Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Rehema Juma Migilla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipata nafasi nami jioni hii nichangie hotuba iliyopo mbele yetu. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa nanyi jioni hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuwashukuru wanachama wa Chama cha Wananchi CUF, kwani kwa kupitia wao kwenye Mkutano wetu wa Saba tumeweza kumchagua Mheshimiwa Prof. Ibrahim Haruna Lipumba kuwa Mwenyekiti wetu mpya. Hakika wana-CUF tunaweza na Mheshimiwa Prof. Lipumba ndiyo Mwenyekiti wetu halali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja, naomba nijielekeze kwenye mada na nitajikita kwenye suala la upandishwaji wa mishahara ya watumishi wa umma. Ni ukweli ulio wazi kwamba tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani watumishi hawa wa umma hawajaweza kuongezwa mshahara wao. Itambulike kwamba annual increment ni takwa la Kikatiba kwa mujibu wa Standing Order lakini watumishi hawa wa Tanzania kwa miaka mitatu mfululizo hawajaongezwa mshahara kama Katiba inavyosema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tujue ni lini sasa Serikali yetu itawaongeza mishahara hawa watu ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu na wanafanya kazi pasipo motisha wa aina yoyote? Nataka niiulize Serikali, kwa sababu kupandishwa mishahara ni takwa la kisheria, je, iko tayari sasa kuwapa mishahara yao kwa mkupuo ambayo wame-delay kuwapa kwa miaka mitatu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nataka nijikite kwenye vitambulisho vya wajasiriamali. Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alitoa vitambulisho 670,000, lengo ikiwa ni kuwatambua hawa wajasiriamali wadogo lakini pia ni kuwatafutia mahali ambapo watafanyia biashara zao pasipo kubughudhiwa kwa aina yoyote. Mimi sikudhani kama hili lilikuwa ndiyo hitaji lao haswa la kuwatambua hawa wafanyabiashara ns wajasiriamali wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya nikiwa na sababu kwamba wafanyabiashara hawa kwanza wanatakiwa walipe Sh.20,000 ambayo baadhi yao ni kubwa mno. Unamkuta mama anauza mbogamboga, mtaji wake ni Sh.3,000 lakini unamtaka mjasiriamali huyu mdogo alipe Sh.20,000 anaitoa wapi? Hata kama tunataka tuongeze mapato siyo kwa namna hii. Nashauri Serikali ifanya tathmini itambue, je, hawa wajasiriamali wadogo wanahitaji kutambuliwa au wanahitaji mitaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba lengo ni kuwatambua na kuwatafutia mahali pa kufanyia biashara wafanyabiashara wadogo lakini bado maeneo ya kufanyia biashara hawana, wanatembea hovyo na bado huko mitaani wakitembea wanasumbuliwa na Mgambo, bado watendaji wetu huko wanawasumbua. Kwa hiyo, niiombe Serikali sasa iweze kutumiza lengo lake la kuwatambua, lakini pia waweze kuwatafutia mahali pa kufanyia biashara ili waweze kufanya biashara kama wafanyabiashara wengine. Kama itawezekana, hii Sh.20,000 ni kubwa sana, tunaiomba Serikali hawa wafanyabiashara wapunguziwe iweze kuendana na mitaji yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni upandishwaji wa vyeo na madaraja kwa wafanyakazi especially walimu. Suala la kupandishwa madaraja kwa walimu sasa hivi limewekewa masharti magumu sana. Leo hii walimu wanaambiwa watapandishwa madaraja kwa kuangalia bajeti ya Serikali, lakini pia wataangalia Performance Appraisal ya huyu mwalimu na uwezo wa Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua wazi kabisa vyanzo vingi vya mapato vimechukuliwa na Serikali Kuu, baadhi ya Halmashauri hazina vyanzo vya mapato vya kueleweka. Kwa hiyo, kama hizi Halmashauri hazina vyanzo, leo tunawaambia hawa wafanyakazi watapandishwa kwa kuangalia bajeti ya Halmashauri, ni lini hawa walimu sasa au Halmashauri zitaweza kujikidhi mpaka ziweze kuwapandisha hawa walimu madaraja? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema Performance Appraisal, kazi ya mwalimu ni kufundisha lakini suala la kusema kumpima kwa kuangalia wanafunzi wamefaulu kwa kiasi gani, hilo suala halimhusu mwalimu. Hivi vigezo vilivyowekwa kwa ajili ya kumpandisha huyu mtumishi naomba viangaliwe kwa jicho lingine tena kwa sababu ni kumbana mwalimu na kumpotezea haki zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuangalia posho za Wenyeviti wa Mitaa na Vitongoji. Kama walivyosema wenzangu, hawa Wenyeviti wa Mitaa na Vitongoji ndiyo viongozi wa kwanza katika maeneo yetu. Hawa watu wanasumbuliwa usiku kucha, watu wakipigana huko na wake zao kwa Mwenyekiti wa Mtaa, mtu amekosea njia, amepotea anakwenda kwa Mwenyekiti wa Mtaa, amlishe na amfanyie kila kitu lakini mtu huyu hana posho wala kitu chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilimsikia Mheshimiwa Waitara pale anasema ni kazi za kujitolea na wawe na shughuli nyingine. Kama Serikali imepanga hadi bajeti ya kuweza kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ina maana tunawatambua hawa watu lakini leo hii tunasema ni kazi ya kujitolea. Kama ni kazi ya kujitolea basi kulikuwa hakuna haja ya kutenga hata bajeti kwa ajili ya uchaguzi wa kuwachagua viongozi hao. Naiomba Serikali iwatambue watu hawa, wao ndiyo wanafanya kazi kubwa na ndiyo hata sisi tunapopatia kura zetu huko. Naomba tuwaangalie hawa watu kwa jicho la tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni elimu bure. Suala hili ni zuri sana, kwanza limeweza kusaidia watoto wa kimaskini waweze kwenda shule kwa wingi lakini pia wazazi wamepunguza baadhi ya gharama kwa elimu bure. Hata hivyo, hili suala la elimu bure haliendi sambamba na uongezekaji wa miundombinu. Sasa hivi asilimia ya wanafunzi itakuwa ni kubwa sana lakini miundombinu ni ile ile, madarasa yale yale na matundu ya vyoo yale yale. Kama tutakuwa tunajisifu tu tuna elimu bure ilhali tunachofanya pale ni kuongeza idadi ya wanafunzi lakini quality education haipo. Ili tuweze kupata quality education ni lazima basi hii elimu bure iende sambamba na ongezeko la wanafunzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kumekuwa na matatizo sana sasa hivi wanafunzi wengi wamechelewa kuanza kidato cha kwanza kwa sababu madarasa hayakuwepo na ndiyo maana wadau wengi wa elimu wamejishirikisha kwa njia moja au nyingine kuhakikisha madarasa yanapatikana. Niiombe Serikali kama kweli tunataka kuboresha elimu yetu, tutumie takwimu za maoteo, takwimu zipo zinafanya kazi gani? Kama kweli takwimu zinafanya kazi leo Serikali ingekuwa haina mzigo wa kujua wilaya fulani kuna upungufu wa madarasa ama nini, ni kwa sababu tu hizi takwimu za maoteo hazitumiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni TASAF. Tunaelewa kabisa kwamba TASAF ni mpango wa kunusuru kaya zilizo maskini na mradi huu ni mradi unaofadhiliwa na mashirika ya nje ya nchi lakini nachokiona kwenye TASAF bado hatuna nia ya dhati kabisa ya kuwasaidia hawa watu wa kaya maskini. Unakuta pesa anayopata mtu wa Dar es Salaam ni sawasawa na anayopata mtu Ulindwanoni huko Kaliua. Tuelewe kabisa kwamba tuna lengo la kuzisaidia hizi kaya maskini lakini hizi kaya maskini ziko maeneo tofauti na zina mahitaji tofauti. Kama tunawapa pesa ambayo inatolewa kwa kiwango kile kile, kwa maeneo tofauti, tunakuwa hatufanyi sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Dar es Salaam …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)