Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii; na jina langu ni Shally Josepha Raymond, lakini kwa vile baba yangu alikuwa anaitwa Joseph, mkiita hivyo naitika na nakubali pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu sana kwamba ametuweka wote hapa tuweze kuzungumzia mambo ya maendeleo ya nchi yetu. Kipekee naomba shukrani hizi ziwafikie wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro ambao ndio walionipigia kura nikaingia hapa kupitia Viti Maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumzia Wizara ambayo ni nzito na Wizara ambayo kwa kweli Ilani ya CCM inazungumza wazi kwamba sasa twende kwenye uchumi wa viwanda kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Iko kwenye ilani! Mwasilishaji wa hotuba hii, Waziri wetu yuko makini na ni mzungumzaji mzuri, ameongea kwa makini, wataalam wameandaa hotuba vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla yangu amezungumza Mwenyekiti wa Kamati hii, na mimi niseme kwamba naungana naye na yote aliyosema, lakini na mimi nataka nihoji kupitia kwako Mwenyekiti, Kamati ilipokaa ilikuwa na nia nzuri na imetuambia, ila kuna mambo magumu nimeyaona kwenye taarifa ya Kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna shida ya uwasilishwaji wa fedha za maendeleo. Hadi kufikia mwezi huu wa tatu walikuwa wamepewa shilingi bilioni moja tu. Sasa shilingi bilioni 1.6 kwa viwanda vya Tanzania nzima, itafanya nini? Nirudi pia kwa Waziri wangu, yeye leo hapa amekuja na kitabu chake hiki, anatuomba hapa tumpitishie shilingi bilioni 81.8, Tanzania nzima! Hivi kweli fedha hiyo ndiyo italeta mabadiliko ya viwanda? Haifiki hata trilioni moja! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipitia hiki kitabu cha Mpango wa Maendeleo, nikidhani kwamba labda hiyo ndiyo Wizara iliyopewa fedha nyingi kutokana na mabadiliko tunayotarajia, lakini nikakuta hapana, kuna Wizara ambazo zimepewa mpaka shilingi trilioni tatu. Sasa hii Wizara ya Viwanda na Biashara inashindikana nini kuipa hata shilingi trilioni mbili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuwaombea fedha ili hii mipango mizuri iliyoainishwa kwenye kitabu hiki iweze kutekelezeka. Niseme wazi kuna jambo ambalo linanikera. Wakati sisi huku tunawaombea fedha au tunaona kwamba fedha hii haitoshi, Mawaziri wetu wanatuambia hiyo hiyo, tutaenda kigumu kigumu! Hii siyo kazi ya mtu! Ni kazi ya nchi hii, sisi tumeona, na ninyi mnatakiwa mwone! Fedha hii haitoshi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye miaka ya 1980, SIDO ilikuwa inafanya vizuri sana nchini. SIDO zikuwepo katika Mikoa yote na sasa hivi SIDO zimebaki mfumfu tu, haziko vizuri. Sasa najua tunapoongelea viwanda, kuna viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. Mimi kwa ajili ya ajira ya vijana wetu, naomba nibaki kwenye viwanda vya kati au vidogo kiasi ili nianzie hapo SIDO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Mkoa una eneo la SIDO limetengwa na wapo sasa watu wanafanya shughuli kule ndani ya SIDO, lakini Serikali kiasi imetoa mkono wake. Mimi nilikuwa naomba maeneo haya ya SIDO na viwanda hivi vilivyokuwa vimeanzishwa kwenye SIDO, sasa vifanyiwe kazi maalum ya kivifufua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shughulil za viwanda, wengi tunazungumzia tu mashine, lakini nguvu kubwa ya kiwanda ni rasilimali watu, na sisi watu tunao. Tunao vijana wetu ambao wanatafuta ajira. Ndiyo maana unakuta hata zile nchi zinazoendelea, zinatafuta nchi ambayo ina labor, yaani cheap labor inakwenda kufanya huko viwanda vyao. Sisi iko hapa hapa, tunataka kufanya viwanda hapa. Kwa hiyo, tuna hao vijana watakaopata ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumbukumbu zangu sahihi kabisa, kila kitu kilikuwa kinapatikana SIDO, vijiko vizuri vya SIDO, makufuli mazuri ya SIDO, vitasa vizuri vya SIDO, makarai, mabeseni, leo imekuwaje? Kwa nini hatuvipati vitu hivyo? Eti tunaagiza, tunataka vitu imported, vitusaidie nini? Matokeo yake ndio hata vitu vingine tunaishia kwenye mitumba, wenzetu wamechoka wametupa, sisi tunaletewa huku, hapana!
Naomba kupitia kwako, Wizara hii isimamie SIDO, vijana wetu wapate ajira na ndiyo hiyo sasa tuanze kuona tunafufua viwanda kwa hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanda vikubwa ambavyo vilikuwa nchini na bado baadhi vipo. Wakati huo nitoe mfano wa Kiwanda cha Kuzalisha Sukari (TPC), kiwanda cha kuzalisha sukari. Ajira yake ni watu 5,000, lakini haikuishia tu ajira, kiwanda hicho kilikuwa pia kina training school. Wale vijana wanakuwa trained pale, wanakuwa na shule ya kuwafundisha, wanaweza kuchonga vyuma, wanaweza kukarabati vyuma hivyo, wanaweza kuvitumia. (Makofi)
Sasa nilikuwa naomba kila mwekezaji anayekuja akaweka kiwanda, awe pia na nafasi ya ku-train vijana wetu ili wawe ni watu ambao wana ujuzi katika jambo lile linalofanyika. Hili linaweza kufanyika pia kwenye viwanda vya sementi, bia labda na viwanda vingine. Pia kwenye hicho kiwanda cha TPC ningependa pia wafufue ile training school.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi nyumbani. Naelewa kwamba charity starts at home. Mimi nitokako ni Kilimanjaro, viwanda vyetu vyote vimekufa, sasa hivi tunacho hicho kiwanda kimoja cha TPC na labda kile cha Bonite ambacho ni private na kiwanda kingine ambacho kipo ni kiwanda kidogo tu cha kutengeneza bia. Tena ni bia ya Serengeti maana ile Kibo imeshakufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Rais anapita katika kampeni zake za kuomba kura za Urais, alisema haitachukua muda mrefu viwanda vyote vitafufuliwa. Kwa haraka haraka naomba nivitaje tu; najua haviwezi kufufuliwa mwaka huu au mwaka ujao, lakini ianze sasa basi process ya kifufua. Tuna Kilimanjaro Machine Tools, tuna Kiwanda kile cha Magunia na hiki ni kiwanda muhimu kwa sababu pale Kilimanjaro ni wakulima wa kahawa na hii kahawa haiwekwi kwenye gunia lingine labda kama la sulfate, hapana, unyevu utabakia. kwenye kahawa. Gunia moja tu linalofaa kuweka kahawa ni lile la jute. Kwa hiyo, bado kuna soko la magunia hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri wangu ajue kwamba sasa kuna kazi kufufua kile Kiwanda cha Magunia. Haiishii hapo, pia kuna Kiwanda cha Ngozi. Kwenye kiwanda cha ngozi, kuna private sector ambayo kuna muhindi, ni Shaha Industries, anatengeneza vifaa vya ngozi ila umeme unakuwa ni shida na pia kodi zimemuwia ngumu amefunga, aweze pia kuzungumza naye ili kiwanda hicho kifunguliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tuna shauku kubwa, tuna hamu ya kuona kwamba tunapiga hatua. Naomba nimtakie kila la heri na ninaunga mkono hoja. Ahsante.