Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba na mimi niweze kuchangia kidogo, lakini naomba nianze na suala la vitambulisho vya ujasiliamali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka labda nijue kwa sababu Serikali iko hapa, kwa sababu mchakato wa vitambulisho vya wajasiliamali halikuletwa Bungeni, tumeona Mkuu wa Nchi, Rais amewaita Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya Dar es Salaam amewapatia vitambulisho na kwenda kuvipeleka kwenye Mikoa au kwenye Wilaya ili waende kuuza shilingi 20,000/=. Sasa swali langu ambalo naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha atuambie, kitambulisho kimoja kilitengenezwa kwa shilingi ngapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ambalo nitaomba anijibu baadaye atakapokuwa anahitimisha, atuambie Mheshimiwa Rais alipokuwa anasema kuanzia wajasiliamali wa mtaji wa shilingi milioni nne kushuka chini, alikuwa anamaanisha kwamba kushuka chini hadi shilingi ngapi? Je, hata mwenye mtaji wa shilingi 500/= naye anahusika? Kwa sababu kuna akina mama ambao wanauza nyanya mafungu mawili; ana mtaji wa shilingi 1,000/= leo anaambiwa akalipe kitambulisho cha shilingi 20,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mama mwingine anauza nyanya chungu, ana mtaji wa shilingi 500 anaambiwa naye alipe kitambulisho cha shilingi 20,000/=. Sasa je, ilikuwa shilingi milioni nne hadi shilingi ngapi? Hapa Mheshimiwa Waziri atatuambia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo naomba Mheshimiwa Waziri atuambie, je, tenda ilitangazwa ili kupata yule atakayetengeneza vitambulisho? Kama tenda hii ilitangazwa, ni nani aliyeshinda? Kama tenda haikutangazwa, tafsiri yake ni kwamba kuna makosa yanayofanyika inawezekana vitambulisho vya ujasiliamali likawa ni dili la mtu na Bunge sisi tusijetukatumika kama rubber stamp kupitisha mambo ya mtu binafsi. Kwa hiyo, tenda ilitangazwa? Nani aliyeshinda kwenye tenda hii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine niseme tu kwamba ukweli ni kwamba sisi wote tunafahamu ukienda leo kule Mbozi kwa mfano pale Mlowo au ukaenda kule Kijijini Igambo au Hampangala akina mama wanahangaika sana. Hii imekuwa kama ni kodi ya kichwa imerudishwa. Leo mama mmoja anauza nyanya kwenye nyumba moja, anaambiwa alipe shilingi 20,000/=; baba anauza miwa, anaambiwa alipe shilingi 20,000/=, mtoto mwingine anauza bamia, alipe shilingi 20,000/=, mtoto mwingine anauza nyanya chungu shilingi 20,000/=. Nyumba moja shilingi 80,000/=. Sasa hii ni zaidi ya kodi ya kichwa. Kama Serikali imeleta kodi ya kichwa, wawaambie Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua wewe unatoka kule Rungwe, wapo akina mama wanaohangaika. Kama leo wamerudisha kodi ya kichwa Bunge hili liwaambie kwamba kodi ya kichwa imesharudishwa na hii Wabunge hatutakuwa tayari kukubali suala hili la kodi ya kichwa kurudishwa kwa mara nyingine tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, leo Serikali ilisema kwamba itapeleka shilingi milioni 50 kila kijiji. Badala ya kupeleka shilingi milioni 50 ya kila kijiji, imeenda kuwadai watanzania wote shilingi 20,000/=. Kwa sababu kama Serikali iliahidi shilingi milioni 50, kwa nini hazijapelekwa? Badala ya kuzipeleka, imeanza kuchukua shilingi 20,000/= kwa kila Mtanzania, kwa sababu nchi hii imewaambia hadi wapiga debe, makonda, wanaoziba pancha za baiskeli, kila mtu. Sasa hali hii ni mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, amezungumza dada yangu hapa Mheshimiwa Suzan Kiwanga, naomba haya maneno ya kuhusu ndugu yangu Jenerali Mabeyo Mkuu wa Majeshi, nimeyanukuu hapa; ili mkisema kwamba kama kuna ushahidi, nimeyanukuu yapo hapa na ushahidi upo. Katika baadhi ya maneno yake alisema kwamba, “ndani ya nchi yetu kwa kushirikiana na vyombo vingine, tutawalinda wananchi na mali zao, tutakabiliana na matishio ndani ya nchi yetu na sasa hivi tunaendelea kufuatilia kauli tata zinazoashiria uchochezi na machafuko ndani ya nchi yetu.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kulinda wananchi na mali zao ni kazi ya Jeshi la Polisi, siyo kazi ya Jenerali Mabeyo. Siyo kazi yake hii. Maana yake kama anataka uteuzi kuwa IGP, atuambie ili Rais amwondoe kwenye nafasi yake… (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: …ya Mkuu wa Majeshi ampeleke kuwa IGP. Maana yake hii siyo kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yeye kazi yake ni kulinda mipaka ya nchi hii. Siyo kazi hii… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)