Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nianze na hoja ya uhuru wa vyombo vya habari.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea naomba niweke record sawa kwamba Tanzania Daima imefungiwa mara kadhaa na kupewa onyo mara kadhaa. Tunachotaka, Serikali isikae upande mmoja. Tunapokuwa tunalalamika ndani ya Bunge, tunategemea Serikali itachukua maoni yetu na kuyafanyia kazi. Watu wanapoitwa ni hatari; na vyombo vya habari vinasomwa na watu wengi. Tunategemea Serikali aidha ichukue hatua inayowezekana kama ilivyochukua hatua kwenye vyombo vingine vya habari ikiwepo Gazeti la Tanzania Daima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la uhuru wa vyombo vya habari tunategemea Serikali ije na mkakati wa kuweza kuwalinda hawa wenye vyombo vya habari pamoja na Waandishi wa Habari. Mpaka nasimama hapa kuzungumza, kuna Mwandishi wa Habari ambaye mpaka leo yamekuwa malalamiko ya Waandishi wa Habari wenyewe pamoja na sisi Wabunge na wananchi wengine. Azori mpaka leo hatujasikia Serikali inasema nini juu ya huyu Mwandishi wa Habari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Watanzania wana haki ya kupata habari kwa mujibu wa Katiba yetu, lakini Waandishi wa Habari wana haki ya kutoa habari. Ni lazima tujue hapa ni kweli kwamba uhuru wa habari una mipaka yake, lakini hiyo mipaka isiwe pale ambapo Serikali inatakiwa kukosolewa. Serikali lazima ikosolewe. Ni kweli lazima kuwe na mipaka kwa sababu kila kitu kikipita kiasi ni sumu. Waandishi wa Habari wanahitaji ulinzi. Sasa hivi wanatishwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, anaweza akaja Mwandishi wa Habari kwamba tunaomba azungumzie utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano. Anapoanza kuzungumza, anakwambia aah, hayo siwezi kutoa kabisa. Sasa umeniruhusu nitoe mawazo yangu; hili suala litaleta shida sana kwa sababu, Waandishi wa Habari wanaweza kutoa habari kwenye chanzo chochote. Sasa kama watawekewa mipaka na vitisho, sidhani kama tutalisaidia Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, tulikuwa tumetoka kwenye hali ambayo sasa tunaamini kwamba ni Taifa huru na uhuru wenyewe ni pamoja na Waandishi wa Habari kuwa huru kutoa kile ambacho wanaona kinastahili kutolewa kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni BASATA. BASATA majukumu yao ni pamoja na kukuza wasanii wetu, lakini tunaona sasa majukumu ya BASATA yamebadilika. Wasanii hawa wanapokuwa wanaanza kule chini, jukumu la BASATA ni kuhakikisha wanakuza vipaji vyao, lakini leo tunaona wanaanza kuwafungia wasanii. Huyu msanii mpaka anaanza kutambulika na Taifa huko chini ana mikakati aliyojiwekea.

Mheshimiwa Spika, napenda nijue Serikali ina mkakati gani wa kuweza kukuza vipaji vya vijana wetu? Siyo wanakuja kuwatambua pale ambapo sasa ana uwezo wa kulisaidia Taifa kwa pesa zake kwenda nje. Kwa sababu sasa hivi kama msaanii anataka kwenda nje ya nchi lazima atoe taarifa kwa BASATA, lakini BASATA mbona hawajaja na mkakati wa kuwasaidia kuwatafutia huko nje; aidha kuwaunganisha na network ya wasaanii wengine ambao wako nje ya nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunategemea chombo hiki kiwasaidie na siyo kuwakandamiza. Jambo lingine ni viwanja vya michezo. Tunatambua kuna viwanja vingi ambavyo vinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi, sitataka kuhoji sana kwa nini wanamiliki viwanja hivi, lakini nilizungumza Bunge lililopita kama wameamua kuvimiliki waviboreshe. Kuvimiliki tu halafu mkashindwa kuviboresha sidhani kama mnawasaidia Watanzania, kwa sababu viwanja hivi vingine kabla, tulipokuwa kwenye mfumo wa chama kimoja vilikuwa vinaendeshwa na Watanzania wote siyo Chama cha Mapinduzi peke yake. Sawa, mmevichukua, tunaomba basi mviboreshe ili viweze kuwasaidia vijana wetu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ningependa kujua, tunapokuwa tunazungumzia mara nyingi hapa, Wizara imekuwa inaleta watu tunawapongeza waliofanya vizuri, ikiwemo Taifa Stars. Taifa Stars ilifanya vizuri na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akatoa promotion ya pombe ambayo iliuzwa nusu bei.

Mheshimiwa Spika, ni vizuri, labda inawezekana tunatafuta njia nyingine ya kuweza kuwasaidia vijana wetu, lakini sidhani kama ile njia ilikuwa sahihi sana. Kwa nini Wizara isije na mkakati; na hamuwezi kuja na mkakati kama hamjajua kwa nini tunashindwa. Kama wameshinda, Serikali ije sasa na mkakati, siyo wa nusu bei ya pombe kwa sababu watu walilewa na sidhani kama ilisaidia mpaka leo.

Mheshimiwa Spika, sasa sidhani kama huo ni mkakati wa Wizara au ni yeye tu alikuja na ile style na hamjasema chochote mpaka leo. Kama itakuwa hivyo, basi tujue kama ni style ya Awamu ya Tano kwamba watakuwa wanawapa nusu bei ili vijana wetu waweze kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, narudia tena kusisitiza, Serikali makini haiogopi kukosolewa. Naamini kuna mambo mazuri yanafanyika, sasa ili yaonekane ni mazuri lazima waruhusu mawazo ya watu wengine waseme. Hamwezi kufanya wenyewe, mnataka kujipongeza wenyewe, lakini anayetaka kukosoa haruhusiwi. Inajenga tafsiri ambayo siyo nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie amejipangaje kuweza kuwalinda wamiliki wa vyombo vya habari, pamoja na waandishi wa habari. Ni namna gani hawa watu wanalindwa? Kwa sababu, hivi vitisho vimekuwa vingi sana.

Mheshimiwa Spika, mwandishi mwenzao wa habari, Serikali inasema nini? Imefikia wapi mpaka leo? Huyu mtu yuko wapi? Lazima Serikali iseme, kunyamaza kimya mnawafanya watu wanakuwa na sintofahamu. Wao hawawezi kusema, sisi ambao tupo kwa niaba yao lazima tuseme.

Mheshimiwa Spika, umezungumza vizuri kipindi anazungumza Mheshimiwa Mwakajoka. Narudia kusema ni vizuri kama sheria inafuatwa kwenye vyombo vya habari, wasiangalie baadhi ya vyombo vya habari. Hili jambo la kutaja watu hadharani kwamba hawa watu ni hatari, kuna mambo mpaka ya ushoga yameandikwa kwenye magazeti.

Mheshimiwa Spika, kuna viongozi ambao wameaminiwa na watu, ni vizuri Serikali ije iweke sawa jambo hili. Kama kweli kuna watu wanafanya mambo hayo, sheria iko wazi, kwa nini wasipelekwe huko kwenye vyombo vya sheria ili sheria ikatafsiri kwamba huyu mtu anafanya kosa la ushoga? Sheria iko wazi, kwa nini chombo hiki kinaandika na Serikali inakaa kimya. Je, tuamini kwamba ni kweli Serikali imepeleka hayo mawazo ili gazeti liandike? Kama sivyo, Serikali isimame hapa itoe maamuzi juu ya chombo hiki. Ukisema hawa watu ni hatari, uhatari wake uko wapi? Umewataja majina na picha zao ziko pale.

Mheshimiwa Spika, wengine ni viongozi ambao tunawaamini, wanaongoza watu wengi ambao wako huko nje. Vinapotokea vitu kama hivi, hatari siyo mpaka mwone watu wanaandamana. Ukiona watu wanasema wengine wanaandamana mioyoni.

Mheshimiwa Spika, ni vizuri huo mwongozo uliotoa ukautoa na kwenye Wizara. Haya malalamiko ya kila siku, hili gazeti ni la nani? Linasukumwa na nani? Nani yuko nyuma ya chombo hiki cha habari? Kama kuna ukweli, hatua zichukuliwe siyo kunyamaza kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. (Makofi)