Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. MUSSA BAKARI MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Na mimi kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha na mimi leo kusimama hapa kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Vilevile nitakuwa ni mchoyo wa shukrani kama sikuwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo langu la Tanga Mjini ambao kwa mara ya kwanza wamebadilisha historia ya Tanzania kwa kupatikana Mbunge wa Upinzani katika Jimbo la Tanga iliyokuwa ngome kuu ya CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia viwanda, biashara na ubinafsishaji. Kwanza nisema bila umeme wa uhakika basi Tanzania ya viwanda itakuwa ni ndoto za alinacha. Nasema hivi kwa sababu nchi yetu imekuwa kama nchi ya kufikirika. Baada ya kugundulika gesi na makaa ya mawe tumekuwa tukiambiwa kwamba umeme kukatikakatika utakuwa kama historia ya vita ya Majimaji iliyopiganwa mwaka 1905 lakini leo umeme umekuwa hauna uhakika, humu humu ndani ya Bunge pia umeme unakatika, sasa sijui Tanzania ya viwanda itakuwa ni Tanzania ipi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba viwanda, biashara, reli na barabara ni vitu vinavyoambatana. Imefika mahali sisi Tanzania tumekuwa tunafanya vichekesho, kwa nini? Leo reli inayotoka Tanga kuja kuungana na reli ya kati imekufa, lakini vilevile pia viwanda vingi, hakuna asiyejua kwamba Tanga ulikuwa ni mji wa viwanda. Tulikuwa na Kiwanda cha Chuma – Steel Rolling Mills, tulikuwa na kiwanda cha Sick Saw Mill, tulikuwa na Kiwanda cha Mbolea, tulikuwa na Kiwanda cha Kamba – Ngomeni, tulikuwa na NMC, tulikuwa na karakana kubwa ya reli, vyote hivyo vimeuliwa chini ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, kutokana na kufa viwanda hivi, leo Mji wa Tanga umekuwa hauna ajira. Tukumbuke Tanga ulikuwa siyo mji wa mazao ya vyakula, ilikuwa ni mashamba ya mkonge nayo pia yamekufa. Sasa imefika mahali Tanga umekuwa kama mji ambao ulikuwa na vita kama Baghdad vile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia kuuliwa viwanda vya Tanga matokeo yake sasa miaka 55 baada ya uhuru Tanzania leo tunaongoza kwa kilimo cha pamba lakini nepi za watoto wachanga made in China. Sindano ya kushonea kwa mkono made in China! Vijiti vya kuchokolea meno (tooth pick) made in China! Miti ya kuchomea mishikaki pia made in China! Basi hata handkerchief pia! Bado tukikaa humu ndani tunajisifu kwamba sisi tuna viwanda na tunataka kuifanya Tanzania ya viwanda, mimi sikubaliani na suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasema kama tunataka kuifanya Tanzania ya viwanda kwanza tufufue vile viwanda vingi vilivyouliwa katika mji wa Tanga! Hakuna asiyejua, ukienda Tanga, Muheza ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya matunda hususan machungwa lakini leo tunanunua packet ya juice kutoka Saudi Arabia kwa shilingi 5,000. Hakuna asiyejua kwamba ukienda maeneo ya Hale na Korogwe kuna maembe ya kutosha lakini hakuna hata viwanda vya ku-process matunda hayo tukaweza kuuza sisi katika nchi nyingine. Leo matunda na juice zote zinatoka nje wanaoleta huku wanachukua pesa zetu za kigeni wakaenda kununulia. Unapokuwa una-import zaidi kuliko ku-export maana yake unajikaribishia umaskini lakini wenzetu hilo hawalioni! Anayezungumza hapa ataanza kupongeza, ataanza kusifu Ilani ya Chama cha Mapinduzi lakini yanapoharibika hasemi kwamba ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi ndiyo inayoharibu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mimi nashangazwa, mbona nchi nyingi duniani zinafanya maendeleo lakini hawataji ilani za chama! Kenya shule zinajengwa, maabara zinajengwa, ukienda Malawi barabara zinajengwa na maendeleo mengine yanafanyika lakini watu hawataji Ilani ya Chama! Mimi naona tatizo hapa ni Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, lazima tubadilike, Serikali yoyote inayokusanya kodi kazi yake ni kurudisha kodi hiyo kwa kuwapelekea wananchi maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye suala la biashara, Watanzania leo wamekuwa wakihangaika hususan akina mama, ukienda katika kila nyumba sasa hivi katika mikoa yetu na miji yetu mikuu, kila nyumba ina frame za maduka kwa sababu ajira hakuna na viwanda hakuna. Leo akina mama ndiyo wanaolea familia, wanahangaika wanafungua biashara lakini cha kushangaza sheria ya biashara ya Tanzania ni tofauti na sehemu nyingine. Kawaida ya biashara, mfanyabiashara anapoanza biashara upya lazima apewe tax holiday ili ajiweke vizuri aweze kupata faida alipe kodi. Hata hapa ndiyo sheria inavyosema kwamba usilipe kodi kabla ya kupata faida lakini Tanzania mtu anakwenda TRA akishapata TIN Number anafanyiwa assessment, analipa kodi kabla hajafanya biashara! Matokeo yake sasa akina mama wanaokopa mikopo katika taasisi za kifedha kama BRAC, Poverty Africa na wengine wamekuwa wakichukuliwa vyombo vyao, wamekuwa wengine wakijinyonga na wengine wamekuwa wakikimbia familia zao kwa kuogopa madeni wanayodaiwa na taasisi za fedha. Sasa kwa nini Serikali yetu haiwasaidii wananchi wake katika biashara? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda Rwanda na Burundi anayekuwa na nia ya kufanya biashara baada ya mtaji aliokuwa nao Serikali inamuongezea fedha na kuambiwa kwamba tunakuongezea fedha uajiri Waburundi wenzako au Warwanda wenzako wawili usaidie kukuza ajira katika nchi yetu lakini Tanzania ni kinyume. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, nakuomba ulizingatie hili, Tanga viwanda vingi vimeuliwa, hususan reli. Panazungumzwa hapa reli ya kati itajengwa katika kiwango cha standard gauge, lakini Waswahili wana usemi wao wanasema, mwiba uingiapo ndiyo unapotokea hapo hapo. Reli ya kati ilianza kujengwa na Wajerumani katika miaka ya 1905 na ilianzia Tanga, vipi leo twataja reli ya kati ijengwa kuanzia Dar es Salaam! Tumesahau kwamba mwiba uingiapo ndio utokeapo? Mimi naomba kama reli ya kati inataka kufanyiwa ukarabati basi ianzie Tanga, Bandarini pale ambapo ndio reli ilipoanzia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nalotaka kusema, tumeambiwa hapa na wazungumzaji wengi kwamba viwanda vilifanyiwa ubinafsishaji na vingine kuuzwa. Amesema Mheshimiwa Lijualikali kwamba kule kwake kuna mbuzi katika kiwanda cha sukari lakini hata Tanga kwenye kiwanda cha chuma! Cha kushangaza walikuja wawekezaji wa Bulgaria, wakaja Wajerumani wakataka kiwanda kile cha chuma lakini matokeo yake wakanyimwa, wakapewa wawekezaji waliotakiwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Matokeo yake sasa kiwanda kile imekuwa ndani kunafugwa mbuzi napo kama vile ilivyokuwa Morogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda cha chuma cha Tanga kilikuwa kinazalisha two products same time, kulikuwa pana misumari bora kabisa katika Afrika Mashariki na nondo zinazozalishwa Tanga zilikuwa ni bora. Sasa na mimi najiuliza, chuma bado kinahitajika siku hadi siku katika ujenzi wa maghorofa, katika ujenzi wa madaraja lakini hata katika body za magari, inakuwaje kiwanda cha chuma kipate hasara mpaka kife? Huu ni ushahidi kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeshindwa kusimamia viwanda vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme Mheshimiwa Waziri, hoja yako siiungi mkono naunga mkono hoja iliyotolewa na Upinzani lakini kwanza iangalie Tanga! Katika viwanda vingine usisahau viwanda vya matunda, Tanga ni mji unaozalisha matunda kwa wingi, tunahitaji viwanda vya matunda navyo vijengwe Tanga ili Tanga iweze kurudia hadhi yake kama zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nikumbushe historia kidogo, hata ukiangalia jina la nchi hii kabla ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar ilikuwa inaitwa Tanganyika. Sasa hebu angalia Tanga ilivyokuwa na umuhimu katika nchi hii, Tanga na nyika zake ndio tukapata hii Tanganyika lakini bado watu wamesahau historia kwamba Tanga imechangia mchango mkubwa katika kuleta uhuru wa nchi hii, leo Tanga imekuwa imeachwa kama mtoto yatima! Hata ukiangalia bajeti ya mwaka huu 2016/2017, Tanga tuna mambo mengi ambayo tumeachwa, tutakuja kuzungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata vilevile pia katika huo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar palikuwa pana mahusiano mazuri sana kati ya watu wa Zanzibar na watu wa Tanga na hususan katika masuala ya kibiashara. Mpaka leo watu wanaingiliana katika biashara, watu wanawekeza upande wa Bara na Visiwani, lakini Serikali imekuwa haitii nguvu kwa hawa wafanyabiashara ambao ni wazalendo.
Vilevile pia tumeacha sasa kuikumbuka na kuisaidia Tanga kwamba ndio yenye historia ya uhuru wa nchi yetu, lakini tunaomba Mheshimiwa Waziri asisahau kwamba hata yeye yawezekana akawa ana jamaa zake na ndugu zake Tanga, kwa nini? Kwa sababu Tanga ulikuwa ni mji wa viwanda, uliweza kukusanya makabila yote ya Tanzania 122 lakini hata nchi jirani kutoka Burundi, tunao Warundi wengi kule, kutoka Malawi tunao watu wanaitwa Wanyasa kule, kutoka Kenya, Uganda, Zambia watu walikuja kufuata ajira Tanga, sasa inakuwaje viwanda vya Tanga vife. Mimi naomba kama Waziri una nia ya kweli ya kuifanya Tanzania ya viwanda hakuna haja ya kujenga viwanda vipya, tukifufua viwanda vya Tanga peke yake na maeneo mengine ya Tanzania kweli tutakuwa Tanzania ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa kabisa tusisahau kwamba bila ya umeme wa uhakika viwanda vitakuwa ni kama vile mchezo wa alinacha. Lazima kwanza tuwe na umeme wa uhakika, iwe tuna dhamira ya kweli kwamba kweli tumegundua gesi, tumegundua makaa ya mawe lakini hata upo umeme pia wa upepo lazima tushirikishe umeme wote huo. Wenzetu wa baadhi ya nchi kama Ujerumani pamoja na ukubwa wake wanatumia solar power system na sisi kwa nini hatuna mpango wa muda mrefu wa Serikali wa kujenga mtambo mkubwa wa umeme wa kutumia solar power system? Kama tuki-fail katika hydro-electric power twende katika gesi, Kama kwenye gesi tumeshindwa, tungekwenda katika solar power. Sasa Waziri unapozungumzia viwanda bila ya kutuhakikishia kwanza kwamba tuna umeme wa uhakika, mimi hapo inakuwa sielewi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri, hakuna haja ya kujenga viwanda vipya, tufufue viwanda vingi zaidi ya 70 vilivyokuwa Tanga ambavyo vimekufa lakini tufufue na viwanda vingine ambavyo vya zamani kama alivyotaja Mheshimiwa mmoja kiwanda cha Nyuzi Tabora na vinginge ili tuweze kufikia maendeleo ambayo Watanzania wanayatarajia.