Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia na mimi angalau kidogo na nitajikita zaidi kwenye viwanda vyetu katika Jiji letu la Mwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa nyingine tena leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka miaka michache iliyopita Mji wa Mwanza ulikuwa maarufu sana kwa viwanda vya samaki na watu wake wengi sana walipata nafasi za maendeleo, za kiuchumi na uchumi kwa kweli ulikua sana. Hata asilimia tunayoizungumza leo inayochangiwa kwenye pato la Taifa na Mkoa wa Mwanza imetokana sana na imetengenezwa na viwanda vya samaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa viwanda hivi vya samaki leo ni viwanda ambavyo vinajiendesha kwa hali dhoofu sana. Nasema dhoofu sana kwa sababu zao hili la samaki miaka mitatu nyuma kiwanda kimoja cha samaki peke yake kilikuwa na uwezo wa kukata tani 250 kwa siku kikiwa kimeajiri wafanyakazi wasiopungua 600; na hawa walikuwa ni vijana kabisa wa kike na wa kiume. Leo tunapozungumza hapa, kiwanda kimoja cha samaki kati ya viwanda saba kinakata tani zisizopungua 20 mpaka 72 kwa siku, kikiwa kimepunguza wafanyakazi kutoka 500 mpaka 750 kufikia wafanyakazi 96 mpaka120. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni kwamba vijana wengi wamepoteza ajira lakini vijana wengi hawana pa kwenda ndiyo sababu unaona Mji wa Mwanza unazidi kujaa kwa vijana ambao hawana kazi, kila mmoja anatamani kufanya biashara ya umachinga, kila mmoja anatamani kufanya biashara ya umama lishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu! Tatizo liko kubwa! Mheshimiwa Waziri viwanda hivi vinakufa kwa sababu zao la samaki linapungua. Zao la samaki linapungua kwa sababu gani? Uvuaji wa njia za sumu umekuwa ni mkubwa zaidi na badala yake samaki hazipatikani kwa njia rahisi, lakini wenzetu wamezalisha samaki hizi na kwenda kuzivuna na kuzipanda makwao, leo unaweza kupata samaki wengi sana kutoka Ugiriki na kutoka Urusi na wameongeza ushindani zaidi kwenye soko letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, quality ya samaki wanaovuliwa sasa kwa sababu uvuvi haramu umekithiri, hii sumu inasambaa sana. Unapozungumzia uvuaji katika Ziwa Victoria, mikoa hii inayotumia sana uvuaji huu kwa Ziwa Victoria, lakini zipo nchi za jirani, Uganda na Kenya, wanafanya biashara kama sisi. Sasa wazo langu hapo Mheshimiwa Waziri, ni lazima tuangalie njia mbadala. Tutafanyaje kuhakikisha tunaokoa, uvuvi huu haramu unaondoka na tunabaki na uvuvi sahihi ambao unaweza kusaidia viwanda hivi?
Mheshimiwa Waziri, Mwanza kwa sasa ukipata mbinu mbadala ya kuhakikisha viwanda hivi vinaendelea na uzalishaji wake kama zamani, vinarudisha ajira kubwa iliyoangaka. Huna sababu ya kufikiria kujenga viwanda vipya vya samaki kwa sasa Mwanza. Hivi tulivyonavyo, kama tunakwenda kujenga viwanda vipya, hivi tunaviweka kwenye kundi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kiwanda cha Mwatex pale, miaka kumi iliyopita, tangu tukibinafsishe mpaka leo, wafanyakazi kutoka 700 na kitu mpaka 30 na kitu kwa siku. Hata walioondoka hawajalipwa mpaka leo, imekuwa ni kero na kasheshe kila kukicha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tuangalie hivi tulivyonavyo kwanza kabla ya kufikiria mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunacho kiwanda cha Tanneries pale, nilikuwa nataka kumpa taarifa rafiki yangu Mheshimiwa Msigwa, bahati mbaya tu nilichelewa, nilitaka tu nimtaarifu kwamba unapozungumza Kiwanda cha Tanneries hakihusiki na kuzalisha nyama, bali kinahusika na kutengeneza na kuzalisha mazao yanayotokana na ngozi. Kiwanda hiki kimeuzwa na kimekuwa godown, hakuna shughuli inayofanyika pale na tumepoteza vijana wengi ambao naamini Serikali mngefikiria vizuri, leo vijana wetu wangekuwa wanafanya kazi pale. Kwa maana siyo kwamba ng‟ombe nao wamekufa, ngozi hazipatikani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, majeshi yetu leo yangekuwa yanapata bidhaa za viatu kutoka pale, mikanda yao wangetoa pale na kadhalika. Sasa hivi tunavyozungumza, makampuni ya ulinzi yamekuwa mengi na maarufu sana nchini hapa. Wote hawa wanahitaji bidhaa za viatu hizi na mikanda yao ni hii hii ya bei za kawaida. Leo hata mikanda tunaagiza kutoka China na bahati mbaya sana inakuja ya plastiki ambayo haidumu, unanunua leo, kesho imekatika inabidi ununue mwingine.
Mheshimiwa Waziri nakuomba, tunayo kila sababu ya kuangalia umuhimu wa kiwanda hiki ambacho kilikuwa kinasaidia watu wa Mwanza kupata ajira na kadhalika, uangalie uwezekano wa kukifanya kirudi na sisi tukitumie kwa manufaa ya Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza suala la uboreshaji wa viwanda tulivyonavyo, tunazungumza suala la anguko kubwa la ajira. Kama ajira hii ambayo vijana wengi wanaitegemea, leo kila tukija hapa, nami kila nikisimama nazungumza juu ya ukuaji wa Mji wa Mwanza. Leo yapo maeneo tupetenga kwa ajili ya EPZ, hizi EPZ zinafanya nini? Tunajenga leo, tunatenga leo, matokeo yake ni baada ya miaka 30. Waachiwe watu maeneo haya wafanye biashara zao nyingine za kawaida, maana kuendelea kutunza maeneo makubwa, na mimi nikupe mfano, walikuja watu wa NDC toka mwaka 1974 wakachukua eneo la zaidi ya ekari 305, sawa na ekari 705. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo haya yamekaa toka miaka ya 1980 mpaka leo, eneo halijaendelezwa na tumeambiwa eneo hili ni kwa ajili ya viwanda vidogo vidogo. Pia maeneo mengi yanayochukuliwa hayalipwi fidia kwa wakati. Tunajua Halmashauri zetu hazina uwezo mkubwa wa ukusanyaji wa mapato. Hebu nikuombe Wizara yako ione umuhimu na maana halisi ya kuhakikisha maeneo yote yanapotengwa kwa ajili ya viwanda, aidha vidogo vidogo au viwanda vikubwa, tafsiri yake tunataka kupunguza mzigo, lakini tunataka kukuza uchumi, zaidi ya yote tunataka kuajiri vijana wengi zaidi ili tufikie kwenye malengo ambayo ilani yetu inasema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatuwezi kuboresha maeneo haya, hatuwezi kuokoa kundi kubwa la vijana ambao wanamaliza vyuo. Sio wanaomaliza vyuo tu, wako watu wana vipaji wanaweza kufanya kazi. Viwanda hivi tunavyovizungumza ni viwanda vinavyochukua watu wenye tabia tatu, wenye elimu ya chini, elimu ya kati na elimu ya juu, wote hawa wanataka ajira. Ni lazima tufike sehemu, kama tunataka kuepukana na matatizo ya msongamano wa vijana machinga, mama lishe na kadhalika kwenye maeneo mengi, lazima tuhakikishe tunajenga viwanda, lazima tuhakikishe viwanda hivi vinahimishwa, vinakuwa sawasawa na vinafanya kazi zake kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nakuomba tu kwamba nitakuunga sana mkono lakini kubwa ninalotaka kulisema, Mheshimiwa Mwijage sisi tuna imani na wewe. Tunayo imani kubwa, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano amekuamini na sisi tunakuamini. Imani yetu tuliyonayo kwako tunataka kuona, tunajua huu ndiyo mwanzo, tunataka kuona hapo ulipo na hayo unayoyasema unayasimamia, unayafanyia kazi. Na wewe ni jembe la shoka, hatuna shaka, hizi nyingine ni kelele tu tumeshazizoea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka uone watu hawana adabu, haiwezekani unazungumza, unatukana, unamaliza unaondoka bila kusubiri majibu. Hawana nia njema na Watanzania hawa.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Meshimiwa Mwenyekiti, tunataka watu ambao ukitoa hoja ya misingi kwa ajili ya Watanzania, ukitoa hoja kutetea vijana kwamba wanatafuta ajira, lazima ubaki upate majibu yake. Waangalie wako wapi? Mheshimiwa Kubenea yuko wapi hapa? Mheshimiwa Msigwa yuko wapi hapa? Wametukana, wameondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nataka niseme Waheshimiwa Wabunge, iko tofauti na lazima tukubali. Tofauti ya Mbunge wa CCM na Mbunge wa Upinzani ni kubwa na itabaki pale pale. Sisi ndio Wabunge wenye Serikali na hiyo ndiyo tofauti, hakuna namna nyingine. Sisi ndio wenye Serikali, ni lazima tuiunge mkono Serikali hii, tufikie malengo ya watu wetu kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mhesimiwa Mwenyekiti, mtu mwingine, rafiki yangu Mheshimiwa Mussa pale anashangaa kila tunachokisema tunazungumzia ilani. Kwenye ushindani kule si kila mtu alinadi ilani yake. Haya ndiyo matunda ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Leo ukisimama hapa unazungumza, mwisho wa siku unaomba. Ndugu yangu Mheshimiwa Mussa ameomba reli ya kati ianzie Tanga. Bila Ilani ya CCM usingeomba reli ya kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwashukuru sana na niendelee kuhimiza, naunga mkono bajeti asilimia mia moja, viwanda kwa ajira za vijana wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.