Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mungu, Muumba wa Mbingu na Dunia kwa kuniwezesha nami niweze kuchangia hotuba hii ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya mwaka 2019/2020. Hotuba hii inakwenda kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kama ilivyoelekeza na kuhakikisha hali ya usalama kwa raia na mali zao unakua wa uhakika. Aidha, nichukue nafasi hii kwa mara nyingine tena kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara hii kwa kuandaa hotuba nzuri.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa juhudi kubwa inazoendelea kufanya kwa majeshi yetu ya Polisi, Uhamiaji, Zimamoto pamoja na Magereza. Serikali imeendelea kufanya maboresho mbalimbali hasa kwa Askari wetu, makazi yao pamoja na mambo mengine mazuri yenye tija kubwa hasa katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao. Serikali imeendelea kudhibiti hali ya ulinzi na usalama nchini kwa kuboresha mazingira ya kuishi Askari na kufanyia kazi, kutoa huduma bora za kubaini, kutanzua na kudhibiti uhalifu, kudhibiti vitendo vya rushwa ndani ya Jeshi la Polisi pamoja na kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi katika kupambana na uhalifu nchini. Haya ni mambo mzuri ya kujivunia hasa katika kipindi hiki. Aidha, hali hii imechangia kupunguza makosa ya kiuhalifu kutoka makosa 37,602 mwaka 2017 hadi kufikia makosa 36,228 mwaka 2018.

Mheshimiwa Spika, halikadhalika kwa upande wa uhamiaji Serikali inatekeleza kwa mafanikio makubwa awamu ya pili ya Mradi wa Uhamiaji Mtandao, ambayo inahusisha utoaji wa huduma ya viza pamoja na vibali vya ukaazi vya kielektroniki. Mradi huu ni wa kisasa kabisa na unaendana kabisa na dunia ya sasa.

Mheshimiwa Spika, vilevile naipongeza Serikali kwa kuzindua mfumo huo hapo mnamo tarehe 26 Novemba, 2018, ambapo sasa unamwezesha mteja kufanya maombi yake kwa njia ya mtandao kama wafanyavyo nchi nyingine zilizoendelea. Hakika mfumo huo, utarahisisha utoaji wa huduma bora za uhamiaji, kuimarisha ulinzi na usalama, kuongeza udhibiti wa wageni wanaoingia nchini, ukusanyaji wa maduhuli ya Seriklai na kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi kupitia sekta ya uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kuendelea kuwawezesha Jeshi letu la Zima moto kwa kuwapa vifaa zaidi kama magari ili pindi yanapotokea matukio ya moto iwe rahisi kuyahimili. Pia naishauri Serikali kuangalia upya namna ya kuwatumia wafungwa waliopo Magerezani ili wawe wanazalisha kama alivyowahi kusema Mheshimiwa Rais wetu, wafungwa hawa watumike katika kuzalisha vitu mbalimbali kama mazao. Baadhi wana taaluma zao, pia wazitumie kuleta faida kwa jamii wakiwa huko huko Magerezani.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kutambua umuhimu wa usalama wa raia pamoja na mali zao, kama mdau mkubwa, nimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha vituo vya Polisi katika Jimbo langu vinajengwa. Nami kwa kushiriki kwa hali na mali na kuchangia mambo mbalimbali yanayohusu sekta hiyo kama ujenzi wa nyumba za makazi ya Askari wetu, kukarabati gari la Polisi, tumejenga baadhi ya vituo vya Polisi kwa nguvu zetu wenyewe, lakini bado havijakamilika.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali yangu sikivu katika bajeti hii kwa umuhimu wa jambo hili sasa watusaidie kumalizia ujenzi wa vituo hivyo ili vianze kuwahudumia wananchi wangu. Tukifanikiwa kumalizia vituo hivyo, kwa kiasi kikubwa hali ya usalama Jimboni kwangu itazidi kuimarika. Aidha, tuna changamoto ya gari la Polis. Uhitaji wa chombo hicho ni muhimu kwani gari lililopo halitoshelezi kuhudumia Jimbo zima. Tukipatiwa gari litasaidia kufanya doria za mara kwa mara ikizingatiwa Jimbo letu ni kubwa kiutawala.

Mheshimiwa Spika, naleta tena ombi hili kwa Serikali yangu sikivu kutusaidia gari la Polisi katika bajeti hii. Halikadhalika, tumekuwa na migogoro ya wakulima na wafugaji na kupelekea maafa. Nakuomba Mheshimiwa Waziri aje Jimboni kwangu kututembelea na kutatua changamoto iliyopo ambayo inahusisha pia na Jeshi letu la Polisi.

Mheshimiwa Spika, aidha, bado tuna changamoto ya nyumba za Polisi. Namwomba Mheshimiwa Waziri wakati wa majumuisho aweze kutupatia majibu ya maombi yetu na changamoto nilizoziainisha.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.