Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa hii nafasi na naungana na waliozungumza asubuhi na maombi aliyotoa jirani yangu Mheshimiwa Mchungaji Getrude Rwakatare kumwombea ndugu Reginald Mengi apumzike mahali pema peponi. Amina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa jioni ya leo na ndio mchango wangu wa kwanza kwenye bajeti na nilikuwa naisubiri sana hii Wizara ya Maji kwa sababu nikiwa kama mwakilishi wa wanawake maji ni kila kitu kwa mwanamke yeyote. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Profesa Makame Mbarawa, Naibu Waziri mwanangu Mheshimiwa Aweso, timu yote ya wanamaji maana yake wao wanafamilia ya maji kutoka wizarani mpaka mikoani, niwapongeze kwa juhudi zao kwa kipindi chote kuhakikisha kwamba maji yanapatikana. Kipekee niwapongeze wanawake wote, wanawake wa Tanzania wasiochoka kuhakikisha maji yanapatikana, kulea familia zao, kutunza familia zao, wakiwemo wa mjini na vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika Mungu ni mwema naye leo ametupa uhai tukaweza kuzungumza haya mambo hapa nami nimrudishie sifa na utukufu Mwenyezi Mungu nikiamini kwamba atatupatia maji mengi zaidi Tanzania. Niseme kwamba ni vyema basi kama tunaamini hivyo na tumeipokea hii ripoti nzuri maana yake hii ripoti kwa kweli inatiririka kama kitabu cha hadithi, niseme kwamba hakuna litakaloshindikana kwenye ripoti hii ila tu Serikali nayo isikie na ili nisikose muda wa kukamilisha azma yangu naomba kuunga mkono hotuba hii kwa aslimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, takribani ni mwaka wa nne sasa toka nimeingia kwenye Bunge hili la Kumi na Moja, nimewakuta Wabunge waliokuwa wametangulia wanazungumzia Sh.50 nyingine ya maji ambazo zimekuwa ring fence ambazo zimefanya kazi kubwa na leo kwa hiari yao wenyewe wanaomba tena Sh.50 ziongezwe, labda chanzo cha mafuta ni kigumu sana kwamba vitu vitapanda bei, lakini Wabunge sisi ndio wawakilishi tumekuja na chanzo kingine tumesema kwamba basi ikatwe kwenye bundle za simu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiari yashinda utumwa, kwa hiari yao na watajua namna ya kuongea na wawakilishi ili kila mtu apate maji safi na salama ambayo ni haki yake. Mungu alitupa maji tunafurahi kabisa. Nimesoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri toka ule ukurasa wa 12 mpaka wa 22 ambapo ukurasa huo wa 12 anazungumzia usimamizi na uendeshaji wa rasilimali za maji, akizungumzia mabonde ya maji, vyanzo mbalimbali na management ya maji, lakini sikuona msisitizo kwenye maji yanayotoka angani. Tanzania inaelekea kupata athari kubwa kwa ajili ya tabia nchi na zikianza mvua zinaanza kwa kasi kama zile za juzi zilizoharibu miundombinu ya barabara au watu walishindwa kupita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niulize tu wasomi wetu wako wapi? Hayo maji yanayotiririka na kupotea ardhini na kurudi tena baharini wamejipanga vipi kuhakikisha tunayakinga. Hivi majuzi Wabunge wote walikwenda kule kwenye mji mpya Ihumwa, sijui yale majengo kama yana makinga maji, mimi nilibahatika pia kwenda na Kamati ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama na tukahoji hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaalamu wa ku-reserve rain water ni mdogo sana. Miaka hiyo nikisoma Kifungilo tulikuwa na rain water na ndio maji safi na salama. Sasa wamejipanga vipi pale Ihumwa kuwa na maji mengi maana yake zikija mvua za Dodoma ni nyingi sana kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia sasa eneo ambalo mimi nashiriki kama Diwani ambapo ni kule Siha. Siha kuna shida ya maji, pia tambarare yote ya Kilimanjaro, wengi waliniambia wewe unachangia nini na Kilimanjaro maji bwerere. Nataka niwaambie hivi kuna maeneo ambayo hayajaona maji safi na salama ikiwepo Same, Mwanga, Rombo na huko Siha, maji safi na salama ni shida. Alipokuja Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye namshukuru sana aliona wote walikuwa wanamwomba maji safi na salama naye alisema jambo hili ataliwekea mkazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi Mamlaka za Maji zina mafanikio makubwa na best practice zinaonekana, successful cases zimeonekana ikiwemo Mamlaka ya Maji MUWSA inayoongozwa na Joyce Msiru binti aliyekubuhu kabisa katika nyanja ya maji na anaipeleka vizuri. Sio hayo tu Dodoma yenyewe hatuna shida ya maji na Dar es Salaam pia niwapongeze sana Wakurugenzi hao na wale wengine. Siha kuna shida moja tu MUWSA ilipopelekwa kwenda kusimamia sasa management maana yake shida ni management na mpaka sasa hivi kwa kipindi kifupi sana tumepata Siha bilioni 4.3, naishukuru Serikali. Hata hivyo, ile bilioni ya kwanza bilioni 1.8 ya mwaka 2016 iliyojenga yale matenki ni kama imepotea maana yake yale matenki sasa hayatoi maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu ambaye nimempongeza sana awali katika ile timu, waone sasa kwamba hawa wenzetu wa MUWSA watakapofika kule Hai wasisikilize hiyo ya kwamba haitawezekana, maana yake zimetokea tuhuma nyingi, hapa sio mahali pake lakini waendelee kusimamia ili maji hayo yaweze sasa kutumika kwa wingi na kusambazwa katika maeneo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiomba fomu ya kuomba maji kule Siha ni Sh.345,000 ambapo MUWSA ni Sh.20,000 tu. Sasa nashindwa kuelewa kwa nini wale wananchi wanashindwa kukubali, labda hapa pamepungua elimu. Nawaomba sana MUWSA itoe elimu na Katibu Mkuu asimamie jambo hili kwa sababu wanaoteseka ni wale wanawake wa kule mbali. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)