Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii. Kwanza namshukuru Mungu na pia nishukuru Wabunge wote kwa salamu za pole mlizotupatia wakati tulipofiwa na mama yetu mzazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nipongeze Serikali kwa kazi kubwa ambayo wamefanya na pia Waziri, Mheshimiwa Jafo, unafanya kazi kubwa sana pamoja na mzee wangu Mheshimiwa Mkuchika, unatumikia vyema chini ya Ofisi ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niguse suala dogo ambalo alikuwa anachangia rafiki yangu Mheshimiwa Heche kuhusiana na Mkuu wa Mkoa kuingilia kati utendaji wa Halmashauri katika Jimbo lake. Ukienda kwenye sheria, wanaotumia Wakuu wa Mikoa, The Regional Administration Act, 1997 kipengele cha 5(3) naomba ninukuu, “For the purpose of this section it shall be the duty of the Regional Commissioner to facilitate and assist local government authorities in the region to undertake and discharge their responsibilities by providing and securing the enabling environment for the successful performance by them of their duties and functions.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa ndio mwakilishi wa Rais katika Mkoa na sheria imempa mamlaka ya kuingilia ili kuona kwamba performance ya Halmashauri inafanyika. Kwa hiyo, kitendo kilichofanyika ni chema na Halmashauri yake inapata service levy kutoka kwenye mgodi 1.5 billion. Wanapata corporate social responsibility shilingi bilioni tano. Kwa hiyo, kama kuna hali ya kifisadi ambayo imefanyika na tume iliundwa, kwa hiyo, ni sahihi kuhakikisha kwamba anadhibiti matumizi ya fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya suala hilo, naomba niingie kwenye suala letu la Mkoa wa Katavi. Bajeti ya TARURA…

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. RICHARD P. MBOGO: Bajeti ya TARURA…

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. RICHARD P. MBOGO: …tumepangiwa shilingi bilioni 3.6.

MWENYEKITI: Taarifa.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe…

MHE. RICHARD P. MBOGO: Tumepangiwa shilingi bilioni 3.6.

MHE. JOHN W. HECHE: Samahani tuvumiliane. Nina haki ya kutoa taarifa.

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hiyo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbogo, tafadhali dakika moja.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Tusikilizane. Mheshimiwa Mbogo, subiri. Sasa nyie mnaongea, huyu mtu anatoa taarifa.

MHE. RICHARD P. MBOGO: Bado ni ndogo sana bajeti hiyo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbogo, subiri kidogo.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, umenipa nafasi ya kutoa taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche ongea wewe siyo wenzako. Wewe ndio unatakiwa utoe taarifa.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimetulia nakusikiliza wewe.

MWENYEKITI: Haya sema hiyo taarifa.

T A A R I F A

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni hii; na iwe very clear. Sisi hatujakataa Mkuu wa Mkoa kuchunguza, kufanya chochote kwenye Halmashauri. Tunachokataa ni kuzuia vikao vya wananchi vi-deliberate kwenye issues za maendeleo ya wananchi. Ndicho tunachokataa. Hana sheria inayompa mamlaka hayo ya kuingilia na kujigeuza Pay Master General, hakuna sheria inasema hivyo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbogo, taarifa hiyo.

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vikao vinakaa halafu havitendi haki ipasavyo, akizuia ni sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee, muda wangu naomba uulinde, utanipa na bonus.

MWENYEKITI: Endelea.

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia kuhusu TARURA; kwa Mkoa wa Katavi tumepangiwa bilioni 3.6, ni fedha ambayo haitoshi. Tuna mtandao wa barabara kilometa 2,563 lakini ambazo zilihakikiwa na ile tume ni kwenye 2,400 na kitu, tofauti ni ndogo sana. Hata hivyo, katika mtandao huu kilometa 24 ndiyo ni lami ambayo ni asilimia moja, kilometa 511 ambayo ni asilimia 20 ndiyo barabara ya changarawe na kilometa 2,027 ambayo ni asilimia 79 katika Mkoa mzima wa Katavi ni za udongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto hii ya ufinyu wa bajeti ambayo tunatengewa Mkoa wa Katavi, naomba sana Mheshimiwa Waziri Jafo na watendaji wa TARURA na kama wako humu ndani naomba walichukue hili; randama hii wakaiboreshe watuongezee iwe angalau bilioni tano. Kwa sababu Mkoa wa Katavi tunatunza mazingira, tuna mvua nyingi tunapeleka maji Ziwa Tanganyika, Ziwa Rukwa na kadhalika, sasa barabara hizi kipindi cha masika hazipitiki. Kwa hiyo tunaomba tuongezewe toka bilioni 3.6 ifike angalau bilioni tano. Ilishangaza sana, kuna halmashauri karibuni 11 zinazidi mkoa mzima, kwa hiyo tunaomba suala hili Mheshimiwa Waziri Jafo na timu yake na watendaji wa TARURA walifanyie kazi, bajeti sio Biblia, bajeti sio Msahafu inaweza ikaboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni kuhusiana na mapato kwenye halmashauri zetu. Halmashauri za Mkoa wa Katavi, Halmashauri ya Nsimbo ambayo tunalima tumbaku pamoja na Chunya, kampuni za ununuzi wa tumbaku zimegoma kutulipa tozo kutokana na kudai fedha zao za marejesho ya VAT (VAT refund). Kwa hiyo, tuombe kama wahusika wa Wizara ya Fedha na wa TAMISEMI watusaidie ili tuweze kupata fedha na tutekeleze miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la utawala bora; hii Sheria ya Regional Administration Act ya 1997 imewapa madaraka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuweza kutoa amri ya kumkamata mtu. Kuna wakati mwingine utekelezaji wake umekuwa hauendani na sheria inavyosema. Niombe Waziri wa Utawala Bora pamoja na Serikali kiujumla na tunajua muda mrefu semina zimetolewa, mafunzo na maonyo mbalimbali kwa watendaji wetu watekeleze sheria hii ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mfano mzuri, naomba ku-declare kabisa, nina mzee wangu anaitwa Ernest Wamryoma alikamatwa tarehe 24, Machi akiwa anatetea ardhi yake aliyoshinda Mahakama Kuu ya Ardhi na Mahakama Kuu ya Ardhi Kikatiba, Ibara ya 107A(1) ndiyo chombo chenye kutenda haki. Kwa hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mheshimiwa Sara Msafiri hajamtendea haki mzee Ernest Wamryoma kwa kumyanyasa na ameshinda Mahakama Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Lukuvi, katika masuluhisho yake ya matatizo ya ardhi huwa anasema jambo lolote ambalo limeamuliwa na mahakama lisiletwe kwenye ofisi yake. Sasa niombe Waziri, Ofisi ya Rais suala la Utawala Bora, naomba asaidie Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni aache kumsumbua huyu mzee, kashinda Mahakama Kuu na aliyemshinda alikuwa amemkaribisha tu, aache mahakama ambavyo imekwishaamua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Uchaguzi wa Vijiji na Serikali za Mitaa mwaka huu. Sasa kwa Nsimbo tuna Makazi ya Wakimbizi ya Katumba, tuombe mtoe mwongozo jinsi gani ambavyo kutokana na hadhi ya makazi ipo Katumba, Mishamo na Ulyankulu, namna gani uchaguzi wa vijiji utakwenda kufanyika na tuna sheria ya upande wa Wizara ya Mambo ya Ndani kuhusiana na wakimbizi ambapo tayari bado maeneo haya yako chini yao. Kwa hiyo tuombe tupate mwongozo jinsi gani uchaguzi utakwenda kufanyika kwenye maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na madeni ya watumishi; ukiangalia hesabu za halmashauri utakuta kuna receivable, wanadai na kuna payable wanadaiwa na watumishi kutokana na maslahi yao mbalimbali, hususan uhamisho na madaraja waliyopanda. Kwa hiyo tuombe watumishi wetu katika halmashauri Serikali itoe fedha ili waweze kulipwa malimbikizo yao ambayo yapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni kuhusiana na uchangiaji wa jana wa kaka yangu, Mheshimiwa Mchungaji Msigwa, alizungumzia consequences kwenye SGR, kwenye ndege, kwenye Stiegler’s Gorge. Uwekezaji wowote una return on investment; Air Tanzania ita-promote utalii na kuanzia baada ya miaka minne ijayo itakuwa inafanya kwa faida, hizo ndiyo positive consequences. Kwenye SGR tutakwenda kunyanyua uchumi wa nchi yetu kwa kubeba mizigo toka kwenye nchi za jirani ambazo ni landlocked; Burundi, Rwanda, Kongo na Zaire. Kwa hiyo uchumi wa nchi utaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye umeme, umeme wa maji ndiyo umeme ambao ni nafuu kuliko umeme wowote duniani. Naibu Waziri wakati anajibu swali la gesi kaeleza gharama ya gesi ni dola 5.1, kwa hiyo utaona jinsi gani kwamba umeme wa gesi uko juu kuliko ambavyo utakuwa umeme wa maji. Kwa hiyo consequences za maamuzi ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imeyafanya ni positive kwa ajili ya wananchi wake na maendeleo ya taifa kiujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. (Makofi)