Isaka penyewe, lakini kuna kata tatu ambazo ziko pembezoni ndani ya kilomita 12 zinapitiwa na bomba hilo;Kata ya Mwalugulu,Kata ya Mwakatapamoja na Kata ya Isaka na Kata ya Jana. Vijiji hivi tunaenda kutengeneza matatizo, wanaona maji yanapita kwenda kwa wenzao wa Isaka wao hawapati maji. Tulisema hii ni awamu ya kwanza, vumilieni hadi kufika 2020 wananchi hawa watakuwa wameanza kuona na wenyewe wakitekelezewa mradi huu. Naiomba Serikali yangu wakubali hili ombi ili awamu ya pili ya kupeleka maji katika vijiji vilivyoko pembezoni mwa hilo bomba kuu uweze kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulibahatika pia kupata ule mradi wa mkopo wa Benki ya Dunia vijiji 10 kila Wilaya. Halmashauri ya Msalala tuna Kijiji kimoja cha Segese kinadai shilingi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango mzuri sana.

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, kwa hiyo naomba tu Kijiji cha Segese kinadai milioni 30 ya kufunga pampu, milioni 700 zimewekwa pale, lakini mradi haufanyi kazi. Tunaomba Serikali isaidie ombi hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja nanashukuru sana kwa nafasi.(Makofi)