Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana nami kunipa nafasi niweze kuchangia kidogo hotuba hizi mbili ambazo ziko mbele yetu. Sababu ya muda mdogo, naomba moja kwa moja nianze na suala la upungufu mkubwa sana wa watumishi na hasa kwenye Sekta ya Afya na Sekta ya Elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli kati ya kitu sasa hivi ambacho kinadumaza elimu, pamoja na ongezeko kuwa la watoto katika mashule yetu, ni suala la upungufu wa walimu kwenye mashule yetu. Wakati enrollment inaongezeka, wakati madarasa yanaongezeka, wakati shule zinaongezeka, walimu hawaongezeki kwa speed ile ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya yetu ya Kaliua, mwaka huu tumefungua shule nne za sekondari; mwaka huu huu tumefungua zahanati nne, mwaka huu huu tumefungua primary school mikondo sita. Walimu wanahamishwa kutoka kwenye maeneno yenye upungufu, wanapelekwa kwenye shule mpya. Kwa hiyo, kwenye tatizo unaongeza tena tatizo lingine, una-create gap pale, unawapeleka kwenye shule nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunataka watoto wetu wapate elimu nzuri, ni lazima tuhakikishe kwamba ongezeko la watoto linakwenda sambamba na ongezeko la walimu, ni muhimu sana. (Makofi)

Leo shule moja ina madarasa saba inakuwa na walimu tisa, wanagawanaje hayo masomo waweze kufundishwa? Zahanati inakuwa na watumishi watatu au wanne na wakati mwingine katika maeneo mengine mpaka watumishi wawili. Mmoja akiugua, au kama ni mtu na mke wake ameugua, au amesafiri, zahanati haifanyi kazi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Utumishi, lazima tuwe na mpango mkakati kabisa wa makusudi ya dhati, kuongeza watumishi na hasa kada hizi mbili, elimu na afya, ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, akina mama wengine, nilisema tena hapa, wanajifungulia kwenye zahanati, hakuna wahudumu; na mhudumu huyu anachoka. Yeye ni binadamu, anatumia damu, hatumii maji. Tunaomba suala la upungufu ya kada hizi mbili ni muhimu mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua mwaka 2018 wilaya yetu imepata watumishi 16; ni wachache sana sana kwenye kada ya afya kwa sababu wamekwenda kuongezwa, kwenye zahanati kulikuwa na wawili, akaongezwa mmoja. Kwa hiyo, bado tatizo liko pale pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi bado tunakwenda kuongeza kujenga zahanati, vituo vya afya, tunaongeza shule, tunaongeza madarasa, lakini tatizo la upungufu wa walimu ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la walimu wa sayansi. Hivi kwa kweli, sasa hivi sijui ni percent ngapi, sijafanya utafiti wa kutosha; lakini shule nyingi, tumejenga maabara na ni agizo la Serikali. Maabara zile hazitumiki, hakuna walimu wa sayansi. Tunakwendaje kwenye uchumi wa viwanda wakati hatuna walimu wa sayansi, hatuna walimu wa biology, walimu wa physics na chemistry? Haiwezekani kwenda kwenye uchumi wa viwanda wakati hatupeleki walimu wa sayansi kwenye mashule yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine mwaka jana, mwaka juzi 2017/2018 Serikali ilipendekeza shule moja katika kila wilaya kupokea watoto wenye mahitaji maalum kwa maana ya watoto walemavu, wenye mahitaji yote, walemavu wa viungo, viziwi wote wamepokelewa pale. Cha ajabu shule zile miundombinu ile siyo rafiki kwa watoto wale, wamepelekwa pale wanapata mazingira magumu sana, hawapati elimu kama watoto wenzao, hawajapelekewa vifaa vya kuweza kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikupe mfano mmoja, sisi Kaliua shule iliyopendekezwa ni Kaliua Primary School, ina watoto 2,295, shule moja, wale watoto wanatumia kaofisi kadogo tu kalikokuwa kakatahapo pembeni.Kwa hiyo ni tatizo. Sasa kama lengo lilikuwa ni kuwasaidia, maana yake kilio chetu hapa Bungeni ilikuwa ni kwamba, watoto wale wamesahaulika, wako majumbani, lakini ni Watanzania wanahitaji elimu kama wengine, Serikali ikaamua kuwasaidia kwa kuwa hatuna shule maalum nyingi kwenye mikoa yetu watenge shule moja. Akili yangu ilikuwa ni kwamba, Serikali ingepeleka nguvu kubwa kwenye zile shule, kujenga miundombinu, kuweka Walimu, kuweka vifaa wale watoto wapate elimu ndani ya maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti,kwa kweli lengo lilikuwa jema, lakini leo kilichofanyika ni kuwaacha katika mazingira yale, kwa kweli hatuwatendei haki. Naiomba Serikali ihakikishe lengo lake lililokuwa la kuweka zile shule kuzitenga litimie kwa kuweka miundombinu ya kutosha, miundombinu rafiki, watoto wanatambaa chini kwenda kwenye zile mashule, wana-share vyoo na wale watoto wengine na wenyewe ni walemavu, siyo haki kabisa! Wengine walikuwa viziwi, wamekaa pale mpaka mwisho wameondoka hakuna Mwalimu wa kuwasaidia. Tuwatendee watoto hawa haki, hawakupenda kuzaliwa walemavu, ni Watanzania wenzetu, wana haki sawa kama watoto wengine ambao wamezaliwa bila kuwa na upungufu wowote.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la TASAF;nakumbuka TASAFthree ambayo tunaenda nayo sasa hivi ya kunusuru kaya maskini ilianza mwaka 2013, maeneo mengine kama Kaliua 2014. Huu mradi ulikuwa ni miaka mitano, tulivyokuwa tumeelezwa pamoja na upungufu kwamba kwenye hivyo vijiji ambavyo wamepewa wachache wengi pia hawapati lakini tulitegemea baada ya miaka mitano waingie wapate tena vijiji ambavyo vilikosa. Leo hakuna majibu yoyote tunayopewa na Serikali nimeuliza suala hili tangu Mheshimiwa Kairuki akiwa Waziri, hatupati majibu, ni lini vilevijiji ambavyo havijawahi kuingia kwenye TASAF vitaingia kwenye TASAF? Imekuwa ni double standard, kuna wazee ambao hawajiwezi kabisa, kuna walemavu hawajiwezi, wanaona kijiji jirani kuna msaada wanapata japo ni kidogo, yeye hapo alipo kijiji hicho hicho jirani hapo pembeni hapati chochote kwa miaka yote, kwa nini Serikali isione kwamba hii ni fursa kwa wote? Kama suala la kusaidia kaya maskini zipo kote, basi baada ya miaka mitano mradi huu ueleweke kwenye vijiji tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa tupate majibu kwa Mheshimiwa Waziri atakavyokuja kujibu kwamba mradi wa TASAF ambao ulikuwa umalizike waweze kupeleka na kwenye vijiji ambavyo vilikosa, Kaliua tulipata vijiji 36 tu, tuna vijiji vingine kwa maana ya Jimbo la Kaliua 36 tu, bado vijiji vingine 26 hawajapata. Kwa hiyo tulikuwa tunategemea kwamba wangeweza kupata kama wengine, kwa kweli wanaumia wazee wale wanasikitika kwa sababu wanaona kwamba Serikali imewaona wenzao wa vijiji jirani wao imewasahau na ukizingatia hapa kwamba hakuna mpango wowote wa Serikali kusaidia wazee popote, hata wale ambao wana nguvu ya kufanya kazi, hakuna mfuko maalum wa kuwasaidia. Kwa hiyo tunaomba TASAF ihakikishe kwamba imeangalia wale wengine ambao pia hawakuingia kwenye Mfuko huu wa TASAF kwa awamu ile ya kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu lingine na la mwisho ni suala la lishe. Suala hili ni muhimu sana, nilikuwa nasoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri; suala la lishe hapa Tanzania kwa takwimu za mwaka 2016/2017 watoto chini ya miaka mitano wenye udumavu ni watoto asilimia 34, ni wengi kweli kweli. Nilikuwa nategemea tupewe takwimu update, tupewe takwimu za 2017/2018, 2018/2019 tujue current situation, udumavu kwa sasa hivi ni asilimia ngapi. Hata kwa takwimu za miaka mitatu iliyopita asilimia 34 kwa watoto chini ya miaka mitano suala la lishe ni muhimu kuliko maelezo, mtoto anapodumaa akiwa chini ya miaka mitano, anadumaa totallykuanzia fikra zake, mawazo yake, uelewa wake,darasani hafundishiki, ni tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ukiangalia bajeti iliyotengwa na Serikali bado ni kidogo sana, haiwezekani tunatengeneza Taifa la kesho, hawa ndiyo Marais wajao, ndiyo Mawaziri wajao, ndiyo Wabunge wajao, Wakurugenzi wajao, wanakua wakiwa wanaudumavu wa akili, tunawapeleka wapi.(Makofi/)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka pia niseme kwamba suala la kuangalia suala lishe siyo kutoa matone ya damu, siyo kutoa matone ya vitamini A na dawa za minyoo tu, hapana. Suala la lishe ni chakula pia na bahati mbaya ukiangalia maeneo ambako watoto wamepata utapiamlo na udumavu wa akili kwa maeneo mengi hasa utapiamlo ni mikoa ambayo wanalima vizuri sana, wanafuga vizuri, leo Mkoa wa Kilimanjaro siyo mkoa ambao tunatakiwa tuwe na udumavu wa akili wala kuwa na utapiamlo, lakini ukiangalia utapiamlo upo mwingi, kwa nini hakuna elimu. Pia ukiangalia bajeti nzima ya Mheshimiwa Waziri hakuna sehemu wamesema watawekeza kutoa elimu namna gani wazazi wawape watoto vyakula vyenye kujenga lishe yao, hawaangalii.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali suala la kutoa matone ya vitamini A nakubaliana nalo, pamoja na kutoa dawa za minyoo, lakini suala kubwa kabisa ni chakula nyumbani. Ukimpa mtoto dawa ya minyoo kamanyumbani alivyokula vitaminiataendelea kudumaa tu, kwa sababu hiyo haimsaidii sana.Vile vile Mkoa wa Tabora tunalima mahindi, tunalima maharage, tunalima karanga, tunalima alizeti vyakula vyote vyenye vitamini vipo, iweje watu wapate utapiamlo au udumavu wa akili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kilimanjaro wanalima, Kilimanjaro wanafuga watu wanakula mayai, maziwa, lakini maziwa yanauzwa mtoto hanywi, mayai yanauzwa,mtoto hali, matokeo yake watoto wanadumaa.Tusiliangalie Mheshimiwa Waziri kama suala dogo, ni suala kubwa kwelikweli, ndiyo maana tunakuja kuwa na Taifa la watu ambao hawafikirii vizuri, hawawazi vizuri, hawawezi ku-deliver kwa sababu udumavu umeanzia kwenye utoto wake.

MWENYEKITI:Ahsante sana.

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii.(Makofi)