Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Yosepher Ferdinand Komba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata nafasi nami nichangie kwenye Wizara hii. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya afya njema anayonijalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nakishukuru chama changu kwa namna ambavyo kinaendelea kuniamini kutekeleza majukumu yangu. Kwa namna ya pekee namshukuru Mwenyekiti wetu na ninamwombea kila la heri katika mapambano haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani. Maoni ambayo wameyatoa ni maoni ambayo Serikali inatakiwa isikilize na kuyachukulia maanani. Ni maoni ambayo ukiangalia hata hotuba ya mwaka 2018 na miaka iliyopita, kuna mambo yanajirudia. Kwa hiyo, inaonekana bado Serikali haijawa sikivu vya kutosha, kuna baadhi ya hoja zinajirudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati namsikiliza mama yangu Waziri Mheshimiwa Prof. Ndalichako akisoma hotuba yake ya mwaka huu, ni hotuba ambayo ukiisikiliza ina ladha sana. Baada ya kumsikiliza nikasema ili niweze kumhukumu vizuri au ili niweze kusema vizuri kwenye hotuba hii, nikajaribu kupitia hotuba ya mwaka 2018. Nimepitia hotuba ya mwaka 2018 nikafananisha na hotuba ya mwaka huu. Kuna baadhi ya mambo nimeyagundua. Mambo haya yanafanya hotuba ya mwaka huu isionekane bora kwa sababu ya historia ya hotuba ya mwaka 2018. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, ukiangalia suala zima la bajeti, wameongea wenzangu, bajeti ya Wizara ya Elimu inaendelea kushuka. Mwaka 2018 kulikuwa na shilingi trilioni 1.4, mwaka huu imetengwa shilingi trilioni 1.3, inashuka. Inashuka katika mazingira ambayo bajeti kuu ya Serikali inaongezeka; inashuka kwenye mazingira ambayo tunasema wanafunzi wanaongezeka kwenye shule za msingi na sekondari, inashuka katika mazingira ambayo vyuo vikuu wanafunzi wanazidi kuhitaji mikopo, lakini bajeti ya elimu inazidi kushuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, nimeangalia kwenye matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo. Pamoja na bajeti kushuka, matumizi ya kawaida yameongezeka lakini matumizi ya maendeleo yameshuka. Kwa hiyo kuna athari nyingi za hii bajeti kushuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye suala la walimu na wataalamu. Wataalamu tunajua wanasaidiwa na Kitengo cha COSTECH lakini ukiangalia mwaka wa fedha uliopita, walikuwa na shilingi trilioni 1.6 wametengewa, lakini hawajapelekewa hata shilingi, ambapo wao ndio wanashughulikia masuala ya tafiti na sayansi. Hata shilingi haijapelekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu wametenga, hatujui kama itaenda. Kama ya mwaka 2018 haikwenda, ya mwaka huu hatujui. Kwa hiyo, hivyo ndivyo namna ambavyo mnaihudumia Wizara hii kwa watafiti na wataalam ambao wangeweza kutusaidia hiyo nchi ya viwanda tukaifikia kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisalia hapo, kuna suala la capitation, lipo kwenye fungu la maendeleo. Tunafahamu capitation mmesema mtakuja na kikokotoo kipya; mtakuja na utaratibu mpya wa namna ya kuandaa hii capitation ili wale wahusika wapate nafuu. Kwa sasa hivi mmefanya tafiti kwenye shule moja tu ambayo ina wanafunzi 444, wao kwa mwezi wanapewa shilingi laki moja na themanini na saba na point. Shilingi 187,000/= uigawanye kwa kila mwanafunzi, kila mwanafunzi anapata chini ya shilingi 500/= kwa mwezi. Hiyo ndiyo capitation ambayo mnahubiri hapa elimu bure, elimu bure, elimu bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwashauri na niwaombe, mnaposema kitu ni bure, inatakiwa kiwe bure kweli. Elimu siku zote ni mchakato, elimu siyo suala la mara moja, ni mchakato. Nawaomba mseme elimu bila ada, siyo elimu bure. Haijawa elimu bure kwenye nchi hii bado. Wako wazazi ambao wanapangishia watoto wao vyumba ili wasitembee umbali mrefu, huwezi kumwambia yule mzazi mwanaye anasoma bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako wazazi ambao wanalipia boda boda na usafiri mwingine watoto wao kwenda shule kila siku, huwezi kusema ile ni bure. Wako wazazi wanachangia majengo. Siku hizi majengo kama alivyosema Mheshimiwa Tendega, mwezi wa Tatu watu wanaenda shule, wanachangia. Wazazi wanaitwa, nyie wazazi wenye watoto waliofaulu, changieni madarasa yakamilike; huwezi kumwambia yule mzazi mwanaye anasoma bure. Kwa hiyo, hiyo ni elimu bila ada, lakini bado wazazi wana mzigo mkubwa wanaolipia kwenye suala la elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu lingine nataka kuongelea siasa vyuoni. Bahati nzuri nimekuwa mwanafunzi, nimekuwa mwalimu na sasa hivi ni mwanafunzi, kwa hiyo, ninachokiongea nakifahamu. Kumekuwa na tatizo kwenye vyuo vyetu vikuu. Vyuo vingi sasa hivi kumekuwa na mkanganyiko; imekuwa ni kosa la jinai kujihusisha na siasa au kuonekana una mrengo fulani wa siasa, imekuwa kosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa Upinzani, wale ambao wanaonekana wana misimamo dhidi ya Uongozi wa Chuo au ya Serikali, ndio hao wanaopatishwa shida kwenye vyuo; lakini tunaona CCM, UVCCM wanafanya vikao kwenye Vyuo vya DUCE, Mwalimu Nyerere, wanafanya vikao. Inapokuja kwenye Vyama cha Upinzani inakuwa shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, Viongozi na Wasimamizi wa Vyuo vyetu wamekuwa wanaingilia chaguzi za wanafunzi kinyume na taratibu. Wakishaona anayegombea ana mrengo fulani, uongozi wa chuo utashirikiana na Polisi kuharibu ule uchaguzi bila sababu ya msingi; na mara nyingi wanakuwa wanatumwa na Chama Kikuu cha Siasa chama ambacho kinatawala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Waziri wa Elimu atakapokuja kuhitimisha hapa atuambie, kama kweli ni marufuku kwa watu ambao wanasoma vyuoni ambao ni watu wazima, wengine wametoka makazini, wengine wametoka sehemu mbalimbali kufanya siasa, iwe marufuku kwa wote isiwe na double standard. Watu hao mnaowapa marufuku ni watu ambao wanaijua siasa vizuri sana, wengine wanaisomea wanatafutia degree.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la changamoto za watoto wa kike; naomba hapa nianze na suala la pad. Tunafahamu Serikali kwenye bajeti iliyopita ilitoa VAT kwa ajili ya kufanya hili suala la pad lishuke bei, lakini Mheshimiwa Waziri ni shahidi, hakuna badiliko lolote lililotokea. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri kushirikiana na TAMISEMI, kushirikiana na Wizara ya Fedha waone namna ambavyo suala la pad wanaweza wakaliingiza kwenye capitation fee. Watoto kuanzia darasa la tano mpaka la saba wanaweza wakawa na utaratibu wamewawekea waweze kupata pads bure, tukiliacha hivi halitakuwa na maana yoyote kwa wanafunzi wetu ambao wanaendelea kupata shida, ambao wanaendelea kupata hii changamoto na kukosa kuhudhuria masomo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nigusie suala ambalo liko kwenye Wilaya yangu ninayoishi, Wilaya ya Muheza, tumeongea mara nyingi sana kuhusu changamoto za Walimu. Changamoto ambazo zinawafanya Walimu washindwe kutimiza majukumu yao, changamoto ambazo zinawafanya Walimu wanakosa morale ya kufundisha na kuwasaidia watoto wetu. Kwenye Wilaya ya Muheza tulikuwa na shida hiyo ya Walimu katika baadhi ya maeneo, tukaamua kwenye Baraza kwamba baadhi ya Walimu wahamishwe kwenye Kata moja kwenda nyingine na kiutaratibu Walimu wanapohamishwa kuna ile tunaita disturbance wanatakiwa walipwe, lakini mpaka sasa hivi ninavyoongea walikuwa Walimu 86 waliotakiwa kulipwa, lakini wamelipwa Walimu 20 tangu mwaka jana mwezi wa Nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe Mheshimwa Waziri aliangalie hilo, wale Walimu wamekosa morale kwa sababu disturbance fee yao hawajalipwa, mpaka sasa hivi zaidi ya mwaka, wanadai zaidi ya Walimu 66.

Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri alichukulie maanani hilo alifanyie kazi ili kuongeza morale ya walimu ambao wanafundisha kwenye maeneo yetu ili waweze kuona na wao ni wafanyakazi kama wafanyakazi wengine ambao wanathaminiwa na ambao wanatoa mchango mkubwa kwenye Taifa hili ili kuongeza masuala ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee fedha za mikopo kwa ufupi sana. Tumeona hapa fedha za mikopo ziko kwenye Fungu la Miradi ya Maendeleo, ambazo zinachukua asilimia kubwa kuliko miradi ya maendeleo yenyewe. Sisi tunashauri kupitia hata hotuba ya Kambi imesema, hizi fedha zitengewe Fungu Maalum ili tuweze kujua jinsi zinavyotoka na jinsi zinavyorudi, lakini hizi fedha zikiwa na Fungu Maalum tutajua fedha halisi zitakazobakia kwenye maendeleo mengine ya elimu kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari kwa sababu kwa kuziacha humu, inaonekana kwenye maendeleo kuna fedha nyingi, lakini kwenye uhalisia nusu ya fedha au zaidi ya nusu zimeenda kwenye Bodi ya Mikopo ambapo watu wanaenda kulipia ada, chakula na malazi, kitu ambacho tunawaacha wanafunzi wetu wanakaa chini, wanakaa nje na wanakosa huduma muhimu kwenye mashule kwa sababu fedha nyingi….(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante. Nitakuongezea muda ukiunga mkono hoja, Mheshimiwa Kahigi, atafuata Mheshimiwa Rukia.

MBUNGE FULANI: Mwambie nimeshaunga.

MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani. (Makofi)