Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba mbili; TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora. Nianze kwa kuunga mkono hotuba hizi lakini naomba uniruhusu ninukuu kutoka kitabu cha Mithali 15:2 inasema kwamba: “Ulimi wa mwenye hekima hutamka maarifa vizuri; bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu”. Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mwenyezi Mungu anisaidie nitumie ulimi wa mwenye hekima katika kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya ndani ya nchi hii. Nampongeza Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wasaidizi wao kwa kazi kubwa ambayo wameendelea kuifanya katika nchi hii.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwambie akae chini.

MWENYEKITI: Kuhusu utaratibu na msiingie na uchochoro wa utaratibu.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasimama kwa mujibu wa Kanuni ya 64(1)(e). Tunapenda kuitumia Kanuni hii lakini labda ama waliyoitunga hawakuitunga vizuri au hatuielewi. Kanuni inasema: “Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ya 100 ya Katiba inayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika Bunge, Mbunge, (e) hatazungumzia mwenendo wa Rais…”

MWENYEKITI: Hebu, rudia Kanuni ya 64 ngapi?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 64(1)(e).

MWENYEKITI: Endelea.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, inasema kwamba: “Mbunge, hatazungumzia mwenendo wa Rais, Spika, Mbunge na kuendelea.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, humu ndani tumekuwa tukizungumzia mwenendo wa Rais. Tofauti yetu sisi upande na huu na upande ule, huku tumekuwa tukizungumzia mwenendo wa Rais ambao tunaona una upungufu na wale wanazungumzia mwenendo wa Rais wanaoona hauna upungufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukabaliane na Kanuni ya 64(1)(e) kwamba ama wote tusizungumzie mwenendo wa Rais au kila mtu azungumzie mwenendo wa Rais kwa kadri anavyoona. Kwa mtazamo wangu naona Kanuni hii inakiukwa. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Soma Kanuni ya 68(10).

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 68(10) inasema: “Uamuzi wa Spika kuhusu suala lolote la utaratibu utakuwa ni wa mwisho.”

WABUNGE FULANI: Aaa, sasa mmeamua nini?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo?

MWENYEKITI: Ndiyo, uamuzi wa Spika ni wa mwisho.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Sikilizeni jamani, hizi Kanuni hazisomwi kama unasoma gazeti, zinasomwa kwa mtiririko.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Kaa chini, endelea Mheshimiwa.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naona mwanangu alikuwa ananipotezea muda tu lakini naendelea kuwaambia kwamba wananchi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaridhika na utendaji wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Kwa kuthibitisha hayo, wananchi wa Korogwe wanaridhika na mwenendo mzima wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi unaofanywa na Serikali hii kwa sababu tumeletewa fedha kwa ajili ujenzi wa vyumba vya madarasa, mabweni, za matengenezo ya barabara kwa kiwango cha changarawe na kiwango cha lami na za kumalizia maktaba katika chuo cha ualimu, kwa nini wasiwe na imani na Serikali ya Chama cha Mapinduzi? Naendelea kuwaombea viongozi wetu hawa Mwenyezi Mungu aendelee kuwapa afya njema ili waendelee kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ujenzi wa vituo vya afya, Korogwe Mjini tulipata Kituo cha Afya kimoja cha Majengo. Tunashukuru tulipata shilingi milioni 500 lakini niombe na Mwenyezi Mungu ikiwezekana aendelee kuwapa afya njema mkipata fedha muweze kunisaidia niweze kupata Kituo cha Afya Mgombezi, tuweze kupandisha Zahanati ya Mgombezi iwe Kituo cha Afya. Kule Mgombezi ni nje ya Mji wa Korogwe na kuna mashamba ya mkonge, wananchi wengi wako kule, ni vijiji sita viko pale Mgombezi. Kwa hiyo, tukiwapa kituo cha afya kitawasaidia wao katika matibabu kwa sababu akina mama wajawazito na watoto wanapopata shida usiku ni shida sana kwenda Mjini. Kwa hiyo, wakipewa Kituo cha Afya kule Mgombezi itawasaidia kupata huduma kwa urahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika, nina Kata ya Kwamsisi, iko nje ya mji, ni mbali na Kituo cha Afya cha Majengo na Hospitali ya Magunga. Nao napenda Mwenyezi Mungu akijalia basi niombe angalau waweze kupata fedha kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya kule Kwamsisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Waziri wa TAMISEMI, bajeti iliyopita walinipa shilingi bilioni 1.5 nijenge hospitali. Kwa bahati nzuri au mbaya hospitali ambayo ilikuwa ya Korogwe Vijijini iko kwenye Jimbo langu, mkasema hiyo hospitali ibaki mjini wakapewa zile fedha ambazo nilikuwa nimetengewa mimi kwenye Halmashauri yangu ya Mji wa Korogwe. Wenzangu wanajenga hospitali, hospitali ile ambayo imebaki sasa ni ya mwaka 1947, naomba sana muweze kuikumba hospitali hii angalau kupewa fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo hayo makuukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba mmetupa fedha tumefanya ukarabati wa shule kongwe ya Korogwe Girls, majengo yanapendeza lakini kwa bahati mbaya sana jengo moja la bweni limeshindikana kabisa kukarabatiwa kwa sababu lina nyufa kubwa ambapo Mhandisi amesema halitawezekana kabisa kufanyiwa ukarabati lijengwe moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa watoto waliokuwa wanakaa kwenye bweni lile ni 120 wamehamishiwa kwenye mabweni mengine, wamesambazwa huko, niombe basi ikiwezekana na Naibu Waziri wa Fedha alifika akaona lile jengo, tupewe fedha ili tuweze kujenga jengo jipya la bweni pale Korogwe Girls ili kusudi wale watoto waweze kurudi kwenye lile bweni lao kama walivyokuwa wanakaa mle. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie masuala ya watumishi, lipo tatizo la watumishi kupandishwa madaraja halafu hawalipwi zile fedha zao baada ya kuwa wamepandishwa yale madaraja. Niombe wanapopandishwa madaraja watumishi hawa basi fedha zao walipwe.