Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Ruth Hiyob Mollel

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia nami pia kwenye hii Wizara. Jambo kubwa ambalo napenda kulizungumzia ni kuhusu mikutano ambayo tunanyimwa kufanya, wakati kikatiba tunaruhusiwa kukusanyika na kukaa na kuzungumza mambo yetu kama vyama, lakini imekuwa ni vigumu kufanya hivyo kwa sababu tunazuiwa kufanya mikutano, hata mikutano ya ndani.

Mheshimiwa Spika, mimi ni Diwani wa Mkuranga, mwezi wa jana nilikuwa na kikao tume-book ukumbi kwa ajili ya kuwa na vikao vyetu vya chama kwa ajili ya kuchagua viongozi wa chama. Nimekwenda Mkuranga, polisi wamekwenda wamemtisha yule bwana mwenye hall pale Mkuranga, akakataa kutupa hall la kufanyia mkutano. Tukaondoka pale, tukaenda kwenye Ofisi za chama, tukakaa nje, lakini bado huwezi kuamini defender zimekuja zina-patrol, wana-patrol watu ambao tumekaa tunazungumza mambo yetu, hatuna silaha, hatuna kitu chochote, patrol inapita mpaka tumemaliza mkutano pale nje, tena nje ya Ofisi ya Chama, nikajiuliza yaani Tanzania tumefikia kiasi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi tumekaa tunazungumza mambo yetu, hiyo petroli ya walipakodi inayozunguka na defender muda wote na maaskari wamejaa kwenye defender, ni sisi kweli wanatuchunga au wanatutisha. Nafikiri hapa tulipofikia si penyewe, tunataka tuirudie Tanzania yetu ambayo tulikuwa tunakaa, tunafanya mikutano yetu kama ni mikutano ya ndani ambayo imeruhusiwa, basi Mheshimiwa Waziri aje na kauli anapokuja kuhitimisha hoja yake atuambie kwanza ni sheria gani ambayo inatunyima sisi kuwa na vikao vyetu vya ndani, wakati chaguzi zinakuja ni lazima sisi kama chama tujipange kwa ajili ya kuingia kwenye chaguzi, tutajipangaje kama hata mikutano ya ndani wanatuzuia kuifanya. Naomba Mheshimiwa Waziri akija kuhitimisha hoja yake aweze kutuambia ni kanuni gani anayoitumia kutokuruhusu sisi kufanya vikao vyetu.

Mheshimiwa Spika, maandamano; maandamano ni namna moja ya wananchi kutoa…

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

SPIKA: Taarifa, pokea taarifa Mheshimiwa Ruth Mollel.

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Ruth Mollel, kwanza mimi namheshimu sana na nafikiri kwamba yeye kwa fursa kubwa aliyoipata katika Jimbo langu la Mkuranga na namna ya kazi anayoshiriki kufanya pale, sikutegemea kama angeweza kuwa ni mmoja katika Wabunge wanalolishutumu Jeshi la Polisi. Nataka awe mkweli kwamba Mheshimiwa Ruth Mollel anafanya mikutano katika Kata ya Kitomondo amekutana na akinamama hadharani wala siyo mikutano ya ndani na anatoa vifaa na vitu mbalimbali. Amekwenda Kata ya Vikindu, amefanya mikutano, ametoa pesa misikitini, amefanyaje, hadharani wala siyo kwa kificho na Ofisi ya Chama cha CHADEMA Mkuranga haijawahi kuwepo. Sasa nadhani wakati Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani atakapo kuja kumjibu kwa kuwa anataka ayapate hayo anayoyaomba hapa, Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, basi mpeni hiyo ladha ambayo anaitamani.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

SPIKA: Mheshimiwa Ruth Mollel taarifa hiyo.

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, hiyo taarifa kwanza siipokei, kwanza kama Mbunge ni haki yangu kwenda kwenye huo Mkoa kuna kutoa msaada na vile vile kunizuia kufanya, hili jambo limetokea na ni lazima nitalisema kwamba walituzuia kufanya mkutano na defender zilikuwepo.

SPIKA: Kengele imelia kwa sababu ulikuwa umenani kidogo, nakuongezea dakika moja ili umalizie hicho cha mwisho.

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nilikuwa nazungumzia suala la maandamano, kwamba watu wanapoandamana wanatoa hisia zao kwa sababu siyo kila mtu ana nafasi ya kumwona Rais, saa nyingine Rais haambiwi ukweli, lakini watu wanapoandamana kwa amani, wanatoa hisia zao kusudi Mheshimiwa Rais aweze kujua wananchi wake waliomteua na kumuweka madarakani wanamawazo gani na maeneo gani ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, maandamano yaruhusiwe, Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani atuambie ni kwa nini anazuia maandamano ya watu kutoa hisia zao. Wananchi wanahitaji kusimamiwa na kulindwa, waende waandamane kwa salama watoe hisia zao na hiyo ni namna mojawapo ya watu kutoa vitu ndani ya roho zao, ukiwafungia watu ndani yanakuwa matatizo makubwa sana.