Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia machache kuhusu hoja iliyo mbele yetu ya bajeti ya Wizara ya Maji. Mimi ni mjumbe wa LAAC, kwa hiyo, tunapata nafasi kubwa ya kutembelea miradi mbalimbali ili tuweze kuona utekelezaji wake lakini pia na thamani ya fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi kuna mtu mmoja alichangia kwa jazba akasema kuna mambo ya hovyo hovyo yanatendeka katika miradi hii ya Wizara ya Maji. Mimi labda nisitumie neno hilo, niseme katika miradi ya maji kuna mambo makubwa sana ya usanii na Mawaziri ninyi hamuwezi kufika kila mahali, kwa hiyo, tunapotoa mawazo yetu, hatuna maana kwamba tunawachukia au tunafanya mambo ya kisiasa hapa, tunatembea tunaona ni namna gani miradi ya maji inavyotekelezwa ndivyo sivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi labda niulize, kuna nini kati ya Wizara ya Fedha, Wizara ya Maji na Halmashauri zetu? Hii miradi ya nyuma yote ilikuwa ina-originate Wizarani. Ina maana Wizara walikuwa wanatoa Mhandisi Mshauri, Mkandarasi, kule Halmashauri wala hawakuwa answerable na miradi hii. Walichokuwa wanafanya Wizara ya Maji wanaleta Mhandisi Mshauri ambaye anakuja kufanya uoembuzi yakinifu ambavyo sivyo. Matokeo yake atasema hapa kuna maji, halafu yule anayekuja kuchimba maji anakuta hayapo, ameshakula fedha ameondoka na miradi mingi sana ya maji ina fedha nyingi, ni ya mabilioni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa ya mwaka ya LAAC tulipendekeza kama alivyosema Mheshimiwa aliyemaliza hapa kwamba iundwe Tume iende itazame miradi hii, iangalie ni miradi gani ambayo haikufanyika kwa ufanisi lakini pia mjue gharama zilizotumika. Inawezekana hamna ukakika hata wa gharama zilizotumika katika miradi hii. Ni jambo la kusikitisha kwa sababu Watanzania wanalipa madeni ya miradi ambayo haina ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitembelea miradi, hawa watu wa Idara ya Maji, wakishapata taarifa kwa mfano Kamati ya LAAC inakuja maji yanatoka kesho yake. Tukifika, wananchi wanatuambia Waheshimiwa Wabunge mmekuja na maji na mtarudi nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko miradi mingi ambayo imetengenezwa haifuati hata BOQs. Kwa mfano, tumekwenda katika mradi mmoja huko Ngara, tumekuta wametengeneza tenki ambalo BOQ inasema watatumia matofari ya block, wao wametumia mawe na wamejenga tenki ambalo walipoweka maji likanza kuvuja. Halafu mtu anakwambia mradi umekamilika. Miradi ya namna hiyo ni mingi sana katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe mchunguze miradi hii, acha hii miradi mipya ambayo inatengenezwa sasa hivi, hii miradi ya nyuma yote imekaa hovyo hovyo. Wananchi hawapati maji ni uongo na Wahandisi wanadanganya na mahali pengine hata Wahandisi wenyewe ambao kwa kweli wana ujuzi wa kuendesha miradi hii hawapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakwenda mahali pengine unakuta wametengeneza miradi chini ya viwango, anaweka mabomba ambayo ni tofauti. Mimi siyo mtaalamu wa mabomba ya maji lakini wataweka mabomba membamba, wakipampu maji mabomba yote yanapasuka. Kwa hiyo, hiyo ndiyo hali halisi iliyoko on the ground. Kwa hiyo, tunaomba mhakikishe mnachunguza miradi hii kama Kamati ya LAAC tulivyopendekeza na wengine ndani ya Bunge from there mtaweza kuona ni miradi ipi inakwenda vizuri, ipi ambayo imetengenezwa kiusanii na gharama ni ipi, muweze kutambua kwama nchi hii imeingia katika ufisadi mkubwa kwa kupitia miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana labda Serikali haina vipaumbele, nawaomba tuhakikishe maji tunayaweka katika priority. Watanzania wanateseka, inawezekana sisi tunakaa mijini, mkienda kule vijijini mtaona watu wanavyo- suffer kusema ukweli, utawahurumia watu hawaogi. Wanawake wanalalamika, maisha hayaendi vizurio ndani ya familia, kama hamuogi mnakaaje? Hili jambo ni serious, tunaomba Waziri na Serikali ihakikishe maji ambayo watu wamesema maneno mengi, ni uhai na kadhalika kwamba miradi yote inatekelezwa na wananchi wa Tanzania wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niongelee kuhusu vyanzo vya maji vijijini. Nina uhakika kwamba Serikali haiwezi ku-supply maji kwa kila mtu Tanzania hii lakini iko mito ambayo ni vyanzo vya maji ambapo kutokana na shughuli za binadamu imekufa. Kwa mfano, katika mkoa wetu sisi yako maeneo mengi watu wanapanda miti na wengine ni wanasiasa, wanapanda miti wanaharibu vyanzo vya maji, kwa hiyo, huwezi kupata mito ambayo inatoa maji mazuri. Kwa mfano, Mkoa wa Kagera, tunayo mito mizuri ambayo inatoa maji mazuri, lakini yote imekufa. Kwa hiyo, pamoja na kwamba wanaoangalia vyanzo vya maji ni watu wa mazingira, tunaomba na Wizara ya Maji isaidiane na Wizara hiyo pamoja na TAMISEMI kuhakikisha kwamba vyanzo vya maji na mito zile chemichemi zinalindwa ili kuweza kusaidia watu wa vijijini ambao inawezekana wasipate huduma ya maji ya bomba ambayo tunaiongelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la kuongeza fedha katika mafuta. Ni kweli tulipitisha miaka mitatu na mimi naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Chenge, hatukatai kukata hiyo shilingi 50, je, implementation yake itakuwaje? Hata za REA haziendi zote. Kama miradi ya REA fedha mnaziweka kwenye Mfuko Mkuu mnafanya mnavyotaka, maana Serikali hii ya CCM sasa hivi hata bajeti hamuiheshimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapitisha bajeti hapa, tunatengeneza na sheria zile zinazofuata pale za kutekeleza bajeti lakini hata wakati mwingine haifuatwi.

WABUNGE FULANI: Wakati wote.

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Wanasema ni wakati wote. Kuna miradi mikubwa mingine hatusemi ni mibaya, lakini je ilikuwa katika bajeti na kama inakomba fedha zote, zile fedha ambazo zingeweza kuhudumia jamii ya Watanzania zitatoka wapi. Je, mnatuhakikishiaje kwamba zile fedha zitakuwa kwenye mfuko wake ili wananchi waweze kupata maji. Maana Watanzania wanapojitolea kukatwa shilingi 50, ujue kwamba unawaongezea na gharama nyingine. Watakatwa ya maji, wanakatwa ya umeme, wanapenda kuleta maendeleo yao lakini fedha zitapelekwa kule ili miradi iweze kutekelezeka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi sipingani na hilo lakini lazima kama Wabunge tuhakikishe kwamba hizi fedha zinakwenda kutekeleza jambo ambalo sisi tumelipanga hapa. Sasa Serikali imekuwa haiheshimu Wabunge na Bunge na sisi Bunge tumekuwa na kauli za naomba, jicho la huruma, jicho la huruma gani, we want the government to do it! Tunaitaka Serikali itekeleze miradi hiyo kwa sababu tunalipa kodi na kodi zinakusanywa, hatuwezi kukaa kubembelezabembeleza jicho la huruma, jicho gani, Serikali tunaiombaomba, tunaomba jicho la huruma, ndiyo maana wanatufanyia haya. Tuwaambie we want the government to do this, tunakutaka Waziri Prof. Mbawala utupe maji, siyo tunakuomba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema haya kwa sababu maji yanaumiza na mnatulipia fedha za walipa kodi tunakwenda seriously. Watu wanakwenda kule, wengine wanavaa hata kabtula kupanda milima, unakuta miradi ya maji mpembuzi yakinifu pampu anaweka kule korogoni ambako anajua Mbunge hata wewe Mheshimiwa Jenista ukipanda kule ukitoka unakufa kwa sababu kupanda ile milima watu wengine mpaka wasukumwe. Pampu iko korongoni halafu maji yanakwenda mlimani, yanatoka mlimani yanashuka, hayo ndiyo mambo mnayotufanyia. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)