Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba ya Waziri wa Elimu. Naomba nizungumzie mambo makubwa matatu. Jambo la kwanza ni kuipongeza Serikali, kuwapongeza watendaji pamoja na watumishi wote wa Wizara hii wakiongozwa na mama yetu, Mheshimiwa Ndalichako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo mengi sana ambayo yamefanyika, kwangu binafsi kwa niaba ya wananchi ambao ninawawakilisha hapa, nitakuwa mtovu wa fadhala kama sitatambua kazi kubwa ambayo wameifanya ndani ya Jimbo la Nachingwea hasa katika eneo hili la elimu. Uko uboreshaji mkubwa wa Chuo cha Walimu Nachingwea umetumia gharama kubwa sana na sasa hivi mazingira yamekuwa ni yakuvutia sana watu kuendelea kupata elimu katika eneo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niunganishe na ombi moja kwa moja hapo hapo, pamoja na jitihada zile bado tunaomba pia tupate fedha kwa ajili ya kukarabati nyumba za watumishi katika eneo lile au katika taasisi ile Chuo cha Uwalimu Nachingwea. Nyumba zilizopo bado siyo nzuri na hazivutii, lakini gharama yoyote ambayo mtakuwa mmetusaidia, basi mtakuwa mmeyaweka mazingira yale yawe ya kuvutia zaidi na hivyo kutoa elimu ambayo tunaikusudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo pia nilitaka nipongeze ni suala zima la ajira mpya kwa walimu. Tunaishukuru sana Wizara, tumepata mgao wa walimu ingawa bado hawatoshi na changamoto kubwa tunayo katika eneo la walimu wa sayansi. Walimu ambao tumepatiwa kwa mahitaji ilikuwa ni 30 lakini tuliopokea ni chini ya asilimia 50. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri na wataalam wakeo hebu walione hili ili waweze kutusaidia tupate walimu wa kutosha ambao wataenda kutoa maarifa kwa vijana wetu katika shule zetu za Wilaya ya Nachingwea na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nilitaka nichangie kupitia hotuba hii linalohusu namna ya kuwaendeleza walimu. Ukiangalia kada mbalimbali za Utumishi, ipo mifumo ambayo inawa-favour watumishi tofauti na kada ya walimu. Katika level za Form Four ambazo wamekuwa wanatumia vyeti kupata elimu ya ngazi ya cheti, wenzetu wa kada nyingine wamekuwa wanatumia vyeti hivyo kwa ajili ya kupata Diploma na Degree, lakini kwa upande wa walimu, nafikiri kwa wale walimu watakubaliana name; tumekuwa na changamoto kutoruhusu walimu wetu kutumia vyeti vya Form Four au vyeti vya certificate kutoka Grade A mathalani kwenda kupata ngazi nyingine ikiwemo Diploma au Degree.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu wataalam wa Wizara ya Elimu wakae walione namna bora ambavyo tunaweza nayo pia tuka-switch na tukatengeneza utaratibu ambao utasaidia walimu au wale wanaojiendeleza na ualimu kutumia certificate kwenda ngazi nyingine za juu ili kuondoa urasimu ambao kwa sasa hivi upo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua imefanyika hivi kutokana na umuhimu wa kada ya elimu na labda lengo lake ni ku-impart knowledge zaidi kwa walimu ili waweze kuwa walimu wazuri, lakini bado naamini mafunzo na mitaala ambayo wanaitumia kupata elimu yao, bado inaweza ikasaidia walimu hawa kujiendeleza na kupata elimu ya juu zaidi ya vyeti ambavyo wamekuwa navyo katika wakati tulionao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ambalo nilitaka nichangie katika hotuba hii ni suala zima linalohusu gharama za uendeshaji katika vyuo vyetu. Serikali imefanya kazi kubwa ya kuboresha mazingira ya vyuo na sasa hivi vyuo vingi vikongwe vinapata huduma muhimu. Hata hivyo, bado zipo changamoto za kuhakikisha vyuo hivi vinajienda vyenyewe. Vyuo vingi sasa hivi wana changamoto ya kupata fedha kwa ajili ya kulipia umeme; vyuo vingi sasa hivi vinapata changamoto kubwa sana kwa ajili ya kupata fedha kwa ajili kugharamia na hata kulipia bili za maji. Yote haya ni kwa sababu Serikali kupitia kukusanya maduhuli, ikiwemo ada na vitu vingine, gharama hizi zote zimekuwa zinaenda Serikali. Kwa hiyo, mgao ambao wanarudisha katika vyuo vyetu haukidhi mahitaji ya vyuo vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kwa heshima na taadhima Mheshimiwa Waziri pamoja na wataalamu wake hebu walione hili, badala ya kuendelea kuwakatisha tamaa Wakufunzi ambao wako katika vyuo hivi vya kati au Vyuo hivi vya Ualimu, tuone namna tunavyoweza kurudisha sehemu ya gharama ili waweze kumudu gharama mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia hili kwa experience ya chuo ambacho nimekitaja, mara nyingi nimekuwa nawasiliana nao, nimeona namna wanavyohangaika kulipia sehemu ya gharama ambazo kimsingi zamani ilikuwa moja kwa moja wao vyuo ilikuwa na mamlaka ya kukusanya na kuweza kutumia moja kwa moja. Kwa hiyo, niliona hili nalo niliwasilishe kama sehemu ya changamoto na pia nipendekeze kwa Serikali ione namna bora ya kuweza kuliangalia hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ambalo nilitaka nichangie katika Wizara hii ni suala nzima linalohusu gharama kwa ajili ya wanavyuo walioko katika hivi Vyuo vya Ualimu. Kwa mwaka sasa hivi wanafunzi wanalipa siyo chini ya shilingi 600,000/=. Nia njema ya Serikali kutoa elimu bure ambayo tunaiunga mkono na imeleta mafanikio makubwa sana, imeanza katika ngazi ya shule za msingi, tumekwenda mpaka sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipato cha Watanzania hawa ambao tumekuwa tunawapa elimu bure kuanzia msingi kwenda sekondari, bado kumekuwa na changamoto ya namna wanafunzi wanavyoweza kugharamia sehemu ya malipo kwa ajili ya kulipia hii Elimu ya Ualimu. Kwa hiyo, nimefanya utafiti kwenye baadhi ya vyuo, wanafunzi wengi wanashindwa kugharamia hizi gharama na imekuwa inaleta usumbufu kidogo katika kukamilisha mafunzo au masomo ambayo wamekuwa wanayapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pamoja na Serikali kuwa na mzigo mzito wa kukopesha wana vyuo katika ngazi mbalimbali za Degree na Shahada mbalimbali naomba nitoe ushauri kwa watu wa Wizara waone kama kuna uwezekano pia wa kuwaangalia hawa Watanzania ambao kwa sehemu kubwa wamenufaika na elimu bure mpaka wanavyofika katika ngazi hii ya elimu ya kati ambayo tukiweka masharti nafuu ya kuweza kuwafanya hawa wamalize vyuo vyao, basi tutakuwa tumejikuta tume-groom walimu wa kutosha ambao watakwenda kutoa elimu moja kwa moja katika maeneo yetu na hivyo tatizo la walimu litaenda kupungua kwa kiasi kikubwa sana. Jitihada hizi za Serikali ambazo zinafanyika, sisi tunaendelea kuziunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwisho kabisa, nizungumzie suala linalohusiana na mgawanyo wa hawa walimu ambao tulikuwa tunawatawanya. Ukienda kwenye maeneo ya Sekta za Utalii, watu kama wa Kilimanjaro huwa wananufaika kwa sehemu kubwa sana na mgao ambao umekuwa unapatikana na vyanzo vile vya utalii na vitu mbalimbali. Hata hivyo, katika maeneo ambao kumekuwa na vyuo ndiyo maeneo ambayo yamekuwa yanaongoza kwa kutokuwa na walimu wa kutosha. Wilaya kama Nachingwea mathalani, ni jambo la ajabu sana kukosa walimu hasa katika level za shule za msingi. Hapa tuna upungufu mkubwa sana, lakini walimu wengi wanazalishwa pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namwomba Mheshimiwa Waziri, najua hivi vyuo ni vya Kitaifa na tunazalisha hawa walimu kwa ajili ya kuhudumia Taifa zima. Naomba tufanye upendeleo wa makusudi katika maeneo ambapo vyuo vipo, basi angalau tuone tunanufaika kwa kiasi kikubwa. Kwa hili, naomba nilete ombi kwa Mheshimiwa Waziri aiangalie Wilaya ya Nachingwea, mgao ambao tumepatiwa safari hii bado hauakisi idadi ya shule tulizonazo na wingi wa shule ambazo tunazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii imetupa changamoto ya namna kutoa elimu ambayo kimsingi tumekuwa tunaikusudia. Kwa hiyo, ebu tutumie chuo kile kilichopo Nachingwea kutupendelea kidogo ili tuweze kupata walimu ambao watatoka moja kwa moja pale na hasa wale ambao wametoka katika shule jirani kutoka maeneo yale ya Chuo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatufanyi hivi kwa maana ya kuwabagua watu wengine, lakini ni ukweli ambao utakubaliana name, lazima moto unapodondokea kwenye mkono, basi yule ambaye umemdondokea aanze kujitoa yeye mwenyewe kabla ya mtu mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliomba nichangie hayo kwa ufupi sana ili kuweza kuboresha bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)