Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Godfrey William Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi, kwanza niishukuru sana Wizara ya Maji nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, nimshukuru sana Naibu Waziri, nimshukuru sana, Katibu Mkuu kwa nzuri wanayoifanya kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ya maji katika Majimbo yetu na katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitapenda sana kuanza na mambo matatu ya muhimu sana, jambo la kwanza nitaenda kwenye mapendekezo ya Kamati, mapendekezo ya Kamati yako mengi, lakini nitazungumza mapendekezo matatu ambayo ningependa sana Wizara iweze kuyasisitiza na kuyaangalia kwa jicho la kipekee, ili tuweze kutatua tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza katika ukurasa wa 18, katika ripoti ya Kamati, imeelezea na imeshangazwa na kushuka kwa kiwango cha bajeti cha asilimia 9 katika kipindi cha bajeti cha mwaka 2019/2020 ukilinganisha na 2018/2019. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ikiwa kama tuna malengo mazuri ya kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ya maji, naungana na Kamati kuuliza swali hili, hivi kwa nini kama tuna malengo ya kutatua tatizo la maji katika nchi yetu ya Tanzania bajeti ipungue kwa asilimia 9? Lakini jambo la pili ninaenda tena kwenye ukurasa wa 19 ambapo unasema inazungumzia masuala mazima ya mfuko wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba mwaka uliopita tulizungumza na miaka mitatu sasa mfululizo tumekuwa tukiendelea kuishauri Serikali kuongeza tozo kutoka shilingi 50 mpaka shilingi 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika kipindi cha miaka mitatu yote, bado hakuna lolote ambalo limefanyika, na kwa kweli kwa sisi Wabunge ambao hasa tunatoka kule vijijini. Tunajua adha ya maji, changamoto kubwa ambayo ipo vijijini ni suala zima la maji, ukienda kule hawaongelei kitu kingine zaidi ya maji, na hata sisi ambao tuko mjini huku wakati tukiwa Dodoma, kitu kikubwa ni maji. Sio kitu kingine, ni maji, utaenda mjini maji, utaenda vijijini maji, sehemu yoyote utakayoenda Tanzania hapa, tatizo ni maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachouliza hivi ni kwa nini Serikali inashindwa kusikiliza na kuamua tu sasa tufanye utaratibu wa kuwa na shilingi 100 badala ya shilingi 50. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nadhani peke yake itaweza kutatua changamoto hii kubwa sana, kwa sababu kwa asilimia kubwa mfuko wa maji, umechangia kwa asilimia 67 ambao unalipa pamoja na mengineyo unalipa wakandarasi, na unasaidia kuendelea kuwa na vyanzo mbalimbali vya maji. Kwa hiyo, ikiwa kama tutaongeza shilingi 50 kwenda 100 basi nadhani changamoto ya maji tunaweza tukaipunguza kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukiangalia ukilinganisha kati ya vyanzo vya mapato ya ndani na hii tozo, utaona kwamba asilimia kubwa ya vyanzo vya ndani havikidhi mahitaji na ndipo hapo utakapoona kwamba asilimia saba ya vyanzo vya ndani vya mapato ndivyo vilivyokidhi mahitaji, lakini kwa asilimia kubwa, asilimia 67 imetokana na changamoto ambayo tumejaribu kuweka tozo ya shilingi 50. Nilikuwa nadhani ni wakati sasa umefika 2019 tuweze kuweka mguu chini, tuweze kuishauri Serikali na Serikali isikilize maoni yetu kama Wabunge kwa sababu tunatoka vijijini tunajua changamoto na tatizo kubwa kule vijijini ni maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine au kitu kingine cha tatu ambacho ningependa kushauri kupitia ripoti ya bajeti ni kwamba kuna maeneo ambayo yameonekana fedha ambazo zinatolewa na Wizara ya Fedha kwenda kwenye maji zinaenda kwa kusuasua. Ningependa kuishauri Serikali kupitia Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba fedha zinaenda kwa wakati. Vilevile maeneo mengine madogo madogo kwa mfano kuna misamaha ya kodi kwenye vifaa vya maji, vifaa pia kuchelewa pale bandarini ambapo vyote vimeelezwa kwenye ripoti ya Kamati. Ningependa sana kuendelea kuishauri Serikali kuangalia mambo haya matatu. Pia tunaweza tukaangalia katika yale mapendekezo mengine ya Kamati, lakini kwangu nadhani kwamba haya matatu ni ya msingi sana kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kitu kimoja kwamba Naibu Waziri amefika pale Jimboni kwangu, kuna mradi mkubwa sana ambao unaendelea kwa zaidi ya miaka mitano ambao umekwama, Mradi wa Isupilo, Itengulinyi, Magunga ambao kwa kadri ya nafasi ambayo nimeipata nimekuwa nikiongea na Waziri, amejitahidi kufanya kazi yake, amekuja jimboni kuangalia changamoto hii, amejaribu kutatua, lakini bado changamoto iko pale pale. Wananchi wangu sasa hivi wameshachoka, toka mwaka 2014 wameongea kitu hicho hicho na wamenituma niendelee kuongea kuhusu mradi huu, mradi ambao umegharimu jumla ya shilingi bilioni 2.2, umelipwa bilioni 1.2 lakini mradi umekufa. Sasa hebu tuangalie tunapoteza au hatupotezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea tu kuwasihi viongozi wa Wizara, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Katibu Mkuu kwamba tuangalie namna ambayo tunaweza tukalisaidia Jimbo la Kalenga, tukasaidia Mkoa wa Iringa, tukasaidia namna ambavyo tunaweza tukapata maji katika Mkoa wa Iringa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru pia Wizara kwa kutusaidia zile milioni 49 katika Mradi wa Nyamlenge ambao Mheshimiwa Naibu Waziri alitusaidia na Mheshimiwa Waziri analifahamu hili, nilikwenda kwake nimeongea, ametusaidia kuweza kuziweka zile milioni 49 kwa ajili ya ku-design Mradi wa Nyamlenge ambao kwa namna moja au nyingine utasaidia kutatua changamoto katika vijiji 16 katika Jimbo la Kalenga. Naendelea kuishukuru Serikali na kuendelea kuipongeza Serikali kwa sababu nina imani na Mheshimiwa Mbarawa, nina imani na Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini vilevile Katibu Mkuu na Wizara yote kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niseme tu shukrani kwa baadhi ya taasisi ambazo zimeendelea kulisaidia Jimbo la Kalenga kupata maji. Niseme WARIDI wametusaidia sana ambao ni wa Marekani, USAID wametusaidia pia kwa kiasi kikubwa lakini pia Makanisa ya Anglikana na baadhi ya Makanisa mengine wameendelea kutusaidia katika kuhakikisha kwamba tunapata maji katika Jimbo la Kalenga. Zaidi ya yote niendelee kusisitiza zaidi na zaidi Mheshimiwa Mbarawa alikuja jimboni wiki tatu zilizopita, tukaongea kuhusu Mradi wa Kalenga- Tanangozi na akanisaidia na akasema kwamba niandike andiko ili tuweze kupata fedha kwa ajili ya mradi huu. Maandiko nimeshaandika nitamsaidia kuyafikisha katika meza yake aweze kututatulia tatizo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa yote, pale Kanisani kwetu sisi tuna wimbo huwa tunasema usinipite Mwokozi, usinipite Mwokozi, kwa hiyo nami leo nasema Mheshimiwa Mbarawa asinipite katika bajeti hii, aje Kalenga atusaidie kupata maji. Mungu ambariki, Wizara yake ibarikiwe na namshukuru sana, naamini kabisa kwamba 2019/2020 atatatua tatizo la maji katika Jimbo la Kalenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsanteni sana. (Makofi)