Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Joseph Osmund Mbilinyi

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbeya Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi nami niweze kuchangia hotuba hii. Kuna msemo unasema Conversation rules the Nation. Ni two ways game; ukipenda kusikilizwa, basi lazima ujue na kusikiliza pia. Leo nitajikita kwenye maeneo mawili, kupongeza na kushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwanza kwa kumpongeza CAG, Profesa Assad kwa uzalendo mkubwa aliouonesha, kwa sababu katika nchi hii watu walianza kutokwa na imani na wasomi wakiwemo maprofesa wetu, lakini kwa hatua alizochukua Prof. Assad recently kwa kweli amerudisha imani kwa wananchi kwamba kunao bado maprofesa ambao wana mapenzi na Taifa hili na wana misimamo yanapokuja masuala ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda nimpongeze Rais kwa kukubali mwaliko wa wafanyakazi Mei Mosi, kuja Mbeya kuwa mgeni rasmi. Pamoja na kwamba anakuja kwenye shughuli ya Kitaifa ya Mei Mosi, lakini Mbeya wanamsubiri sana kwa sababu ni sehemu ambazo alikuwa hajakanyaga kabisa toka awe Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaase wanaoshughulika na ile protocol ya Mheshimiwa Rais wajaribu kuwazuia Chama cha Mapinduzi wasitake au kujaribu kutumia ujio wa Mheshimiwa Rais ambayo ni ziara ya kiserikali kwa maslahi ya chama chao kwa sababu wanaweza wakavuruga ziara ya Mheshimiwa Rais kwa sababu Mbeya ni Cosmopolitan kisiasa, imechanganyika sana. Kuna vyama vyote vinatamalaki pale na viko vyama ambavyo vinazidi idadi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi, hususan Jijini Mbeya.

MHE. GOOLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

KUHUSU UTARATIBU

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbilinyi, kuhusu utaratibu.

MHE. GOOLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Menyekiti, nasimama kwa mujibu wa Kanuni ya 68 kuhusu utaratibu, nikisoma Kanuni ya 64(1) (c) nikisoma pamoja na Kanuni ya 53(8), kuwa Mheshimiwa Mbunge hatazungumzia suala ambalo tayari Bunge lilishafanyia maamuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tangu asubuhi alianza Mheshimiwa Ally Saleh kuongelea suala la CAG, akaja Mbunge mwingine akaongelea tena suala la CAG na sasa hivi Mheshimiwa Sugu. Sisi suala la huyu mtu tayari tulishaliongea kama Bunge na tulishafanya maazimio, lakini bado tu wamekuwa wakijaribu kulifukua kitu ambacho ni kinyume na kanuni zetu. Kwa hiyo, nilikuwa naomba hilo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa umeeleweka. Mheshimiwa Selasini.

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Kanuni aliyotumia siyo. Kanuni ya Utaratibu ni ya 64. Pili, imekuwa ni mazoea Mheshimiwa Mlinga ku-interrupt wasemaji wa Kambi hii kila wanapozungumza na kwa vitu vya ovyo kabisa, kupoteza muda tu. Sasa ningependa kujua, huu ndiyo utaratibu? Au Kambi hii ya Chama cha Mapinduzi imemu-assign yeye ku-interrupt wazungumzaji wa Kambi hii kila wakati?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jenista.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu. Twende tu kwa utaratibu, kwa heshima na Bunge litatuelewa. Yote yanaweza kuwa ni mambo mema, tunataka kupata mfumo mzuri wa kujadiliana hapa ndani, lakini maneno pia anayoyatumia Chief Whip mwenzangu katika kueleza, umesikia sitaki kurudia lile neno alilolitamka hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nafikiria pia tutumie lugha nyepesi, ambazo ni za kibunge, zitatusaidia tu kufuata kanuni na utaratibu utaenda vizuri. Tupunguze kutumia lugha ambazo siyo nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nafikiria lugha ya Chief Whip mwenzangu, hebu apunguze kidogo na ikiwezekana tuiondoe, sitaki kuirudia.

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, naomba tuelewane. Mheshimiwa Mlinga alirekebisha kanuni; alianza 68 lakini baadaye akarudia 64(1); kwa hiyo, alikwenda kwenye utaratibu, lakini jambo ambalo linazungumzwa, Chief Whips wote wawili mko sahihi, tunatakiwa twende kwa mujibu wa utaratibu. Lugha pia tuwe nazo nzuri.

Kuhusu suala la CAG lililozungumzwa, ikiwa mtu anajadili taarifa; na ikiwa mtu anajadili jambo ambalo limeshazungumzwa Bungeni, ni jambo lingine.

Kwa hiyo, twende kwenye utaratibu. Kama tunazungumzia taarifa, tuzungumzie taarifa, lakini tusizungumzie masuala ambayo yamepita Bungeni. Kwa hiyo, tuendelee na utaratibu huo.

Mheshimiwa Mbilinyi naomba uendelee.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, almost naanza hapa, kwa sababu niliongea kwa sekunde 20, kwa hiyo, kwa kuwa nina dakika 10 na nili-keep my watch, nina dakika tisa kama na sekunde kama 40 hivi, ukiondoa tano hizi ambazo nimeongea sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa statement ya ukaribisho kwa Mheshimiwa Rais Jijini Mbeya na hali ya siasa, niendelee kumpongeza na niseme kwamba leo nimesema nitapongeza na kushauri. Masikio ya wafanyakazi na familia zao yote yatakuwa Mbeya Mei Mosi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Wafanyakazi wa Mbeya ambao mimi ni Mbunge wao na Wafanyakazi wa nchi nzima, naomba sasa with respect, nimshauri Mheshimiwa Rais atakapokuwa Mbeya mwaka huu Mei Mosi, atangaze ongezeko la mshahara kwa wafanyakazi. Kwa sababu toka ameingia madarakani huu ni mwaka wa tatu mishahara haijaongezeka hata ndururu na wafanyakazi wana hali mbaya sana katika maeneo yote ya nchi hii na ngazi zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia aangalie suala la wastaafu. Wako wengi sana wamestaafu, wengine mwaka wa pili sasa lakini hawajalipwa mafao yao katika Idara mbalimbali wakiwemo wastaafu kwenye Idara za ulinzi na usalama kama Magereza, Polisi, wamestaafu miaka miwili sasa na hili nilishalisema bado wako kwenye Police Quarter hawaondoki, hawana hata nauli za kubebea mizigo kurudi hata makwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama suala la mishahara haliko kwenye bajeti, Waheshimiwa Mawaziri, naomba safari hii mrudi mezani mwangalie namna gani mtafanya ili basi Mheshimiwa Rais atakapokuja Mbeya atangaze ongezeko la mishahara kwa wafanyakazi wetu nao wapate unafuu wa maisha kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naunga mkono kauli ya Mheshimiwa Rais kuwa Watanzania sio wajinga. Aliongea wakati anamwapisha Mheshimiwa Balozi aliyekuwa anakwenda Cuba. Ni kweli kabisa Watanzania siyo wajinga; na ukitaka kupima, angalia jinsi walivyolipokea suala la CAG baada ya CAG kufanya Press Conference jana Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ujinga aliousema Mheshimiwa Rais kwamba Watanzania sio wajinga, aka-cite suala la MO Dewji kutekwa na maelezo yake ya nini kilitokea, Polisi, uchunguzi ulikwendaje, hewa; hivyo hivyo Watanzania wanajiuliza kuhusu Mheshimiwa Tundu Lissu, wanajiuliza kuhusu Ben Saanane, wanajiuliza kuhusu Azori na watu wengine wote waliopotea. Kwa hiyo, naungana mkono kabisa na Mheshimiwa Rais kwamba Watanzania sio wajinga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niungane na ahadi ya Mheshimiwa Rais aliposema kwamba baada ya kumaliza miaka kumi iwapo atashinda mwakani hataongeza hata saa moja Ikulu. Hili namuunga mkono na asiwasikilize wapotoshaji wanaoleta njaa kwenye masuala ya uongozi wa nchi kwa kumperemba na kutaka kumwingiza chaka kwa sababu Afrika hiyo imeshapita na mifano ipo, nitaisema mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, itapendeza zaidi kama akiahidi kwamba atakuwa tayari kukabidhi madaraka kwa amani mwakani iwapo atashindwa kwenye uchaguzi wa 2020 mwakani. Atoe kauli na siyo tu aahidi kwa maneno, aahidi kwa vitendo kwa kutusaidia kuifumulia mbali Tume ya Uchaguzi kwa sababu Tume ya Uchaguzi iliyokuwepo haikidhi, imejaa makada wa wazi kabisa wa Chama cha Mapinduzi, chama tawala watu wanaovaa uniform za chama kesho wanaenda kusimamia uchaguzi. Uchaguzi huo utavurugika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila Tume Huru, tutaingiza nchi hii kwenye machafuko ya kiuchaguzi kama ilivyotokea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Kenya mwaka 2017. Take my word, wakati tunaanza hili Bunge nilisema humu ndani kwenye briefing, I was worried about the future; I was scared of the future, mkacheka cheka hapa lakini leo everybody sees future imetukaliaje. Sasa tunayo nafasi ya kujirekebisha kuokoa mambo mabaya yanayokwenda kutokea yasitokee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchaguzi wa mwaka 2020 itakuwa siyo mchezo, kwa sababu wananchi wanakwenda kuchagua kati ya taabu na nafuu. Sasa watu wanaochagua kati ya taabu na nafuu, huwezi kuwaletea mchezo. Maisha yamekuwa magumu; wafanyabiashara hoi, wafanyakazi hoi. Huu ni mwaka wa tatu sasa President Dr. Magufuli yuko Ikulu lakini bado analalamika na kutumbua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nimemwangalia kwenye tv akiwa Namtumbo, bado mpaka leo hii nchi hii Rais anakwenda ku-question ujenzi wa shilingi milioni 60 wa zahanati sijui jengo gani kule wakati ameweka timu, ameweka Wakuu wa Wilaya; wote kazi yao ni kumvizia Sugu wamkamate wamweke ndani masaa 48, halafu wanashindwa kusimamia kazi ambazo Mheshimiwa Rais amewachagua wao kufanya hizo kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huu ni mwaka wa tatu Mheshimiwa Rais analalamika, bado anatumbua, timu haijakaa sawa na sasa tunaenda dakika ya 85 kuelekea dakika ya 90. Msaidieni sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nishauri tubadili approach. Masuala ya ukali hayasaidii, turudi sasa kwenye lile suala kama aliloongea Mheshimiwa Japhary…

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHES. JOSEPH O. MBILINYI: …Meya Mstaafu wa Arusha aliposema kwamba…

MWENYEKITI: Taarifa.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Tunahitaji kujenga taasisi imara

MHE. MARWA R. CHACHA: Kaa chini.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbilinyi, taarifa.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: …na siyo kujenga mtu imara.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbilinyi, Mheshimiwa Mbilinyi subiri kidogo, taarifa. Mheshimiwa Chacha.

T A A R I F A

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa, mwongeaji anasema Tume ya Uchaguzi siyo huru. Liliundwa Bunge la Katiba lililokuwa linaunda Tume, wakaunda chombo kinaitwa UKAWA wakaondoka Bungeni. Leo wanataka Tume huru, ipi? (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbilinyi.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, yule nampuuza. Ila acha niseme neno moja, kwa nini Bunge linafika hapa? Angalia hoja muhimu zinazoletwa humu Bungeni, halafu angalia Wabunge wa sasa upande wa CCM wanaochangia. Huwezi kuona Mheshimiwa Chenge kasimama au Mheshimiwa Mwinyi au hata Mheshimiwa Jenista mwenyewe hawezi kusimama kuchangia vitu vya msingi. Wanawaachia mapoyoyo kama yule wavuruge Bunge tu kwa style ya namna hii. (Makofi/Kicheko)[Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee. (Makofi/Kicheko)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbilinyi umeyatafuta haya. Mheshimiwa Jenista.

Mheshimiwa Mbilinyi subiri, Mheshimiwa Jenista.

KUHUSU UTARATIBU

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 64(1) (f) na (g), inakataza kabisa kutumia lugha ya kuudhi na inayodhalilisha watu wengine na hairuhusu kutumia lugha zinazofanana na lugha ya matusi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni zinatutaka humu ndani unapom-address Mbunge mwenzako, utatumia jina lake kwa kumwita Mheshimiwa. Mheshimiwa Mbilinyi anamwita Mbunge mwenzake poyoyo. (Kicheko/Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jenista, malizia.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana hii siyo lugha ya Kibunge. Katika tafsiri ya lugha za Kibunge tulizonazo, hii siyo lugha ya Kibunge. Ni lugha ya kudhalilisha na kuudhi. Tunaomba lugha hiyo aifute na aiondoe kwenye Hansard ya leo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbilinyi, hilo neno hata mimi maana yake siijui, naomba ulifute tu.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uzingatie dakika zangu, bado saba hata kengele ya kwanza haijapiga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tupo kwenye shida kidogo. Angalia ma-RC na ma-DC…

MWENYEKITI: Naomba ufute lile neno.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshafuta. Poyoyo! Nimeshafuta, nitalitumia nje. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia state tuliyokuwepo ma–RC, ma–DC ni vituko kabisa. Angalia yule RC wa Tabora, Mheshimiwa Aggrey Mwanri. Namheshimu sana my brother; anakaa anasema, yeye atamwomba Mungu, Mungu amshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa kazi nzuri. Kweli! That is blasphemy. Hiyo ni blasphemy inaitwa, maana yake kwa Kiswahili ni kufuru. katika baadhi ya maeneo ambayo wako serious na Mungu, Mheshimiwa Aggrey Mwanry sasa hivi angekuwa mahali pabaya sana kwa kufanya blasphemy.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu ni Mkristo, tunamwona Kanisani kila siku, nashangaa hata Mheshimiwa Msigwa, mwandishi wake wa habari hajalaani kitendo kile. Tunaliingiza hili Taifa kwenye laana, namwomba Mungu alihurumie hili Taifa kwa kauli za watu kama akina Mheshimiwa Aggrey Mwanri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mko busy sana kuzuia maandamano. Maandamano ni haki ya Kikatiba watu ku- express, yatawasaidia ninyi wenyewe kujua joto likoje. Hamwezi kuzuia maandamano kwa kutumia Polisi. Yakifika hayazuiliki. Omar Al-Bashir saa hizi siyo Rais. Jana amelala Rais, leo siyo Rais. Amezuia shughuli za vyama vya siasa, amezuia maandamano, amefuta vyama vya siasa kwa miaka 30 akiwa Ikulu ya Khartoum, Sudan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bei ya mkate tu, mwaka 2018 mwishoni kapandisha bei ya mkate tu, watu wameingia barabarani, vyama vya siasa hakuna, haoni mtu wa ku-negotiate naye, ameishia ku-negotiate na Jeshi, Jeshi limemwambia kaa barracks, hatuwezi kupiga risasi watu, imetosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mtafanya mbinu kuzuia maanadamano, mtafanya nini; yatakapofika mama! Kumbuka Algeria. Yule jamaa, yule mzee na ni wapambe tu. Mzee wa watu, Bouteflika, ana miaka 82, amechoka yuko kwenye wheel chair, wapambe wanalazimisha aongeze muda, agombee ili wao wabaki kwenye nafasi, kama wanavyofanya baadhi ya watu hapa sasa hivi kuanza kumwambia President Dr. Magufuli, eti aongeze muda sijui aongeze miaka saba kwa maslahi yao binafsi. Hiyo Afrika imepita, tutapata taabu sana. Namwomba sana Mheshimiwa Rais asisikilize huo upuuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)