Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake wa kutukuka kwa Watanzania. Nawapongeza pia Mawaziri, Mheshimiwa Suleiman Saidi Jafo na Kapteni Mstaafu Mheshimiwa George H. Mkuchika na Manaibu Waziri wote Mheshimiwa Josephat Kandege, Mheshimiwa Mwita Waitara na Mheshimiwa Dr Mary Mwanjelwa kwa kazi kubwa wanazozifanya usiku na mchana kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya Shule za Msingi na Sekondari. Shule nyingi za msingi zimepatwa na ongezeko kubwa la wanafunzi, udahili wa wanafunzi wa darasa la kwanza umeongezeka. Ongezeko hili limesababisha upungufu mkubwa wa madarasa, hivyo, Serikali iongeze fedha za ujenzi wa madarasa. Wananchi hasa wa maeneo ya vijijini hawana uwezo wa kumudu kujenga madarasa mfano katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, shule nyingi hasa zilizojengwa zamani hazina madarasa ya kutosha, naiomba Serikali itusaidie au ituongezee fedha za ujenzi wa madarasa hata kwenye shule zilizojenga nyuma ya miaka ya 1970. Mfano wa shule kongwe ni Sovi (1950s), Lupembe (1950s) na Kanikelele (1970). Majengo ya shule hizo za msingi yamechoka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa sekondari ni muhimu sana shule zetu za sekondari za kati, kujengwa mabweni kwa ushirikiano wa Serikali na wananchi. Shule nyingine za kata hazina mabweni na majengo mengineyo muhimu kama vile majengo ya utawala na mabwalo ya chakula. Uwepo wa majengo hayo huongeza ufaulu wa wanafunzi. Wanafunzi wanakuwa huru kusoma wanapoishi bwenini na ufaulu wao huongezeka. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe shule ambazo hazina mabweni ni Shule za Sekondari ya Ninga, Ikuna na Mlunga, Kidegembye (bweni la wavulana), Lupembe (mabweni yaliyojengwa zamani (yamechakaa), Sovi (bweni la wavulana) na Itipingi (hakuna mabweni ya A-level).

Mheshimiwa Naibu Spika, Ukusanyaji wa Mapato; Halmashauri nyingi hazikusanyi mapato au zinakusanya chini ya makadirio, Halmashauri nyingi zinakusanya chini ya asilimia hamsini hii inatokana na:-

Moja inawezekana kuna uzembe wa ukusanyaji mapato na kupelekea kukusanya chini ya kiwango; au Pili, inawezekana wataalam waliopo katika Halimashauri zetu wanashindwa kubuni miradi ambayo itawaingizia kipato cha uhakika sambamba na hali ya Halmashauri zao au kutegemea vyanzo hivyo bila kutabiri uendelevu na vyanzo hivyo. Mfano wa Halmashauri za Mikoa ya Katavi, Kigoma, Mtwara na Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TASAF; naipongeza Serikali kwa kuendelea kuzisaidia kaya zenye kipato kidogo kupata mahitaji ya msingi na kuwawezesha kujikwamua kwenye wimbi la umaskini kupitia mpango wa TASAF. Kuna baadhi ya vijiji havikuingizwa kwenye mpango wa TASAF, tunaomba vijiji hivyo viingizwe kwenye mpango huu ili kuondoa malalamiko. Mfano, katika Halimashauri ya Wilaya ya Njombe kuna Kijiji cha Sovi kilirukwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), wanafanya kazi kubwa sana. Watanzania zaidi ya asilimia 75 ni wakulima, kwa hivyo barabara za vijijini ndiyo tegemeo kubwa sana kwa wakulima hawa. Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ina jumla ya barabara za vijijini zenye urefu wa kilomita 582. Eneo la Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ni eneo la uzalishaji wa mazao mbalimbali kama vile chai, kahawa, miti ya mbao na nguzo, mahindi, maharage, nanasi, parachichi na mihogo. Mazao mengi kati ya hayo huzalishwa wakati wa mvua nyingi na ni kipindi hicho barabara hizo huharibika sana na kukwamisha shughuli za uzalishaji na usafirishaji wa mazao hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili barabara hizi ziweze kufikika na mazao kufikia kufika sokoni, ni muhimu kutenga fedha za dharura ili kufanya matengenezo ya muda kwenye barabara hizi hasa kwenye maeneo yenye mvua nyingi kama Jimbo la Lupembe. Mwaka huu kutokana na mvua kubwa iliyoanza kunyesha Mwezi Februari, mpaka sasa barabara nyingi hazipitiki. Kuna baadhi ya maendeo hata madaraja yamekatika mfano barabara ya Lole – Maduma na Kidegembye – Image. Madaraja ya barabara hizi yanatakiwa kujengwa upya, hivyo ni muhimu Serikali kuwaongezea bajeti Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) ili kusaidia kuchochea uchumi wa halmashauri na mkoa kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja za Wizara zote mbili.